Wadau wa Jukwaa heshima kwenu.
Kwa niaba ya Shirika linalojihusisha na Utalii Tanzania -TANAPA pamoja na Bodi ya Utalii-Tanzania. Kuwaletea hii platform hapa Jamiiforums itakayohusiana na mambo ya utalii, ili kuhamasisha zaidi utalii wa ndani.
Karibu pia Utushirikishe sehemu ambayo uliwahi kutembelea ndani ya nchi yetu na ikavutia sana. Au kama ulikutana na changamoto yoyote iseme. Nakaribisha pia Maoni, Mapendekezo na ushauri kuhusiana na mambo ya utalii. Nawakaribisha sana, kama utakuwa na swali lolote! Litapatiwa ufumbuzi.
Karibuni Wote.
Tanzania ni nzuri yenye vivutio vya kila aina.
Baadhi ya vivutio ambavyo vinasimamiwa kikamilifu na Shirika la Hifadhi za Taifa la Tanzania (TANAPA) ni pamoja na hifadhi ya Taifa ya Arusha, Gombe, Katavi, Mlima Kilimanjaro, Mahale, Mikumi, Manyara, Ruaha, Rubondo, Serengeti, Saadan, Tarangire, Udzungwa, Kitulo, Mkomazi na Saanane.
Na Kuna hifadhi nyingine mpya Tatu ambazo ni Hifadhi ya Nyerere (Selous), Hifadhi ya Kigosi na Hifadhi ya Mto Uggala.
Hapa chini nitakuletea sifa za Hifadhi moja hadi nyingine.
1.Hifadhi ya Taifa ya Arusha(Arusha National Park)
Hifadhi ya Taifa ya Arusha kuwa ina ukubwa wa kilomita za mraba 328.4, iko umbali wa kilomita 62 (kiasi cha mwendo wa saa moja kwa gari) kutoka mji wa kitalii wa Arusha.
‘’Hifadhi hii ina maeneo matatu muhimu ambayo ni bonde la Ngurdoto (Ngurdoto Crater), maziwa ya Momella ambayo kila moja hutoa mandhari tofauti pamoja na Mlima Meru wenye urefu wa mita 4566 (futi 14990), hali ambayo inaifanya hifadhi kuwa na mazingira ya baridi’’ anasema Mbugi.
Ikumbukwe kuwa hifadhi hii ni maarufu kwa wanyama jamii ya tumbili wajulikanao kama Mbega weusi na weupe. Wanyama wengine wanaopatikana katika hifadhi hii ni pamoja na Twiga,pundamilia, Nyati na digidigi.
Unaweza kuwaona Chui wakibarizi katika vivuli vya matawi ya miti inayokingwa na maaguko ya maji huku makundi kadhaa ya batamaji yakitafuta wadudu katika maziwa ya Momella.
Zaidi ya aina 400 za ndege wamethibitika kupatikana ndani ya hifadhi hii. Safari za miguu na kupanda milima Meru ni moja ya burudani muhimu katika hifadhi ambapo mpandaji anahitaji kati ya siku 3-4 za kupanda mlima.
Wakati mzuri wa kutembelea hifadhi hii ni kati ya mwezi Juni na Februari ingawa mvua inaweza kunyesha mwezi Novemba. Kuna maeneo ya malazi ndani ya hifadhi yenye hadhi tofauti tofauti kama hoteli, nyumba za wageni na makambi ya kupuga mahema ingawa wageni pia wanawezakupata malazi eneo nje ya hifadhi katika mji wa Usa River na Arusha mjini.
2. Hifadhi ya Mahale
Hifadhi hi inaundwa inaundwa na vilima vilivyojipanga na kufunikwa na misitu minene ikiwa na jumla ya kilomita za Mraba 1613. Kama ilivyo hifadhi ya jirani ya kaskazini ya Gombe, hifadhi ya milima ya Mahale ni makazi ya jamii adimu zilizobakia za sokwe barani Afrika.
Mabaki ya matunda yaliyoliwa na kinyesi kibichi ni miongoni mwa alama zitakazokuongoza mgeni hadi kuwafikia viumbe hawa katika misitu iliyopo katika mlima huo na hifadhi hii ipo Maharibi mwa Tanzania ikiwa inapakana na Ziwa Tanganyika.
Ukifika hapo utaona na sehemu ya asili ya watu wa kabila la Watongwe walipokuwa wakiaabudia mizimu yao milimani, kisha kurudi ziwani na kujitumbukiza kwenye maji baridi na maangavu.
Wakati mzuri wa kutembelea hifadhi hii ni kipindi cha kiangazi, kati ya mwezi Mei na Octoba.
4.Gombe
Hifadhi ya Taifa ya Gombe ni ndogo kuliko zote nchini ikiwa na jumla ya kilomota za mraba 52 lakini ina umaarufu mkubwa unaotokana na kuwa na wanyama aina ya Sokwe.
Gombe ni moja ya makzi ya machache yaliyosalia ya Sokwe duniani. Ipo kilomita 16 kaskazini mwa mji wa Kigoma, hifadhi hii ni ukanda mwembamba wa msitu wa mlima unaokatizwa na miteremko mikali inayoingia katika mwambao mwa Ziwa Tanganyika.
Wanyama wengine wanaopatikana katika hifadhi hii ni pamoja na Kima wenye mikia myekundu na kima wa rangi ya bluu na wale wanyama jamii ya Paka hawapo katika hifadhi hii kama vile Simba na Chui hivyo kuifanya kuwa salama kwa safari za miguu.
Unaweza kwenda kutembelea hifadhi hii kwa ndege za abiria au za kukodi kutoka Dar es Salaam hadi Kigoma mjini na baadaye kwa boti mpaka makao makuu ya hifadhi, kadhalika kuna huduma za treni kutoka Mwanza na Dar es Salaam pamoja na barabara itokayo Mwanza, Mbeya na Dar es Salaam.
Wakati mzuri wa kutembelea hifadhi hii ni wakati wa kiangazi, Julai mpaka Octoba kwani Sokwe hawapendi kutembea nyakati za mvua.