Mabadiliko ya siasa nchini Tanzania kuanzia mwaka 1967 ndiyo yalisababisha kusimama kwa uchumi wa taifa. Operesheni vijiji vya ujamaa ilisababisha watu kuondolewa kwa nguvu kutoka kwenye makazi yao na mashamba yao, walikusanywa kwenye maeneo mapya yenye wanyama wakali bila nyumba wala chakula. Watanzania hawa walianza maisha mapya kwa kuanza kujenga nyumba kufyeka na kusafisha mapori na kuanza kulima, hali hii ilichukuwa miaka mingi na kipindi hiki ndicho ambacho tatitizo la ukosefu wa chakula lilianza.Wakulima walitoka vijijini kutafuta chakula mijini.
Tatizo la pili lilikuwa ni kutaifisha mabenki, bima, viwanda nyumba na mashamba ya walioitwa mabwenyenye, makabaila n.k. kutaifisha maana yake ni kuchukua mali ya mtu kwa nguvu bila ya ridhaa yake na bila kumlipa kitu chochote. Matokeo yake mashamba ya mkonge yaligeuka mapori, kwa sababu bei ya mkonge ambao ndio wakati huo ulikuwa ukiingiza fedha nyingi za kigeni iliporomoka. Magonjwa ya ajabu ajabu alianza kushambulia kahawa, nayo mavuno yakapungua kwa kiwango cha kutisha. Serikali ilifika wakati ikaliona tatizo lakini ilishindwa kusema ukweli kwa wale wote ambao mali zao zilichukuliwa. Badala yake serikali ilianza kuwaalika kama wawekezaji na siyo tena mabwenyenye. Tukumbuke kuwa kosa lolote baya likifanyika kinachofuata ni kujitakasa kwa toba kwa wale wote ambao serikali iliwapora mali zao. Ni kweli wawekezaji walianza kuja nchini, tunakumbuka walivyochukua benki ya NBC watanzania tulipiga kelele nyingi jinsi walivyoichukua kwa bei ya kutupa. Lakini jambo moja la msingi ni kuwa kibaka akipora mkufu wa dhahabu atauza kwa bei yoyote atakayokuja nayo mnunuzi. Hizi benki hazikuwa zetu tulipora mali za watu na kinachofanyika sasa hivi tunauza kwa staili ile ile ya vibaka. Raisi wetu kila siku ni kiguu na njia akizungukia dunia kutafuta wawekezaji, sawa tunaowapata ndio kama akina buswagi. Bila toba kwa dhambi iliyofanywa na awamu ya kwanza, kwa kukaa na wale wote walioporwa mali zao na kukubali kosa na kuomba msamaha na kukubali kulipa fidia angalau kidogo ni hakika hatasimama kiongozi yeyote katika taifa hili akabadilisha maisha ya watanzania, bila ya kuondoa hii dhuluma taifa la Tanzania lililowafanyia mabwenyenye na makabaila.