Kuhusu kwenda nje na viza ya kutalii halafu usirudi nyumbani
Viza ya kutalii ni viza ya muda mfupi, mara nyingi huwa kati ya miezi 3 hadi 6. Viza hii haikuruhusu kufanya kazi wala kusoma. Unaweza kupata viza hii kwa kuwa na uwezo wa kifedha au kwa kupata mwaliko wa mkaazi halali wa nchi unayotaka kwenda.
Kuna mtindo wa watu kutumia viza hii kama njia ya kuingilia nchi za Ulaya na Marekani halafu baadae 'kujilipua' ama kuishi chini kwa chini.
Zoezi zima la kujilipua polisi na kuomba ukimbizi ni suala la bahati nasibu ambayo kwa asilimia kubwa huwa watu wanarudishwa nyumbani na kupigwa marufuku ya muda mrefu ya kutembelea nchi hiyo. Kutokana na wimbi la wakimbizi la miaka ya karibuni, imekuwa ni vigumu kupata hifadhi kama mkimbizi. Unaweza kuwa Msomali lakini ukanyimwa hifadhi sababu mji ulipotoka Somalia hakuna vita. Mchakato huu huwa unachukua miaka mingi na katika kipindi hiki nchi nyingi haziruhusu ufanye kazi.
Kuishi chini kwa chini. Hapa watu huwa wanaishi nchi fulani bila vibali (hawana makaratasi). Kutokana na nchi zote zilizoendelea kuwa na namba za utambulisho, huwezi kupata ajira rasmi wala kusafiri ukiwa katika hali hii. Unaweza ukapata kazi (maarufu kama black job) lakini mwajiri wako atakulipa mshahara mdogo mno ambao haukidhi mahitaji ya kila siku. Ukifanya kazi hizi, hulipi kodi, huchangii pensheni wala huna haki zozote kama wafanyakazi wengine halali. Watu wa aina hii ndio mara nyingi inapita miaka mingi bila kurudi nyumbani maana hawawezi kusafiri.
Katika kipindi hiki cha miezi 3 au 6 ya viza ya utalii, unaweza ukabahatika kupata mwanamke akakusaidia kupata makaratasi kwa njia ya ndoa. Pia, ni ngumu kwa mwajiri yeyote kukuajiri kama ukiwa na viza ya utalii, usitegemee kupata kazi ukiwa na viza hii.
Viza ya utalii ya Schengen
Hii viza inakuwezesha kutembelea nchi yoyote kati ya nchi wanachama wa makubaliano hayo. Viza hii haikuruhusu kufanya kazi wala kusoma. Unaweza ukaangalia orodha ya nchi za Schengen hapa
Schengen Area Countries List - Schengen Zone