ASKOFU KUONGOZA MATEMBEZI YA HIARI YA RAIA KUHAMASISHA UUNDAJI WA TUME HURU YA UCHAGUZI NA UANDIKAJI WA KATIBA MPYA NCHINI TANZANIA!
Wapendwa Watanzania!
Tunapenda kuwajulisha kuwa Askofu Mwamakula, anakusudia kuongoza Matembezi ya Hiari ya Raia yasiyopungua umbali wa Kilometa 15 katika Mikoa mbalimbali nchini Tanzania na nje ya nchi. Watu watakaoshiriki Matembezi hayo watatokea kila kona za mji husika hadi sehemu ya kukutania ambapo watu wote watakusanyika kwa ajili ya kufikisha au kutolea ujumbe. Ili kuepusha usumbufu, watu watakuwa wanatembea kimakundi lakini kila kundi halitazidi watu 20 na kama watu watakuwa wengi kutokea njia moja kutakuwa na muachano au umbali wa kilomita moja kati ya kundi na kundi njiani!
Lengo la Matembezi hayo ni kuwahamasisha Watanzania umuhimu wa Kuunda Tume Huru ya Uchaguzi na Kuandika Katiba Mpya kabla ya Mwaka 2025. Kwa mazingira yaliyopo sasa ambapo Bunge la Tanzania limekuwa ni Bunge la Chama kimoja ambacho katika Ilani yake hawana hoja ya Tume Huru na Katiba Mpya, hatuwezi kutegemea mambo hayo kuanzishwa na Bunge hili. Hata hivyo, watu wa makundi yote watahamasishwa kushiriki Matembezi hayo pasipo kujali vyama na itikadi zao.
Kila mkoa au mji utakuwa na Timu ya Uratibu ambayo itasaidia kuratibu na kuandaa Matembezi hayo. Wale watakaopenda kusaidia au kuwezesha Matembezi hayo wataelekezwa kuwasiliana na Timu ya Uratibu ya Kitaifa itakayosaidia Uratibu kwa niaba ya Askofu. Timu hiyo ya Uratibu wa Kitaifa sambamba na Timu za Mikoani zitatangazwa mapema kuanzia Januari 2021 baada ya kuundwa!
Kwa taarifa hii, tunaomba Watanzania wote wajiandae kushiriki Matembezi hayo katika kila Mkoa. Matembezi hayo yataanza mapema mwaka 2021 na tarehe ya kila Mkoa itatangazwa na utaratibu wote. Kuanzia Januari 2021, Askofu atatangaza rasmi utaratibu wa namna ya kushiriki ikiwemo Waratibu wa Matembezi katika kila Mkoa!
Kwa Watanzania walioko nje ya Tanzania, Askofu anaweza kufika katika nchi hizo endapo wataweza kuandaa mazingira.
Kwa sasa Askofu anamuomba kila mtu kusambaza ujumbe huu ili kuwaandaa Watanzania wote kwa matukio hayo ya kihistoria!
Mwana Kondoo Ameshinda! Tumfuate!
Askof Mkuu Emmaus Bandekile Mwamakula
Namashuri tu kwanza angeanza na matembezi ya waumini wake ndipo aje ya mji wake kisha nchi nzima.
Kwanza huyo ni askofu qa kanisa gani? Maana huwa nasikisikia tu mwamakula. Ushawishi wake kwanza kwenye mji aliopo ukoje?
Watu wengine wakishashiba zaka na sadaka wanakosa cha kufanya.
Mimi nadhani kuna namna bora ya kufikisha ujumbe wa kuandikwa kwa katiba mpya na tume huru. Lakini hayo ndio mahitaji ya msingi ya watanzania kwa sasa.
Mimi namshauri aanze kwanza kabla ya kudai katiba mpya kwa matembezi ambao ni ushamba na kukariri atueleze
1. Hii iliyopo ina mapungufu gani, imechangia vipi kutufikisha hapa tulipo, imekwamishaje maendeleo ya nchi na ya mtu mmoja mmoja nk.
2. Hiyo anayoitaka inatakiwa kuwa iwe na vitu gani vitavyo harakisha maendeleo ya nchi na ustawi wa mtu mmoja mmoja. Isije kuwa kama Kenya wameandika katiba mpya miaka hata 10 haijaisha wanaandika tena katiba nyingine, ni upuuzi tu. Na je hiyo katiba mpya walioandika ni kwa maslahi ya wananchi au wanasiasa.
3. Tume huru ya uchaguzi, je hii iliyopo sio huru, kivipi sio huru? Watu wanadai matokeo yamepikwa. Ushahidi wa kuiba kura uko wapi? Sio mnapiga kelele gari imekamatwa ikiwa masanduku ya kura zimepigwa kwa Magufuli. Gari la nani? Gari namba gani za usajili? Kwanini hamkulilipoti tume ya uchaguzi au waangalizi wa kimataifa likiwa na ushahidi. Mbona kura mlizokamata mlikuwa mnazichoma moto kupoteza ushahidi.
Kwa ujumla ni wanasiasa kutafuta vurugu tu na kusema muonekane mpo kwenye siasa lakini sio kwa maslahi ya wananchi. Kabla ya kuwatembeza hata waumini wake kudai katiba mpya na tume. Ni bora angewatembeza kuwafunza kuwajibika kujiletea maendeleo wao na taifa lao. Utakuta waumini wenyewe ni maskini tu na wala hawajitambui
Namhakikishia, wala polisi hawatahangaika kuzima maandamano uchwara, yatajizima yenyewe