YANGA inatua Dar es Salaam leo saa 12.40 jioni lakini kocha wake mkuu Kosta Papic amefunua moyo wake na kuweka bayana mambo matatu yaliyoitoa Yanga kwenye ligi ya mabingwa.
Yanga ilifungwa bao 1-0 na FC Lupopo katika mechi ya marudiano iliyofanyika Jumamosi Stade de Kenya mjini hapa.
Mabingwa hao watetezi wa ligi kuu ya Bara walihitaji ushindi wa mabao 2-0 kusonga mbele kutokana na kufungwa mabao 3-2 katika mchezo wa awali jijini Dar es Salaam. Yanga imetolewa kwa jumla ya mabao 4-2.
Papic amesema kuwa kuna mambo matatu yameiponza timu yake ambayo ni uwanja mbovu, hali ya hewa pamoja na matokeo ya Dar es Salaam.
"Kiufundi hapa timu ilikuwa vizuri kabisa muda wote kuliko mechi yoyote tuliyowahi kucheza, lakini uwanja umetuharibia mbinu zetu umejaa maji na matope unateleza tu kila mara."
"Wachezaji walipokuwa wanapanga mashambulizi kwa kasi lazima mmoja wao alikuwa anaanguka na kutoa faida kwa mwenyeji ambaye anaonekana kuzoea hii hali kwahiyo tukawa tunatumia nguvu kubwa sana.
"Ilifika wakati kukawa hakuna ufundi mpira unapigwa tu mbele kutafuta matokeo kutokana na hali ya uwanja, kama ulikuwa mkavu kama Dar es Salaam tungebadilisha matokeo."
"Mambo mengine yaliyotuharibia ni kufungwa Dar es Salaam pamoja na hali ya hewa ya hapa ni mazingira mageni.
Timu yangu imeondolewa kwenye mashindano pale Dar es Salaam siyo hapa, Lubumbashi imecheza sana," alisema Papic.
Yanga ambayo wachezaji wake saba wa timu ya Taifa waliwasili Dar es Salaam jana, inaondoka hapa leo saa 5.15 asubuhi na kutua Nairobi saa 10.25 na saa 11.25 itaondoka na kuwasili Dar es Salaam saa 12.40 na ndege ya Shirika la Ndege la Kenya, KQ 424.