Sehemu ya tatu
MWANZO WA LIGI
Nakupitisha kuanzia mwanzo kabisa ili tuelewane vizuri
Pichani kushoto ni Milan Celebic, kocha wa kwanza wa kigeni wa timu ya taifa, kuanzia Tanganyika hadi Tanzania.
Kulia ni mchezaji wa timu ya taifa, Ally Samatta, baba yake nahodha wa sasa timu ya taifa, Mbwana Samatta.
Kocha huyo raia wa Yugoslavia, alikuja nchini mwaka 1964 akiletwa na serikali.
Wakati huo hakukuwa na ligi ya taifa bali ya Dar Es Salaam pekee iliyosimamiwa na chama cha soka cha Dar Es Salaam (Dar Es Salaam Football League Association-DFLA)
Chama cha soka cha taifa kilichoitwa TFA (Tanganyika Football Association) kilisimamia mashindano ya Taifa Cup ambayo yalishirikisha timu za mikoa.
Kupitia Taifa Cup ya 1964, kocha Celebic alimuona Ally Samatta na kumchagua kama mchezaji bora wa nchi, na kumuita kwenye timu ya taifa.
Mwaka huo Tanganyika na Zanzibar ziliungana na kuzaliwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Chama cha soka cha Tanganyika, TFA, kikabadilika na kuwa chama cha soka cha Tanzania, FAT.
FIFA ikakisajili rasmi chama hicho kama chama cha soka cha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Lakini kwa ndani, FAT ilisimamia soka la Bara, na Zanzibar ikaundwa idara maalumu ya kusimamia soka, iliyoitwa IFOZA, yaani Idara ya Football Zanzibar.
Baada ya michakato yote hiyo, Kocha Milan Celebic akaishauri FAT kuanzisha ligi ya kitaifa itakayomsaidia kupata wachezaji wa timu ya taifa.
Rais wa FAT, Balozi Majjid, akakubaki na ndipo mwaka 1965 ikaanzishwa ligi ambayo iliitwa Mashindano ya kutafuta Klabu Bingwa ya Taifa.
Ligi hiyo ilichezwa bila madaraja, na iliendeshwa kwa mtoano kama ilivyo ASFC, na ilisajiliwa kama ligi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Lakini kwa miaka yote ya 1960, timu za Zanzibar hazikushiriki kutokana na sababu mbalimbali, zikiwemo za kiuchumi na kushindwa kujipanga vizuri kwa IFOZA.
Zilianza kushiriki mwaka 1972 pale timu za Ujamaa na Navy zilipovuka na kuja, na zikaendelea kuongezeka kila mwaka
Miaka ya 1970, mashindano haya yalianzia ngazi ya wilaya, mikoa hadi taifa.
Ngazi ya taifa ilikuwa kwenye kituo kimoja, kama ilivyokuwa 1974 kwenye kituo cha Nyamagana Mwanza.
Itaendelea