Tuuangalie mambo kwa muktadha wa hadithi.
Kuna mtu alikuwa akiitwa bwana Msafiri aliishi kale , kabla ya sayansi na teknolojia kushika hatamu.
Bwana Msafiri alikuwa anataka kutoka Magogoni kwenda Kigamboni, aende sehemu inaitwa Mjimwema kuanzisha makao mapya sehemu yenye nafasi zaidi.
Sasa, alivyofika Magogoni, akakutana na maji. Akasema hapa siwezi kuogelea, itabidi nipate msaada wa wenyeji kuvuka kwa mtumbwi. Hakuna jinsi.
Akakubaliana na wenyeji wamsaidie avuke kwa mtumbwi kutoka Magogoni mpaka Kigamboni.
Baada ya kuvuka, wale wenyeji wakamwambia, ili uweze kusafiri kwa salama huko mbele, ambako hatukujui vizuri na unaweza kukutana na mto , inakubidi uuchukue huu mtumbwi uubebe. Ukikutana na mto mwingine, uweze kuvuka kwa mtumbwi. Hivyo tutakuuzia huu mtumbwi. Popote unapoenda, usiuache kamwe.
Bwana Msafiri akakubali. Akaununua ule mtumbwi, akaubeba. Mtumbwi ulikuwa mzito sana, na Msafiri hakujua kama huko mbele kutakuwa na mto mwingine au hakutakuwa na mto. Ila, akaona ni bora aubebe mtumbwi tu, kwa kuwa hawezi kubahatisha kwenye suala muhimu kama hili.
Baadaye akafika Mjimwema. Akajua kuwa baada ya kuvuka kuja Kigamboni, hapo mbele kuja Mjimwema hakuna mto. Akamaliza shughuli zake. Akapapenda Mjimwema na kuhamia huko.
Basi Msafiri akawa kila akitoka nyumbani kwake, lazima atoke na mtumbwi kaubeba, akawa anasafiri hivyo, miaka nenda, miaka rudi. Hata akirudia njia ambayo alishaijua na haina mto, aliamua kuubeba tu mtumbwi, maana alisema "Huwezi kujua, mambo yanaweza kubadilika, ni bora kuwa salama kwa kubeba mtumbwi".
Watu wakimuona wakawa wanamwambia, wewe bwana Msafiri, kwa nini unaubeba mtumbwi huu kila unapoenda? Shida yako nini?
Msafiri akiwajibu, "Huwezi kujua siku utakayohitaji kuvuka maji, hivyo ni bora ubebe mtumbwi".
Wale jirani zake Msafiri wakawa wanamcheka, wengine waliomhurumia wakawa wakimwambia, siku hizi kuna magari, kuna pantoni, kuna madaraja yamejengwa, inawezekana zamani ulivyokuja Kigamboni ulihitaji kutembea na mtumbwi, lakini, siku hizi huhitaji. Unaweza hata kupanga safari yako kwa kuangalia ramani kwenye mtandao, ukajua barabara zote utakazopita.
Msafiri alikuwa ni mtu mwenye kung'ang'ania alichokijua tangu utoto wake, hakutaka kubadilika, hakutaka kujifunza mambo mapya. Aling'ang'ania kutembea na mtumbwi wake popote alipokwenda. Alikataa hata kupanda gari akisema kuwa mtumbwi wake ni bora kuliko gari.
Matokeo yake, Msafiri alidhoofika sana kutokana na kutoweza kusafiri mbali, kutokana na kushindwa kufanya shughuli nyingi za kiuchumi. Kazi ya kubeba mtumbwi kila sehemu ilimfanya apate kibiongo. Zaidi, watoto walimcheka na kumjaza sonona. Kila alipoenda aliitwa kichaa. Yeye alijigamba kwamba yeye ni kati ya watu wa kwanza kukaa Mjimwema, na yeye ndiye mtunza utamaduni, na anaweza kutembea mbali huku kabeba mtumbwi wake bila ya msaada wa gari.
Baadaye Msafiri alikufa mapema kabla ya umri wa wastani wa kufariki, kwa sababu ya shurba za kubeba mtumbwi kila alipokwenda.
Wengi waliusema ujinga wake wa kutaka kubeba mtumbwi kila alipokwenda kuwa ni sababu kubwa iliyomtia umasikini na kifo cha mapema.
Waliobaki wakamtungia nyimbo na kumuandikia historia kukumbushana juu ya maisha ya Bwana Msafiri.