Uzi maalum wa kupeana Likes: Comment chochote upate "Like"

YALIYO NIFIKA NAFSI YANGU NA HAYO YENYE KUITWA "MAPINDUZI"
Kiasi cha saa 12 za magharibi siku ya Jumaatatu taarikh 13 Januari 1964, siku ya pili ya hayo yenye kuitwa 'mapinduzi', mimi pamoja na mke wangu na chungu ya wananchi wenzetu wa kike na wa kiume, wakubwa na wadogo, tulikuwepo katika klabu ya wazee wa Kingazija "Comorian Club" iliyokuwepo Kisiwandui, Unguja. (klabu hiyo kwa wakati huo, wakuu wa mavamizi waliifanya kuwa ni miongoni mwa vituo vya wakimbizi).
 
Ghafla tulisikia mlango ukigongwa kwa vishindo vikubwa na baada ya kufunguliwa, tuliwaona vijana watatu wametuingilia, wawili walikuwa wamechukua bunduki na mmoja alikuwa na bastola, huyu alikuwa ni Mzanzibari, kwa jina ni Ahmed Bushir Aboud na hao wenzake walikuwa vijana wa Kibara. Kwanza waliwachukua, Sheikh Ameir Tajo na Sheikh Ali Ahmed Riyami na baada ya muda walirejea na walinichukua mimi (Aman Thani) na Sheikh Mohammed Aboud Mkandaa. Wote hao wenzangu wameshafika mbele ya haki. (Mungu awape malazi mema, Amin). Safari yetu hiyo ilimalizikia katika jumba la Raha Leo (Civic Centre) Miafuni
 
Jumba hilo kwa siku hizo za mavamizi, 36 lilifanywa ndio Makao Makuu ya Wavamizi. Mbele ya uwanja wa jumba hilo, tulikuta umati wa watu mkubwa sana na kila mmoja alikuwa na silaha mkononi mwake. Wengine walikuwa na mabunduki, wengine walikuwa na mapanga, mashoka, mishale, na mipinde pamoja na mikuki. Wengine walikuwa kama ni vichekesho kwani walikuwa wamejiremba marangi mwilini mwao na wamejizongeresha majani na magozi, na huku mtu mmoja huyo huyo amechukua bunduki mkono mmoja, panga mkono wa pili na upinde ameuvaa shingoni na mishale ameichomeka kiunoni.
 
Ndani ya hilo jumba la Raha Leo, kulikuwa kumejaa watu, wake kwa waume wakubwa kwa wadogo hata vitoto vichanga, pamoja na mama zao, hao pia walichukuliwa kutoka majumbani mwao na kuletwa hapo ati kwa usalama wao. Kitendo hichi kilithibitisha kuwa majumba yetu kuanzia wakati huo yalikuwa hayana tena usalama. Mimi pamoja na mwenzangu Mohammed Aboud Mkandaa, tulipelekwa ndani ya jumba hilo na huko tulitengwa upande. Katika upande huo tuliotengwa sisi, tuliwakuta, Sheikh Issa Mohammed Issa Barwani, Sheikh Mwinyi Nemshi na Sheikh Omar Mohammed aliyekuwa Katibu wa Umoja wa Vijana, "Youth Own Union".
 
Muda mdogo baada ya kuwekwa hapo, alikuja kijana mmoja ambaye mpaka wakati huu nilionao sijaweza kumtambua ni nani, kwani sikumbuki maisha yangu kuwa nimepata angalau kukutana naye pahala. Kijana huyo alinitaka nisimame na kiasi cha kusimama tu, alinipiga kofi la uso, niliona vimuri muri na baada ya hapo alinitesa kwa kunipiga makonde na mateke na kunipopotoa kila sehemu aliyokuwa ameipenda. Baadae aliamuru ninyanyue mikono juu na hapo alimpa amri mwenzake ambaye alikuwa na bunduki kwa kumwambia,
"Muangalie huyu asiteremshe mikono yake chini mpaka nitapokuja mimi. Na ikiwa atateremsha, basi mpige risasi".
 
Nilibakia katika hali hiyo kwa muda mkubwa mpaka yule kijana aliyeachiwa kuniangalia, alinionea huruma na aliniachia kwa kiasi cha muda fulani kuiteremsha chini mikono yangu. Haya yote yanathibitisha kuwa misingi ya hayo mavamizi ilikuwa ni chuki na idhlali kwa wananchi. Baada ya muda walitujia, Comrade Ali Mahfoudh na Comrade Badawi Qulatain na walitutaka mimi, Sheikh Mohammed Aboud Mkandaa, Sheikh Issa Mohammed Issa na Sheikh Mwinyi Nemshi tuwafuate
 
Walituongoza, Ali Mahfoudh akiwa mbele na Badawi akiwa nyuma na sisi tukiwa katikati mpaka nje ya jumba; na hapo tulitiwa ndani ya gari aina ya "pickup" kubwa (Lori) na tulifuatanishwa na walinzi wanane, wote wakiwa na bunduki, na wote pamoja na dereva wetu walikuwa wamelewa. Hao walinzi waliwauliza mabosi wao, "Hawa wa wapi?" Comrade Ali Mahfoudh alijibu, "Wapelekeni Kilimani".
 
MAAFA YA GEREZANI
Tulifika katika Gereza la Kiinua Miguu, ambalo sasa linaitwa, Chuo cha Mafunzo, kiasi cha saa nne za usiku na hapo tulimkuta Comrade Hemed Hilal Barwani, ambaye yeye ndiye aliyekuwa na dhamana ya gereza hilo kwa wakati huo. Comrade Hemed Hilal alitutaka tuvue nguo zetu zote, na tulizivua na tukabaki kama tulivyotoka matumboni mwa mama zetu. Hakuweza kumwekea sitaha hata mzee wake, Sheikh Issa Mohammed Issa Barwani.
 
Baada ya kwisha kusachiwa, Comrade Hemed Hilal alitoa amri tupelekwe kwenye vyumba vya "security" vya kuwekewa mahabusi. Tulipewa virago vya kulalia, (kirago ni kizulia cha usumba urefu wake kiasi cha futi nne mpaka tano na upana wake ni kiasi cha futi mbili mpaka tatu) shuka mbili za bafta na kopo la kunywia maji, uji na kunawia baada ya kwenda haja ndogo au kubwa, ndio hilo hilo.

Baada ya kupewa vitu hivyo, tuliongozwa na sajin wa gereza mpaka katika hivyo vyumba. Mimi na Sheikh Mohammed Aboud Mkandaa tulitiwa katika chumba kimoja na Sheikh Issa na Sheikh Mwinyi Nemshi walitiwa katika chumba kimoja. Sehemu hiyo ilikuwa na vyumba sita, kila upande vyumba vitatu na katikati ujia. Tulifungiwa kwa kufuli, lango la nje pia lilitiwa kufuli.
 
Baada ya kuondoka huyo sajin aliyetupeleka, tulisikia sauti ikitoka katika chumba kimoja ikiuliza, "Ni nani wenzangu mliyoletwa"? Sauti ilikuwa si ngeni kwetu lakini kwa mughma tuliyokuwa nao wakati huo, tulishindwa kuitambua. Tulimuuliza kwani wewe ni nani mwenzetu?

Alitujibu, "Mimi Suleiman Said Kharusi, na chumba chengine yumo Sheikh Humoud Ali Harthi, na chumba chengine yumo Sheikh Mohammed Idi Mjasiri, na chumba cha mwisho yumo mwanangu Edi Kharusi". (Mohammed Ali Said Kharusi) Na mimi nilimjibu, "Mimi Aman Thani, na mwenzangu Sheikh Mohammed Aboud Mkandaa, tumo katika chumba cha pili mkono wa kulia kutokea mlangoni". "Na wenzetu wawili, Sheikh Issa Mohammed Issa Barwani na Sheikh Mwinyi Nemshi, wao wametiwa katika chumba cha mwisho katika mkono huu 37 huu wa kulia."

 
Tukiambizana kwa sauti tu si kwa kuonana. Ndani ya chumba tuliwekewa ndoo mbili. Moja ndio choo na ya pili ya maji ya kunywa. Tuliwekwa katika vyumba hivyo kwa muda wa wiki mbili bila ya kutolewa nje hata dakika moja. Ndoo za uchafu zikitolewa na wachungaji, na chakula tukiletewa na wachungaji.
 
Wakati huo kila sehemu ya kuwekewa wafungwa katika gereza hilo ilikuwa imejaa wananchi waliokuwa wameletwa humo ati kwa kuhifadhiwa maisha yao. Kwa jinsi umma ulivyokuwa mkubwa, Serikali ya Mavamizi iliwaachilia wafungwa wote hata waliyokuwa wamesha hukumiwa vifo, nao pia waliachiliwa huru ili ipatikane nafasi ya kuwekwa hao ati wenye kuhifadhiwa! Chumba (cell) kilichokuwa kwa kawaida wakiekwa wafungwa sita mpaka wanane, walitiwa baina ya watu 12 mpaka 16 na juu ya hivyo, bado wengine walikuwa wakilala katika vijia vya kupitia
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…