Waziri Mchengerwa ametangaza Wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na Kidato cha Kwanza 2025

Waziri Mchengerwa ametangaza Wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na Kidato cha Kwanza 2025

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Joined
Apr 18, 2017
Posts
3,984
Reaction score
13,760


Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa ametangaza jumla ya Wanafunzi 974,332 waliohitimu Elimu ya msingi mwaka 2024 tayari wamepangiwa Shule za sekondari ambao wataanza Januari 2025.

Waziri Mchengerwa ametangaza matokeo hayo mbele ya vyombo vya habari Jijini Dar es Salaam leo Disemba 16, 2024.


===============

TAARIFA YA WANAFUNZI WALIOCHAGULIWA KUJIUNGA NA KIDATO CHA KWANZA JANUARI, 2025

Ndugu Wananchi, awali ya yote, napenda kutumia fursa hii, kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutujaalia uzima na kutuwezesha kuendelea kutekeleza majukumu yetu mbalimbali tukiwa na afya njema.

Pili, ninamshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuwekeza katika Sekta ya Elimu kwa kuhakikisha kila Mtoto wa Kitanzania anapata fursa ya kupata elimu. Kutokana na uwekezaji huo, Wanafunzi wote wenye sifa ya kujiunga Kidato cha Kwanza wanapata nafasi ya kujiunga na Kidato cha Kwanza bila ya kuwepo kwa chaguo la Pili kama ilivyokuwa awali.

2.0 Uchaguzi wa Wanafunzi wa Kidato cha Kwanza 2025

Ndugu Wananchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI imekamilisha zoezi la Uchaguzi wa Wanafunzi wa Kujiunga na Kidato cha Kwanza mwaka, 2025 kwa kuzingatia miongozo iliyotolewa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

3.0 Vigezo vilivyotumika Kuwapangia Shule Wanafunzi na Aina ya Shule Walizopangiwa:

Ndugu Wananchi, Uchaguzi wa Wanafunzi wa Kujiunga na Kidato cha Kwanza mwaka, 2025 umezingatia kigezo cha ufaulu wa mtahiniwa anayechaguliwa. Kila mtahiniwa aliyefanya Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi mwaka, 2024 na kupata jumla ya alama za ufaulu kati ya 121 hadi 300 amechaguliwa na kupangiwa Shule ya Sekondari ya Serikali.

Uchaguzi huu umehusisha wanafunzi 974,332 sawa na asilimia
100 ya wanafunzi wote waliokuwa na sifa ya kuchaguliwa wakiwemo Wasichana 525,225 na Wavulana 449,107. Wanafunzi hao ni wale waliofanya na kufaulu Mtihani wa Kuhitimu Elimu ya Msingi mwaka, 2024.

Ndugu Wananchi, Shule za Sekondari za Serikali walizopangiwa wanafunzi zipo katika makundi mawili: Shule za Bweni na Shule za Kutwa. Shule za Sekondari za Bweni za Serikali zimegawanyika katika makundi matatu ambayo ni; Shule za Sekondari za Bweni za Wanafunzi wenye ufaulu wa Juu (Special Schools), Shule za Amali za Kihandisi (Ufundi) na Bweni Taifa. Shule za Bweni ni za Kitaifa hivyo, zimepangiwa Wanafunzi kutoka maeneo mbalimbali ya nchi kwa kuzingatia mgawanyo wa nafasi uliobainishwa na vigezo vilivyowekwa ili kuimarisha Utaifa.

Ndugu Wananchi, Uchaguzi wa Wanafunzi katika makundi hayo ulifanyika kwa mujibu wa Mwongozo wa Uchaguzi kama ifuatavyo:-

a) Shule za Sekondari za Bweni kwa Wanafunzi wenye Ufaulu wa Juu:
Nafasi katika Shule za Wanafunzi wenye Ufaulu wa Juu zimegawanywa kwa kila Mkoa kulingana na idadi ya watahiniwa

wa Darasa la Saba waliotahiniwa katika Mkoa husika kwa kutumia Kanuni ya kugawa nafasi hizo Kitaifa.
Nafasi zilizotolewa kwa Mkoa zimegawanywa sawa kwa Halmashauri zote bila kujali idadi ya watahiniwa waliotahiniwa katika Halmashauri. Shule hizi ni Msalato, Mzumbe, Kilakala, Kibaha, Ilboru, Tabora Girls na Tabora Boys.

b) Shule za Sekondari za Bweni Amali za Kihandisi:
Nafasi katika Shule za Sekondari za Amali za Kihandisi zimegawanywa kwa kila Mkoa kulingana na idadi ya watahiniwa wa Darasa la Saba kwa Mkoa husika kwa kutumia Kanuni ya kugawa nafasi hizo Kitaifa. Nafasi zilizotolewa kwa Mkoa zimegawanywa sawa kwa kila Halmashauri bila kujali idadi ya watahiniwa waliotahiniwa katika Halmashauri. Shule za Sekondari za Bweni za Amali za Kihandisi ni Tanga Tech, Moshi Tech, Musoma Tech, Bwiru Boys, Ifunda Tech, Iyunga Tech, Mtwara Tech, Mwadui Tech na Chato Tech.

c) Shule za Sekondari za Bweni Taifa:
Nafasi katika Shule za Bweni za Kitaifa zimegawanywa kwa kila Halmashauri kwa kufuata idadi ya watahiniwa wa Darasa la Saba waliotoka katika Halmashauri husika kwa kutumia Kanuni ya kugawa nafasi hizo Kitaifa.

Ndugu Wananchi, jumla ya Wanafunzi 974,332 wakiwemo wasichana 525,225 na wavulana 449,107 ikijumuisha Wanafunzi wenye Mahitaji Maalum 3,067 (wasichana 1,402 na wavulana 1,665) wamechaguliwa na kupangwa katika Shule za Sekondari za Serikali kwa ajili ya kuanza masomo ya Kidato cha Kwanza mwaka, 2025 kwa mgawanyo ufuatao:-

(a) Shule za Wanafunzi Wenye Ufaulu wa Alama za Juu: Jumla ya Wanafunzi 809 wakiwemo wasichana 329 na wavulana 480 wamechaguliwa kujiunga katika Shule za Sekondari ambazo hupokea Wanafunzi wenye ufaulu wa Alama za Juu. Shule hizo ni Ilboru, Msalato, Kibaha, Kilakala, Mzumbe, Tabora Boys na Tabora Girls.

(b) Wanafunzi Waliochaguliwa Shule za Amali za Kihandisi: Jumla ya Wanafunzi 1,174 wakiwemo wasichana 197 na wavulana 977 wamechaguliwa kujiunga na Shule za Amali za Kihandisi. Shule hizo ni Ifunda Tech, Bwiru Boys, Mwadui Tech, Iyunga Tech, Moshi Tech, Mtwara Tech, Musoma Tech, Tanga Tech na Chato Tech.

(c) Shule za Bweni Taifa:
Jumla ya Wanafunzi 6,810 wakiwemo wasichana 5,199 na wavulana 1,611 wamechaguliwa kujiunga na Shule za Bweni Taifa. Kati ya wanafunzi hao, Wanafunzi Wasichana 3,320 wamechaguliwa kujiunga na Shule za Sekondari za Wasichana za Sayansi za Mikoa katika mikoa yote.

(d) Shule za Kutwa
Jumla ya Wanafunzi 965,539 wakiwemo wasichana 519,500 na wavulana 446,039 wamechaguliwa kujiunga katika Shule za Sekondari za Kutwa ambazo hupokea wanafunzi kutoka katika eneo la karibu na shule ya Msingi aliyosoma Mwanafunzi husika.

Ndugu Wananchi, Serikali ilifanya maandalizi mapema ili kuhakikisha kuwa wanafunzi wote watakaofaulu Mtihani wa kumaliza Darasa la Saba mwaka, 2024 wanajiunga na Elimu ya Sekondari ifikapo Januari, 2025. Kutokana na maandalizi hayo Wanafunzi wote 974,332 wakiwemo wasichana 525,225 na wavulana 449,107 waliofaulu Mtihani wa Kuhitimu Elimu ya Msingi

2024 wataanza muhula wa kwanza wa masomo wa mwaka 2025 utakaoanza tarehe 13 Januari 2025.

Ndugu Wananchi, napenda kutumia fursa hii kuwapongeza Wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na Kidato cha Kwanza mwaka, 2025. Vilevile, nawashukuru Viongozi wa ngazi ya Mkoa, Wilaya, Halmashauri, Wakuu wa Shule, Walimu na Wadau wa Elimu nchini kwa kutoa ushirikiano katika kusimamia uendeshaji na utoaji wa Elimu ya Msingi na Sekondari nchini.

Aidha, napenda kuwaasa wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na Kidato cha Kwanza mwaka 2025 nchini watumie vizuri fursa waliyoipata kusoma kwa bidii ili wafikie malengo waliojiwekea na matarajio ya wazazi.
4.0 Maelekezo ya Jumla na Utekelezaji wa Mtaala Ulioboreshwa kuanzia Januari, 2025:
Ndugu wananchi, kama mjuavyo, mnamo mwezi Januari, mwaka 2024 tulianza utekelezaji wa Mitaala iliyoboreshwa ya Elimu Ngazi ya Elimu ya Awali, Msingi na Sekondari. Ofisi ya Rais – TAMISEMI inaendelea na utekelezaji wa mitaala hiyo. Hivyo, Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa zinahimizwa kuweka mazingira wezeshi ya utekelezaji wa mitaala hiyo kwa lengo la kuhakikisha kunakuwa na ufanisi wa utekelezaji. Katika kuweza kutekeleza vema mitaala hiyo ninatoa maelekezo yafuatayo:-
(a) Kila Shule ya Sekondari itumie vema kipindi cha orientation kwa wanafunzi kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kuwasiliana katika lugha ya Kiingereza na kuchagua aina ya fani wanazopenda kusoma katika shule zenye mkondo wa amali zisizo za kihandishi;
(b) Wazazi/Walezi kufanya maandalizi ya kutosha kwa watoto waliochaguliwa kujiunga Kidato cha Kwanza mwaka wa

masomo 2025 ili kuepuka watoto kuchelewa kuanza masomo yao kwa wakati na
(c) Mikoa na Halmashauri zote nchini kuhakikisha kuwa wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na Kidato cha Kwanza mwaka wa masomo 2025 wanaripoti shuleni na kuandikishwa ili kupata haki yao ya msingi ya elimu.

Ndugu Wananchi, natoa wito kwa Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Viongozi na Watendaji wa Halmashauri kwa kushirikiana na wadau wa elimu kuhakikisha Wanafunzi wote waliochaguliwa wanaanza masomo yao mwezi Januari, 2025 bila vikwazo vya aina yoyote ili kutekeleza azma ya Serikali ya utoaji wa Elimumsingi Bila Malipo.

Hivyo, Ninawaagiza Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri na Wakuu wa Shule kuhakikisha maandalizi yote kwa ajili ya kuwapokea Wanafunzi wa Kidato cha Kwanza mwaka, 2025 yanakamilika kwa wakati ili kuhakikisha Wanafunzi wote wanaripoti Shuleni ifikapo tarehe 12 Januari, 2025 kwa Wanafunzi waliochaguliwa Shule za Bweni na tarehe 13 Januari, 2025 kwa Wanafunzi waliochaguliwa Shule za Kutwa.

Vilevile, ninawahimiza, Wazazi, Walezi na Jamii kushirikiana na Uongozi wa Shule, Mikoa, Wilaya na Halmashauri ili kuhakikisha kuwa Wanafunzi wote waliochaguliwa wanaandikishwa, wanahudhuria na kubakia Shuleni hadi watakapohitimu Elimu ya Sekondari.

Ndugu Wananchi, orodha ya Wanafunzi wote waliochaguliwa pamoja na Fomu za Maelezo ya Kujiunga na Kidato cha Kwanza mwaka, 2025 (Joining Instructions) kwa Shule zote za Bweni zinapatikana kwenye tovuti ya Ofisi ya Rais - TAMISEMI kupitia

kiunganishi cha www.tamisemi.go.tz na Baraza la Mitihani la Tanzania www.necta.go.tz.

Ndugu Wananchi, pamoja na maelekezo haya, kwa Mwanafunzi, Mzazi na Mlezi atakayekuwa na suala linalohitaji maelekezo au ufafanuzi zaidi aende katika Ofisi za Wakuu wa Shule, Ofisi za Elimu za Halmashauri na Mikoa au apige simu kwenye Kituo cha Huduma kwa Wateja, Ofisi ya Rais - TAMISEMI kwa namba za simu 026 160210 au 0735 160210.

Mohamed O. Mchengerwa (Mb.)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA)
16 Desemba, 2024
 
Back
Top Bottom