JESHI la Polisi mkoani Arusha, linamshikia Blandina Fred mkazi wa Kijiji cha IIkirev, Kata ya Olturoto wilayani Arumeru, kwa tuhuma za kumuua kwa kumchoma kisu mpangaji mwenzake, Erick Adam kisa shilingi 1000 ya mchango wa umeme.
Tukio hilo limetokea Jana baada ya kutokea ugomvi baina ya wapangaji hao wawili ambapo inadaiwa marehemu Adam aligoma kulipia deni la umeme ambao kwa kawaida wapangaji huchangia.
Kamanda wa Polisi mkoani humo, Justine Masejo akizungumza na chombo kimoja cha habari leo, June 20, 2023, amesema tukio hilo lilitokea majira ya mchana wakati, Blandina akiwa na kisu akijiandaa kupika.
"Kilichotokea ni kwamba wote ni wapangaji walikuwa wakigombana huyu binti alikuwa na kisu kwa kuwa alikuwa jikoni, sasa ndio alimchoma mwenzake," amesema.
Amesema Adam alifariki kutokana na kutokwa na damu nyingi baada ya kuchomwa kisu, huku mtuhumiwa bado yupo chini yaulinzi kwa mahijiano zaidi, na taratibu zikikamilika atafikishwa mahakamani.