Haya matukio ya mauaji, vurugu za kila mara, watu kupigwa mabomu kwenye mikusanyiko ya kisiasa na ibada, watu kutekwa, kuteswa kwa kung'olewa meno; kucha na kutobolewa macho yote yana msukumo wa serikali iliyoko madarakani. Haiwezekani hata kidogo matukio yote haya yanaachwa yanaendelea na hakuna jitihada zozote zinazofanywa na serikali kudhibiti vitendo hivi vya kihalifu.
Kikwete na wenzake ni vyema wakatambua kuwa waliapa kwa kutumia misahafu kuwa watailinda nchi yetu pamoja na wananchi wake. Yanayotokea sasa ni kinyume kabisa na kiapo alichoapa na nachelea kusema kuwa anaombea haya mambo ya kihalifu yaendelee kutokea ili wananchi wasipate muda wa kuhoji utendaji wa serikali yake.
Wao wana vyombo vya dola vinavyoendeshwa kwa kodi za watanzania lakini wamekataa kwa makusudi kutowalinda wananchi wanyonge. Wasifikiri damu inayomwagika kila uchao ni sawa na damu ya ng'ombe ama mbuzi wanaochinjwa kwenye machinjio. Wameshindwa kutimiza wajibu wao wa msingi na sasa watu wanaishi kwa hofu na kutegemea kudra za Mwenyezi Mungu kana kwamba tuko Somalia, Darfur ama Syria.
Damu inayomwagika kwa kushindwa kwao kutimiza yale yanayowapasa itabaki kwenye mikono na mioyo yao muda wote wa maisha yao na hakika hawataweza kujitakasa asilani.
EE MWENYEZI MUNGU ILINDE NCHI YETU NA WATU WAKO WANYONGE.