Elimu hapo ndipo penye tatizo kubwa sana. Mpaka leo hatujui lengo lake hasa ni nini. Mkakati mama katika ukombozi wa binadamu (kama ilivyofanya kwa wenzetu huko) sisi tumeigeuza kuwa ni chombo cha kufanyia uhuni wa kiuchumi na hata kisiasa ili tutajirike tusichekwe na jamii. Ati elimu yetu hii, dhima yake hasa ni nini? Tunaitaka ituzalishie watu wa aina gani?
Sisi ni lab. Wanakuja kufanyia majaribio kwetu hawa jamaa. Kwa mfano tumeletewa hii demokrasia ya Kimagharibi. Hatujui hata maana yake kwa sababu haikuwa kwenye utamaduni wala historia yetu. Hata kwenye jamii haimo. Matokeo yako karibu bara zima dhana hii inatupa shida sana.
Demokrasia ya maana ni lazima izingatie utamaduni na historia ya jamii. Ndiyo maana demokrasia hii ya Kimarekani imeshindikana sehemu nyingi duniani hata ilikopelekwa kwa nguvu kama huko Uarabuni. Demokrasia na mifumo mingine kama elimu inapaswa itokane na jamii yenyewe. Matokeo yake ni vurugu tupu na siamini kama hii tuliyonayo Afrika ndiyo demokrasia yenyewe. Hao tunagombana na hata kuuana. Wanakuja wapya madarakani wanafanya madude yale yale miaka nenda miaka rudi na bara zima liko pale pale linapiga makitaimu. Ni kwa sababu hii mimi huwezi kunikuta nikishabikia hizi siasa uchwara za Afrika kwa sababu najua hata aje nani kama mifumo yetu bado ni ile ile hakuna cho chote kitakachobadilika.