Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Emmanuel Nchimbi amewaongoza wajumbe wa NEC alioongoza nao ziarani mkoani Mwanza na wanachama wa chama hicho mkoani humo wamemchangia Shilingi Milioni Tano Makamu Mwenyekiti wa chama cha CHADEMA, Tundu Lissu ili kufanyia matengenezo gari yake.
Kada wa CCM, Mchungaji Peter Msigwa akiwa kwenye mkutano wa chama hicho kwenye uwanja wa Furahisha jijini Mwanza alimuomba Katibu Mkuu wa CCM, Dkt. Nchimbi kuhamasisha wanachama wa CCM kumchangia Lissu ili gari hilo limuwezeshe kufanya shughuli za siasa.
Kwa upande wake, Dkt Emmanuel Nchimbi amesema siasa si uadui hivyo ni vyema kushikana mkono pale panapobidi kwani wanasiasa wote wanaijenga Tanzania.
Alipotafutwa kuzungumzia kitendo hicho kilichofanywa na CCM, Lissu amewashukuru CCM kwa mchango na kwamba atazipokea fedha hizo kama ambayo amekuwa akipokea kutoka kwa makundi tofauti ya watu.
"Nawashukuru, kama nilivyosema...hatukusema tunachangiwa na wanaChadema peke yao, kama nilivyotibiwa, sikutibiwa na wanaChadema peke yao. Kwa hiyo, wakichangia nitazipokea, sina sababu ya kukataa," amesema Lissu.
Mwananchi