#HABARI: Watu zaidi ya 80 wamepoteza maisha yao huko nchini Pakistan baada ya kutokea ghasia za kidini maeneo ya kaskazini magharibi mwa nchi hiyo.
Mamlaka ya Pakistani inasema kuwa wameafikiana kusitisha mapigano kwa siku saba, baada ya vifo hivo.
Ghasia hizo zilianza siku ya Alhamisi, wakati watu wenye silaha waliposhambulia misafara ya Waislamu wa madhehebu ya Shia waliokuwa wakisafiri katika eneo hilo chini ya ulinzi wa polisi.
Zaidi ya watu 40 walikufa katika tukio hilo, ambalo lilisababisha mashambulizi ya kulipiza kisasi.
Waislamu wa madhehebu ya Shia na Sunni wamejihusisha katika mizozo ya kikabila na kimadhehebu kuhusu migogoro ya ardhi kwa miongo kadhaa.
Siku ya Jumapili afisa wa utawala wa eneo hilo aliiambia AFP: "Mapigano na mashambulizi ya msafara mnamo Novemba 21, 22, na 23 yamesababisha vifo vya watu 82 na majeruhi 156."
Akizungumza kwa sharti la kutotajwa majina, alisema kuwa watu 16 kati ya waliofariki ni Sunni na 66 ni wa jamii ya Shia.