Jeshi la Polisi Mkoa wa Kusini Unguja limeanza kufanya uchunguzi zaidi kuhusu tukio la Msimu Jaffari (33), kudaiwa kuchoma moto gari ya mumewe, ambaye wiki iliyopita alitoa taarifa ya kuongeza mke wa pili katika ndoa yake.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Unguja, Suleiman Hassan alithibitisha kutokea kwa tukio hilo. Kesi hiyo imeripotiwa katika Kituo cha Dunga Wilaya ya Kati Unguja.
Kamanda Hassan alisema tukio hilo, limeripotiwa mwishoni mwa wiki huko Kitumba Wilaya ya Kati Unguja. Gari aina ya Spacio inayomilikiwa na Abdallah Hijji (43) ilitiwa moto usiku.
Mke wa kwanza wa mtu huyo, anatuhumiwa kufanya tukio hilo. Alisema taarifa za awali katika uchunguzi uliofanywa na Jeshi la Polisi, unaonesha kwamba Hijji alitoa taarifa kwa familia na mkewe wake wa kwanza, kwamba anakusudia kuongeza mke wa pili.
‘’Uchunguzi uliofanywa na Jeshi la Polisi katika hatua za awali unaonesha kwamba tukio hili linahusishwa na wivu wa kimapenzi, ambapo mume alimjulisha mkewe nia ya kuoa mke wa pili na kama unavyojua wanawake wengi hawapendi ukewenza. Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi zaidi ili kujiridhisha na ukweli halisi wa tukio hilo,’’ alisema.
Uchunguzi zaidi uliofanywa na gazeti hili, kwa kuwahoji watu mbalimbali huko Kitumba, umeonesha kwamba Hijji aliongeza mke wa pili wiki iliyopita. Hatua hiyo ilimtia hasira mke wa kwanza, ambaye kabla ya ndoa hiyo alikuwa akitoa tahadhari kwa mumewe, kwamba asithubutu kuoa mke mwingine.
‘’Huyu mwanamke hataki ukewenza, kwa muda mrefu amekuwa akimuonya mumewe asijaribu kufanya kitu hicho na akifanya atajuta,’’alisema jirani ya Hijji, Haji Omar ambaye alidai amekuwa akishuhudia mara kwa mara ugomvi wa watu hao.
Jeshi la Polisi limesema uchunguzi utakapomalizika, jalada la kesi hiyo litapelekwa Ofisi ya Mkurugenzi wa mashtaka (DPP) kwa hatua zaidi.
Chanzo: HabariLeo