Wimbo wa Sulemani 1:5-6
Mimi ni mweusi, lakini ninao uzuri, enyi binti za Yerusalemu, Kama hema za Kedari, Kama mapazia ya Sulemani. Msiniangalie kwa kuwa ni mweusi, Kwa sababu jua limeniunguza.
Kimsingi hakuna mzungu anaekua mweusi kwa kukaa juani ila mtu mweusi akikaa juani ndio anazidi kuwa mpingo.
Ayubu 30:30
Ngozi yangu inakuwa nyeusi juu yangu, Na mifupa yangu inateketea kwa sababu ya hari.
Ayubu anasema ngozi yake ilikuwa nyeusi juu yake kutokana na mateso aliyokuwa akipitia, mzungu au mtu mweupe kiasili achana na hawa weupe wa kiafrika, hawawezi kuwa weusi hata wapitie shida kiasi gani zaidi wanakua wekundu tu.
Kutoka 4:6-7
Bwana akamwambia tena, Ingiza mkono wako kifuani mwako. Akauingiza mkono wake kifuani mwake; hata alipoutoa, tazama, mkono wake umekuwa na ukoma, mweupe kama theluji. Akasema, Uurudishe mkono wako kifuani mwako. Akauingiza tena kifuani mwake; kisha akautoa kifuani mwake, na tazama, ukawa umegeuka tena, ukawa kama mwili wake mwingine, hili andiko liko wazi na linaonesha jamaa mwili wake haukua mweupe na badala yake alikua na rangi ya giza.
Kwa maana kama Musa alikuwa mweupe tayari, basi hili lisingekuwa jambo la kushangaza, lakini kwakua alikuwa na ngozi ya giza, ndio maana badiliko hili lilikuwa la kushangaza, likiashiria kuwa ngozi yake ya asili ilikuwa na rangi tofauti.
Ufunuo 1:14-15
Kichwa chake na nywele zake zilikuwa nyeupe kama sufu, kama theluji; na macho yake yalikuwa kama mwali wa moto. Na miguu yake ilikuwa kama shaba iliyosuguliwa sana, kana kwamba imesafishwa katika tanuru; na sauti yake ilikuwa kama sauti ya maji mengi.
Hapa utaona neno sufu limetumika na kimsingi hili neno sufu huwa linahusiana na muundo wa nywele za waafrika.
Lakini pia andiko linasema na miguu yake inafanana na shaba iliyosuguliwa sana, wote tunajua ya kwamba shaba ina rangi ya kahawia iliyokolea au ya dhahabu yenye giza, kwahiyo tafsiri hii inaonesha ya kwamba Yesu hakuwa na ngozi nyeupe ila alikua na eidha rangi ya kahawia(kama ile ya kiethiopia au ngozi nyeusi)
Pia nenda kapitie Yeremia 13:23, ambayo inasema hivi…
Mweusi aweza kuibadili ngozi yake, Au chui madoa yake? Kama ndivyo, ndipo mwaweza kutenda mema, Ninyi mliozoea kutenda mabaya.
Yeremia anatumia mfano wa mweusi kuonyesha kitu ambacho hakiwezi kubadilika.
Sasa ikiwa watu wa Israeli walikuwa weupe, kwa nini Yeremia anatumia mfano wa mtu mweusi ili kuonyesha utofauti wa wazi.
Nenda kwenye Waamuzi 16:13-19
Samsoni alikuwa na nywele saba zilizofungwa (locks), hii inamaanisha nywele zake hazikuwa laini bali zilikua ngumu kama zilivyo zangu kwa maana nywele laini za kizungu ni ngumu kujifunga kwenye mashungi saba kwasababu ya ule mtelezo wake.
Hesabu 12:10-12
Wingu likatoka juu ya hema; na tazama, Mariamu alikuwa na ukoma, mweupe kama theluji; Haruni akamwelekea Mariamu, na tazama, alikuwa na ukoma. Haruni akamwambia Musa, Ee bwana wangu, nakusihi, usitutie dhambi hii juu yetu, kwa kuwa tumefanya upumbavu, nasi tumekosa. Nakusihi, asiwe kama mfu, ambaye nyama ya mwili wake huwa tayari imeshakula mara atokapo tumboni mwa mama yake.
Kama huyu Mariamu angekua mweupe basi sidhani kama haya mabadiliko ya ngozi yake yangeweza kushangaza lakini pia ingekua ngumu kuyaona mabadiliko haya kwenye ngozi ya mtu ambae ni mweupe.
Mathayo 27:32, Marko 15:21, Luka 23:26
Kwenye hizo Aya tunaona maandiko ya mtu aitwae Simon wa Kirene ambae alilazimishwa kubeba msalaba wa Yesu kwa maana ya kumpokea. Kwa wana history wanajua ya kwamba Kirene eneo ambalo ilikuwa koloni la Kigiriki lililoko kaskazini mwa Afrika kwa sasa ndio Libya na eneo hilo lilikuwa na mchanganyiko wa watu, lakini lilikuwa na idadi kubwa ya waafrika weusi.
Hesabu 12:1
Kisha Mariamu na Haruni wakanena juu ya Musa, kwa sababu ya yule mwanamke Mkushi aliyemwoa; maana alikuwa amemwoa mwanamke Mkushi.
Mkushi inahusiana na Ethiopia, ambayo kihistoria imekuwa na watu wa asili ya Kiafrika. Hii inaashiria kwamba mke wa Musa alikuwa mweusi, na wakati huo huo tulishaona hapo awali ya kwamba hata Musa nae hakuwa mweupe kwahiyo hii combo haiwezi kuzaa mtu mweupe hata siku moja.
Matendo 21:38.
Je! Wewe si yule Mmisri, ambaye kabla ya siku hizi alifanya fitina, akawatoa wale watu elfu nne wa hao wenye kuua waliokuwa jangwani?
Hapa ni Warumi walimchanganya Paulo na Mmisri, Misri ni Afrika, na Wamisri wa kale walikuwa na rangi ya giza au kahawia(hakuna mwana historia anayebisha hili). Kwahiyo kutokana na andiko hili kuna uwezekano kwamba Paulo alikuwa na rangi sawa na Wamisri wa wakati huo.
Lakini pia kwenye historia ya Yusufu tunaona baada ya kuangukia Misiri na kuwa mtu mkubwa pale kisha ndugu zake walivyokuja kununua chakula hawakumtambua ila yeye aliwatambua hii inamaanisha kwamba rangi ya Yusufu haikua na utofauti wowote na rangi ya wamisri kwa maana hakuwa anaonekana wa tofauti.
Anyway, mifano iko mingi yenye kuonesha utata wa rangi halisi za watu wa kwenye biblia ingawa ukiwa muelewa lazima utaelewa ya kwamba biblia ilizungumzia watu wenye rangi fulani hivi ya kahawia au nyeusi ila si rangi myeupe kama ambavyo watu wanadhani au kuamini.