Tokea mwanzoni mwa wiki hii pamekuwepo uvumi kuwa Rais JPM ni mgonjwa. Bahati mbaya sana, pamoja na matetesi hayo kupitia mitandao ya kijamii, serikali imenyamaza kimya pasipo kukanusha au kukubaliana na uvumi huo.
Japo serikali hailazimiki kuibuka na kujibu kila kitu kinachojadiliwa kwenye mitandao ya kijamii, lakini kutokana na unyeti wa Ofisi ya Rais, pana haja ya serikali kujitokeza kupitia msemaji wa serikali au Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu kusema neno.
Ukimya wa serikali si afya kwa utulivu wa jamii kwani Watanzania wana haki ya kuelezwa ukweli kuhusu Rais wao. Tabia ya kunyamazia uvumi inatoa mwanya kwa watu kusadikishwa mambo yasiyo na ukweli na hivyo kusababisha taharuki isiyo na msingi.