Sheikh nafikiri usingekuwa unakutana na hoja za watu kudai kwamba wewe ni Mdini kama makala zako zingebeba uwiano kwenye mizani ya makala yako, sidhani kama harakati za kupigania uhuru zilifanywa na waislamu pekee ingawa sikatai kwamba kwa miaka ya 1950s ukanda wa pwani ulijaa waisilamu lakini katika TANU kuna viongozi wengi tu wa dini na imani tofauti walipata kuwepo. suala la kitabu chako kuwepo mwaka wa 21 sasa na kufikia toleo la 4 ni jambo jema na linaloonesha kinakubalika na najua unafahamu vizuri wanunuaji wakubwa wa hicho kitabu ni watu wenye imani na dini fulani unayoifahamu.
Samurai...
Tatizo ni kuwa historia ya TANU inawatisha lakini Uislam ulitumika sana wakati wa kudai uhuru.
Kwa kuwa naona hili limekuwa somo ambalo halijulikani nimeamua kutoa darsa maalum ili liwe msingi wa kuielewa historia ya uhuru wa Tanganyika kama ilivyokuwa:
DARSA NO. 1
Dini ilivyotumika kuwaunganisha watanganyika dhidi ya ukoloni sehemu ya kwanza: Mwanzo wa harakati 1950
Utangulizi
Nami nasubiri patulie In Shaa Allah nataka niandike jinsi Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alivyochaguliwa kuongoza harakati za kupigania uhuru wa Tanganyika katika kikao cha watu watatu Nansio, Ukerewe nyumbani kwa Hamza Kibwana Mwapachu mwaka wa 1953 na moja ya sifa kubwa iliyotajwa ni dini yake. Wazalendo hao wote watatu waliokubaliana kumkabidhi Baba wa Taifa uongozi walikuwa Waislam, mmojawapo akiwa Katibu wa Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika (Umoja wa Waislam wa Tanganyika).
Kisha nitaeleza vikao vyote vya dua alivyoshiriki Baba wa Taifa pamoja na Waislam katika kumlilia Allah awape msaada Watanganyika washinde dhulma zote za Waingereza na Allah alikubali dua ya wenye kudhulumiwa.
***
Mwaka wa 1950 uongozi wa TAA ulikuwa chini ya Dr. Vedasto Kyaruzi kama Rais na Abdulwahid Sykes akiwa Katibu na ikaundwa TAA Political Subcommittee (Kamati ya Siasa ya TAA) iliyokuwa na pamoja na Rais na Katibu, wajumbe hawa wafuatao: Sheikh Hassan bin Ameir aliyekuwa Mufti wa Tanganyika, Sheikh Said Chaurembo, Hamza Mwapachu, Steven Mhando na John Rupia,
Katika kipindi hiki cha mwaka wa 1950 Abdul Sykes alikuwa katika majadiliano na Chief David Kidaha Makwaia akimtaka aingie TAA wamchague kuwa rais kisha waunde TANU yeye akiwa rais wadai uhuru wa Tanganyika.
Kwa kuwa hapa tunazungumza nafasi ya dini katika historia ya uhuru wa Tanganyika napenda kueleza kuwa Chief David Kidaha Makwaia hakuwa Muislam ingawa alikuwa mtoto wa Chief Makwaia Mohamed Mwandu.
Wakati huu Abdul Sykes alikuwa mmoja wa viongozi wa Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika (Umoja wa Waislam wa Tanganyika) lakini hili halikuingia katika fikra zake katika kumtaka Chief Kidaha Makwaia kuongoza harakati za kudai uhuru wa Tanganyika na uhuru ukipatikana awe Waziri Mkuu wa Kwanza wa Tanganyika.
Juhudi hizi hazikufanikiwa.
Mwaka wa 1951 Waingereza walimpa uhamisho Dr. Kyaruzi na kumpeleka Jela ya Kingolwira, Morogoro kisha wakamuhamishia Nzega.
Hamza Mwapachu yeye akahamishiwa Nansio, Ukerewe na yote hii nia ya Waingereza ilikuwa kuivunja nguvu TAA Makao Makuu, New Street kudhoofisha juhudi za kuunda chama cha siasa.
Mwaka wa 1952 Mwalimu Julius Nyerere alipelekwa kwa Abdul Sykes na Joseph Kasella Bantu.
Wakati huu Abdul Sykes alikuwa Kaimu Rais wa TAA na Katibu.
Picha hizo hapo chini aliyevaa kitenge ni Chief David Kidaha Makwaia, Hamza Kibwana Mwapachu, Abdulawahid Kleist Sykes, Mufti Sheikh Hassan bin Ameir na aliyefunga kilemba cha Ki-Omani ni Chief Makwaia Mohamed Mwandu wa Siha.
Itaendelea...
DARSA NO. 2
DINI ILIVYOTUMIKA KUWAUNGANISHA WATANGANYIKA DHIDI YA UKOLONI SEHEMU YA PILI: UJIO WA MWALIMU JULIUS NYERERE DAR ES SALAAM 1952
Joseph Kasella Bantu ndiyo alimchukua Mwalimu Julius Nyerere kutoka Pugu na kujanae nyumbani kwa Abdul Sykes Mtaa wa Stanley na Sikukuu kuja kumtambulisha.
Kupitia kwa Abdul Sykes Nyerere akajuana na watu mashuhuri wa mji na wenyeji wa Dar es Salaam.
Mapenzi makubwa yalijengeka baina ya Nyerere na Abdul Sykes na ndugu zake wawili Ally na Abbas ambae wakati ule alikuwa kijana mdogo.
Kufikia mwaka wa 1953 kuelekea uchaguzi wa TAA Abdul tayari alikuwa keshauona uwezo wa Mwalimu Nyerere kama kiongozi na jina la Nyerere lilitawala mazungumzo baina ya Hamza Mwapachu na Abdul Sykes.
Shajara za Abdul Sykes za nyakati hizi zipo nyingine zimeandikwa kwa hati za kawaida na nyingine kwa hati mkato bahati mbaya shajara hizi hazijatolewa hadharani kwa watafiti kuzisoma na mwandishi ingawa aliziona hakupewa idhini ya kusipitia lakini ni wazi zitakuwa zimejaa mengi katika viongozi kama Chief Kidaha Makwaia na Julius Nyerere waliotegemewa kuongoza mapambano ya kudai uhuru wa Tanganyika.
Nalisema hili kwa kuwa katika nyaraka zingine zipo taarifa za wanasiasa wengi kama Dr. Wilbard Mwanjisi, Dr. Michael Lugazia, Ali Migeyo na Rashid Kawawa kwa kuwataja wachache.
Miezi michache kabla ya uchaguzi wa TAA uliokuwa ufanyike mwezi Aprili, 1953 Abdul Sykes akiongozana na Ali Mwinyi Tambwe aliyekuwa Katibu wa Al Jamiatul Islamiyyya fi Tanganyika walikwenda Nansio kuonana na Hamza Mwapachu.
Abdul Sykes alikuwa anataka apate kauli ya mwisho kutoka kwa Hamza kuhusu jambo ambalo walikuwa wakilizungumza kuanzia mwaka wa 1950 nalo lilikuwa kuunda TANU na kudai uhuru wa Tanganyika.
Abdul alimuuliza Hamza Mwapachu kama msimamo wake bado ni ule ule kuwa yeye ampishe Nyerere kwenye nafasi ya urais wa TAA na mwaka unaofuatia, 1954 waunde TANU kama chama cha ukombozi kudai uhuru wa Tanganyika.
Ilikuwa muhimu kwa Abdul kumkubaii Nyerere kwani Nyerere alikuwa mgeni na hakuna aliyemjua Dar es Salaam kwa hiyo ikiwa Abdul atagombea nafasi ya rais ambayo alikuwa akikaimu toka mwaka wa 1951 kwa nia ya kupata ushindi, kwa umaarufu wake Nyerere hatoweza kumshinda Abdul Sykes.
Hamza Mwapachu alimwona kati ya Abdul na Nyerere, Nyerere alifaa zaidi katika kuongoza harakati za kudai uhuru chini ya chama cha TANU kuliko Abdul.
Zaidi, Nyerere alikuwa na shahada ya pili kutoka Chuo Kikuu Cha Edinburgh, Uskochi.
Lakini kubwa ambalo Hamza Mwapachu alisema kumwambia Abdul yalikuwa maneno haya, ''Abdul wewe ni Muislam na sisi tunakabilliana na Waingereza katika kudai uhuru wa nchi yetu. Ikiwa wewe utaongoza harakati hizi inaweza zikachukuliwa hizi kama vurugu za Waislam dhidi ya Waingereza. Nyerere ni Mkristo, Waingereza hawatotishika na Nyerere katika hili.''
Vita Vya Maji Maji vilikuwa bado viko katika kumbukumbu ya vijana wanasiasa wa wakati ule ambapo katika vita vile Waislam walikuwa mstari wa mbele.
Unyama ambao wananchi wa Tanganyika walifanyiwa na Wajerumani baada ya vita vile ulikuwa bado uko katika kumbukumbu mbaya sana katika historia ya nchi.
Majemadari zaidi ya 60 wa vita vile wengi wao Waislam walinyongwa na kuzikwa kwenye kaburi moja.
Hakuna aliyetaka ijengeke picha kuwa Waislam walikuwa wanjikusanya upya kwa mara ya pili kuoambana na Waingereza na hapa ndipo ilipoingia dini ya Nyerere.
Fikra ya Hamza Mwapachu ilikuwa dini ya Nyerere haitakuwa tishio kubwa kwa Waingereza.
Kazi iliyotakiwa ni kwa Abdul kuhakikisha kuwa Nyerere anashinda uchaguzi wa mwaka wa 1953 na mwaka wa 1954 wanaunda TANU na kuanzia hapo kazi itakayofuata ni kuwahamasisha wananchi wote wa Tanganyika kummunga mkono Nyerere, TANU na harakati za kudai uhuru.
Nyerere alipita kwa shida sana uchaguzi ule uliofanyika Ukumbi wa Arnautoglo tarehe 17 Aprili, 1953.
TAA ilipata viongozi hawa wafuatao hapo chini:
J. K. Nyerere, Rais, Abdulwahid Sykes, Makamu wa Rais; J. P. Kasella Bantu, Katibu Mkuu; Alexander M. Tobias na Waziri Dossa Aziz, Katibu wa pamoja wa muhtasari; Wajumbe wa Kamati: Dr Michael Lugazia, Hamisi Diwani, Tewa Said Tewa, Denis Phombeah, Z. James, Dome Okochi, C. Ongalo na Patrick Aoko.
Picha hapo chini ni Dome Budohi, Joseph Kasella Bantu na Julius Nyerere.
DARSA NO. 3
DINI ILIVYOTUMIKA KUWAUNGANISHA WATANGANYIKA DHIDI YA UKOLONI SEHEMU YA TATU: KUUNDWA KWA TANU 1954
Chama cha TANU asili yake ni African Association iliyoasisiwa mwaka wa 1929 na mwaka wa 1948 African Association ikabadili jina ikawa Tanganyika African Association (TAA).
Mwaka wa 1933 Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika ikaasisiwa na ikasadifu kuwa waasisi wa chama hiki cha Waislam Kleist Sykes na Mzee bin Sudi walikuwa pia katika uongozi wa African Association.
Ikawa sasa viongozi wa African Association ndiyo wale wale viongozi wa Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika na hii ndiyo sababu TANU ilipoasisiwa rais wake wa kwanza Julius Nyerere akajikuta amezungukwa na watu wa dini moja.
Lakini hii haikuwa tatizo kwani wakati wa ukoloni hapakuwa na ubaguzi baina ya wananchi kwa kubaguana wenyewe kwa wenyewe kwa misingi ya dini na hii ndiyo sababu kubwa ya Baba wa Taifa Julius Nyerere kuweza kuchaguliwa kwanza kuwa rais wa TAA mwaka wa 1953 kisha rais wa TANU mwaka mmoja baadae na wale waliomchagua wengi wao walikuwa Waislam.
Katika mazungumzo ya Nansio ya kupata kiongozi wa kuongoza harakati za kudai uhuru katika ya Abdul Sykes, Ali Mwinyi Tambwe na Hamza Mwaochu, rai aliyotoa Hamza Mwapachu ilikuwa Nyerere atakuwa kiongozi muafaka kwanza katika macho ya Waingereza na pili katika kuwavuta wasio Waislam kuiunga mkono TANU kwa kuwa ingawa wanachama wengi walikuwa Waislam lakini chama kilikuwa kinaongozwa na kiongozi ambae hakuwa Muislam na hili iitajenga umoja wa Waafrika wa Tanganyika.
Wanachama wa mwanzo wa TANU walitafutwa kutoka Rufiji sehemu ambayo wakazi wake walikuwa wengi wao ni Waislam.
Mwalimu Nyerere alipokwenda kusajili TANU, aliulizwa kama anayo rejesta ya wanachama na kwa bahati mbaya haikuwapo.
Alipokwenda kumfahamisha Abdul Sykes tatizo hili, Abdul alimuomba Said Chamwenyewe aende Rufiji akatafute wanachama.
Hivi ndivyo ikawa kuwa wanachama wa mwanzo wa TANU walipatikana kutoka Rufiji ambako Mufti Sheikh Hassan bin Ameir kama Khalifa wa Tariqa Qadiriyya alikuwa na murid (wafuasi) wengi.
Makao Makuu ya TANU New Street kulikuwa na Baraza la Wazee wa TANU ambalo baraza zima wajumbe wake 120 walikuwa Waislam lakini hili halikuwa tatizo kwa umoja wa wananchi na sababu yake ni kuwa azma kubwa ya viongozi wa TANU ilikuwa umoja wa wananchi wote.
Hii ndiyo ikawa sababu ya Iddi Faiz Mafungo aliyekuwa Mweka Hazina wa Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika na Iddi Tosiri wakiwa wanachama wa mwanzo wa TANU wakamchukua Mwalimu Nyerere, mguu kwa mguu hadi Bagamoyo kwenda kumtambulisha kwa Sheikh Mohamed Ramia, Khalifa wa Tariqa Qadiriyya Bagamoyo.
Sheikh Mohamed Ramia alikuja TANU na kundi kubwa la murid na TANU Bagamoyo ikawa na nguvu sana.
Southern Province ni ngome kuu ya Kanisa Katoliki na TANU ilipata tabu kubwa kuingia khasa kwa kuwa kanisa lilikuw alikiwatisha waumini wake kuhusu makusudio ya TANU wakielezwa kuwa italeta vita nyingine ya Maji Maji.
Sheikh Mohamed Yusuf Badi wa Lindi alipoingia TANU mwaka wa 1956 na alipompokea Mwalimu Nyerere kwa zafa na dufu iliyopigwa na wanafunzi wa madrasa yake iliyokuwa mjini Lindi, kitendo hiki kilivunja fitna zote dhidi ya TANU na chama kikaenea kuanzia Masasi hadi Tunduru na Nachingwea.
Viongozi hawa Waislam wote kwa umoja wao walikuwa nyuma ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na hapa ndipo ulipojengwa msingi wa umoja wa Watanganyika.
Si wengi wanaojua kuwa kuiongoza TANU kiwe chama cha siasa cha kisekula kazi kubwa ilifanywa na Sheikh Hassan bin Ameir kwani alijua kwa jinsi TANU ilivyokuwa na wanachama wengi Waislam hii ingeweza kupelekea TANU kukwepwa na wale ambao hawakuwa Waislam.
Hii ingesababisha pengine kuanzishwa kwa chama kingine katika misingi ya dini kwa hofu ya kuogopa kumezwa na TANU chama cha Waislam.
Katika mikutano ya mwanzo ya TANU, pale Mnazi Mmoja, Mwalimu Nyerere alikuwa akipanda jukwaani na kutambulishwa na Sheikh Suleiman Takadir aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa TANU.
Picha hapo chini inamwonyesha Mwalimu Nyerere akiwa na Baraza la Wazee wa TANU. Sheikh Suleiman Takadir wa pili kulia waliokaa chini, Mtu wa pili waliosimama ni Dossa Aziz,wa sita Mwalimu Nyerere akifuatiwa na John Rupia na tisa ni Said Chamwenyewe akifuatiwa na Mohamed Jumbe Tambaza na Mshume Kiyate.
Picha nyingine ni hiyo inayomwonyesha kulia Iddi Faiz Mafungo, Sheikh Mohamed Ramia, Julius Nyerere, Saadan Abdu Kandoro na Haruna Taratibu wakiwa Dodoma wakati wa kuitangaza TANU.
Kumbukumbu kubwa ya kujenga umoja huu ni mwaka wa 1956 pale Mwalimu Nyerere aliposhiriki katika hafla kubwa ya khitma kwenye shamba la Sheikh Abdallah Chaurembo, Mtoni.
Picha hiyo hapo chini inamwonyesha Baba wa Taifa akiwa na viongozi wakubwa wa Kiislam shambani kwa Sheikh Abdallah Chaurembo.
Picha ya mwisho inamwonyesha kulia Bi. Titi Mohamed, Clement Mtamila, Sheikh Suleiman Takadir, Julius Nyerere na nyuma ni Rajab Diwani, John Rupia na Mama Maria Nyerere.
MWISHO