Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi, imemuachia huru Padre Sosthenes Soka (42), baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha shitaka lililokuwa likimkabili pasipo kuacha shaka.
Katika kesi hiyo ya jinai namba 44 ya mwaka 2022, ambayo upande wa Jamuhuri uliwakilishwa na wakili Julieth Komba na upande wa utetezi uliwakilishwa na wakili Silayo Edwin, Soka alikuwa akisthakiwa kwa kosa la ubakaji na ulawiti kwa mtoto mwenye umri wa miaka 12 katika Kanisa alilokuwa akihudumu, kosa ambalo alidaiwa kulitenda Agosti, 2022.
Akisoma hukumu hiyo leo Septemba 22, 2023, Hakimu Mkazi Mfawidhi, Jenipha Edward, amesema upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha shitaka dhidi ya mshtakiwa pasipo kuacha shaka yoyote kwa sababu upande wa utetezi wameweza kuibua mashaka ambayo yalikosa majibu kutoka kwa mashahidi upande wa mashtaka.
Amesema ushahidi wa mhanga pia umeibua mashaka juu ya ukweli wa kile alichokiongea mahakamani kwa sababu ushahidi huo ulikuwa una utofauti kati ya ushahidi wake uliotolewa kwanza na ushahidi wa mashahidi wengine wa upande wa mashtaka uliotolewa mahakamani. "
Lakini pia upande wa utetezi uliibua hoja ya kutokuwepo katika eneo la tukio katika tarehe husika ambayo ni Agost 26, 2022 na Septemba 9,2022 ambapo walifuata taratibu za kuleta notisi ya utetezi huo na pia walileta mashahidi na vielelezo vya kuthibitisha hilo mahakamani," amesema Hakimu Edward.
Amesema pia ushahidi wa mhanga alioutoa mahakamani ulikuwa tofauti na maelezo aliyoyatoa polisi ambapo yalitumika mahakamani kama ushahidi kwa upande wa utetezi. "Kulikuwa na tofauti ya ushahidi wake mwenyewe alioutoa mahakamani, lakini pia kulikuwa na tofauti baina ya ushahidi wake na mashahidi wa mashtaka na kulikuwa na tofauti baina ya ushahidi wake na maelezo aliyotoa polisi," amesema.
Aidha amesema upande wa mashtaka pia umeshindwa kuleta mashahidi muhimu wa kuthibitisha kama tarehe hizo mshtakiwa alikuwepo eneo la tukio na kama kweli mhanga na yeye alikuwepo. (Imeandikwa Flora Temba)
mwananchiupdates