Jamani jana nimesikia mahojiano BBC ambapo Mh Mbowe alikuwa akitoa ufafanuzi wa jinsi ambavyo CUF hawakutaka kuungana na Chadema baada ya kuombwa kwamba wafanye alliance katika upinzani. Mbowe alisema kuwa aliambiwa na Hamad Rashid kuwa wao hawataungana na Chadema lakini wataungana na vyama vingine vya upinzani, ingawa wanajua kwa hakika kuungana kwao hakuwezi kuwaezesha kuunda serikali kivuli.
Na hapo hapo alihojiwa Hamad Rashid wa CUF kuhusu kutoridhia kwao kujiunga na Chadema, na alisema kuwa wao walikataa kujiunga na Chadema kwa kuwa kilikataa kufanya alliance na vyama vingine vya upinzani. Alichukulia mfano wa bunge lililopita ambalo wao walishirikiana na vyama vingine vya upinzani kuunda serikali kivuli.
Kwa maoni yangu napenda niwakumbushe CUF kwamba Chadema pekee sasa ina uwezo wa kuunda serikali kivuli bila kushirikiana na chama chochote. Na ni haki ya Chadema kama chama kilicho na uhalali wa kuunda serikali kivuli, kuchagua chenyewe ni nani wa kuwa naye katika kambi yake na ni yupi hafai kuwa katika kambi yake. CUF kama anayekaribishwa katika serikali ya umoja kivuli hana haki ya kuichagulia chadema chama rafiki. Utakuwa ni uhuni kudai kwamba ili washirikiane lazima vyama vyote vinavyoitwa vya upinzani vishirikishwe. Hii ni kuilazimisha Chadema kufanya jambo ambalo haitaki na jambo hili halikubaliki.
Kuna mfano utokanao na wao CUF, kwamba hata wao wakijua kwamba kuna vyama vingi vya siasa na wakijua wao kwamba ndio Chama kikuu cha upinzani Zenji waliamua wao pekee bila kushirikiana na vyama vingine vya upinzani ambavyo vilikuwepo kukaa na Serikali ya CCM na kufanya muafaka ambao unawanufaisha wao tu na si vyama vingine. Hakuna ambaye amewapigia kelele kwa jambo hili bali vyama vingi vimekaa kimya vikijaribu navyo kuona kwamba vinajaribu kujijenga ili na vyenyewe vifike hatua waliyofikia CUF. Ni uhuni kujifanya CUF kuwa wao wana uchungu wa kushirikiana na vyama vingine sasa katika bunge hili, wakati hata wao hawaamini rohoni mwao hiyo dhana kwamba ni sawa.
Kwa upande mwingine nawashauri viongozi wa Chadema kutokubali kuungana na CUF kabisa katika serikali kivuli maana leo CUF sio chama cha upinzani. Ni uongo na ulaghai kabisa tukiita CUF kuwa ni chama cha upinzani Tanzania. Kwani wanampinga nani wakati wote wako serikalini? Kawaida mnapokuwa mnaendesha serikali ya mseto ina maana wote mnakuwa na makubaliano katika uendeshaji wa serikali sasa hapo nani anayepinga mwingine wakati wote nyie ni watawala? CUF kwa sasa hivi kinatumika kusambalatisha upinzani kwa kujivika sura ya upinzani lakini ukweli ni kwamba wao kwa sasa hivi hawapo upinzani tena bali wako serikalini! Nawasihi viongozi wa Chadema wasijaribu kabisa kujishirikisha na CUF.
Pia napenda kuwashauri Chadema kushirikiana na Chama cha NCCR tu kama kitaonyesha kuhitaji kufanya hivyo pamoja na tofauti zilizopo. Vyama hivi vinaweza kuingia makubaliano na kushirikiana. Najua kuwa kuna mtafaruku wa mwenyekiti wao kuhusiana na mambo ya uchaguzi lakini bado naamini hayo ni mawazo yake binafsi lakini kichama, Chama kinaweza kuwa na mawazo tofauti. Nasema hivi kwa sababu Chama si Mbatia, bali Mbatia ni sehemu ya Chama. Lakini wakiona wao hawawezi kushirikiana nanyi waacheni.
Nawatahadhalisha sana Chadema kuepuka kuungana na TLP na UDP maana wao walishajipambanua wazi kuwa wao si wapinzani. Wao na CUF wako sawa. Ni mapandikizi ya CCM na wanaweza wakaiunga mkono CCM if they wish na at the end historia itawahukumu. Waache wakae wanavyotaka, wakitaka kuwaunga mkono sawa, wasipotaka waache maana sisi wananchi tuliowapigia kura nyingi nyie tunajua nini la kufanya na tutawamaliza wakati ujao.
Nihitimishe kwa kuomba tena viongozi wa chadema kufanya kazi kwa nguvu bila kujali nani atawaunga mkono au la, na huku mkijua sisi wananchi tuko nyuma yenu. Mtu au kikundi chochote kisiwatishe maana wananchi bado tuna imani na nyie. Simamia haki na sheria na sisi tutawapa reward. Msishinikizwe na chama chochote kwa tishio la kutowaunga mkono. After all, vyama vyote tofauti na CCM, viko vichache tu. Na hata kama mungeweka msimamo mmoja, wingi wenu hauwezi kubadilisha maamuzi ya CCM. Kwa hiyo kujitoa kwa CUF na wengine hakuwezi kuwatisha tena. Wacha waendelee kushirikiana na wala nchi maana nia yao ni kula nchi pia. Sisi Chadema nia yetu ni kuona mabadiliko katika Katiba, siasa na uchumi. Tutasimamia kile tunadhani ndio sahihi na mwisho agenda zote tutazirudisha kwa wananchi wenyewe waamue. Nina hakika kwa kansa iliyokwisha kamata CCM hakutakuwa na mabadiliko ya maana kwani ahadi zao hazitekelezeki, ufisadi utadumu kwa kasi zaidi, na tumesha anza kuona indicators za mfumuko mkubwa wa bei sasa kwa kila kitu kuanza kupanda bei kwa kasi ya ajabu.
HIMA TUKAZE BOOT NA TWENDE MBELE BILA WOGA.