Ndugu msomaji, fahamu kuwa kwa mujibu wa mafundisho sahihi ya Uislaam, maiti ana haki nne anazopaswa kutendewa, ambazo ni:
1. Kuoshwa,
2. Kuvishwa sanda,
3. Kuswaliwa, na
4. Kuzikwa.
Hii ina maana kuwa Waislamu watawajibika kuyafanya haya kwa kila maiti Muislamu na si vinginevyo. Na watakapoacha kumfanyia maiti mambo hayo watapata dhambi Waislamu wote wa sehemu ile.
1: Namna ya kumuosha maiti hatua kwa hatua unaweza soma hapa
Ili maiti aweze kuoshwa vizuri hatua zifuatazo ziweze kupitiwa: 1. Maiti awekwe kwenye kitanda chenye tobo katikati kwa ajili ya kupitisha uchafu utokao tumboni kama upo. 2. Lichimbwe shimo (ufuo) usawa wa tobo la kitanda ili kuhifadhi uchafu utokao kwa maiti. 3. Maiti afunikwe na shuka kubwa...
www.jamiiforums.com
2: Kuvishwa Sanda
Baada ya maiti kuoshwa vizuri, hatua inayofuata ni kuvishwa sanda, nguo au shuka ndefu yenye uwezo wa kufunika mwili wote wa maiti. Ni bora zaidi na inapendeza shuka hiyo ikiwa nyeupe. Na hii ni kutokana na Hadiyth sahihi ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)aliposema:
”Pendeleeni kuvaa mavazi meupe kwani hayo ni katika mavazi bora kwenu na mukafini (muwavishe) maiti wenu kwa hizo sanda”.[11]
Sanda huwa ni shuka tatu (3) tu, na si zaidi, kutokana na Hadiyth iliyosimuliwa na mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhwi ya Allaah ziwe juu yake) aliyesema:
“Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)alikafiniwa (alivishwa sanda) katika nguo tatu..”[12]
Ndugu msomaji, hakuna tofauti kati ya sanda ya maiti mume na sanda ya maiti mke, na hii ni kutokana na kukosekana ushahidi sahihi juu ya hilo, na kama upo, basi ni Hadiyth ambazo hazikusihi upokezi (sanadi) wake. Mfano wa Hadiyth dhaifu inayotumiwa na baadhi ya watu ni Hadiyth ya Layla bint Qaaif Ath-Thaqafiy inayoeleza kuwa sanda ya kike ni nguo tano zikiwa shuka mbili, kikoi, kanzu, na kilemba. Hadiyth hii upokezi (isnadi) yake ni dhaifu. Ndani ya msururu wa wapokezi (isnadi) kuna mtu mmoja, anaitwa Nuuh bin Haakim Ath-Thaqafiy, ambaye hajulikani zaidi ya jina lake tu, kama alivyoelezea al-Haafidh bin Hajar na wengineo
Uandaaji Wa Sanda
Shuka hizo kwa ajili ya sanda zitatandikwa sehemu safi. Kisha zitafukizwa udi na manukato mazuri mara tatu, kama alivyoelekeza Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
Mtakapoweka manukato ya maiti basi wekeni mara tatu.”[14] Isipokuwa sanda ya aliyehirimia kufanya hija haitapakwa manukato wala haitafukizwa udi.”
Baada ya kutandikwa sanda, maiti atalazwa juu yake. Itachukuliwa ncha ya upande wa kulia na iletwe hadi kifuani mwake, na ncha ya kushoto itafanywa hivyo hivyo. Utaratibu huo utafuatwa kwa shuka ya pili na ya tatu. Kisha itachukuliwa kuanzia kichwani na itafungwa na miguuni pia itafungwa. Pia itawekwa pamba iliyolowanishwa manukato mazuri na itawekwa juu ya macho yake na mdomoni mwake kama alivyoelekeza Shaykh Ibn ‘Uthaymiyn. Mpaka hapa, maiti itakuwa tayari kwa ajili ya kutekelezewa jambo la tatu ambalo ni kuswaliwa.
3: Kuswalia maiti
Ndugu msomaji, ni wajibu kumswalia kila maiti wa Kiislamu isipokuwa hawa wafuatao:
1. Mtoto mdogo ambaye hajafikia kubalehe.
2. Mtu aliyekufa shahidi (aliyekufa vitani) kwani Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakuwaswalia waliokufa katika vita vya Uhud.
Ndugu msomaji, fahamu kuwa tunaposema kuwa si wajibu kuwaswalia watu wa aina hii hatuna maana kuwa ni haraam kuwaswalia, bali tunamaanisha kuwa hakuna ulazima au uwajibu wa hilo. Lakini wakiswaliwa inafaa kwa kuwa kuna ushahidi juu ya hi
lo
4: Kuzikwa
Jambo la nne analopaswa kutekelezewa maiti ni kuzikwa. Kaburi ni lazima liwe refu kwenda chini na liwe pana. Kina cha kaburi kiwe sawa na kimo cha mtu mzima na kunyoosha mkono, na litachimbwa kiasi maiti akilazwa kwa ubavu wa kulia atakuwa anaelekea Qiblah
Kaburi likiwa tayari, maiti atachukuliwa katika jeneza na kuwahishwa katika kaburi. Wakati wa kusindikiza jeneza (kumpeleka maiti kaburini), mambo yafuatayo yanapaswa kuchungwa:
Kwanza, lisifuatwe jeneza kwa sauti wala kwa moto
Hapa inamaanisha sauti yoyote ya mwanadamu. Pia haifai kubeba chetezo cha ubani chenye moto wakati wa kusindikiza jeneza.
Pili, jeneza lisifunikwe na chochote. Kufunika jeneza au kaburi wakati wa kuzika ni miongoni mwa mambo yasiyokuwa na ushahidi. Baada ya maiti kuwasilishwa kaburini, watatakiwa watu baadhi washuke ndani ya kaburi, na iliyo bora zaidi ni kuwa watakaoingia ndani ya kaburi wawe ndugu wa aliyefariki.
Maiti atalazwa kama tulivyoelezea katika uandaaji wa kaburi, huku wakisema wanaomlaza maiti kwenye mwana-ndani:
“Kwa jina la Allaah na juu ya mila ya Rasuli wa Allaah” au “Kwa jina la Allaah na juu ya Sunnah ya Rasuli wa Allaah.”
Wanaotakiwa kuyasema maneno haya ni wale wanaomuweka maiti katika mwanandani (sehemu ndogo inayochimbwa ndani ya kaburi kwa ajili ya kumlaza maiti kwa ubavu wake wa kulia) na sio walio juu ya kaburi.
Baada ya maiti kulazwa katika mwanandani, kaburi litafukiwa na mwisho litainuliwa kiasi cha shibri moja tu.
Kujengea Kaburi
Kwa taratibu na mafunzo sahihi ya Kiislamu, kaburi halitajengewa. Haikupata kuonekana zama za Nabiy (Swalah na salaam za Allaah iwe juu yake) kaburi likajengewa na yeye akiwa hai, bali alionekana na kusikika kwa kinywa chake akilikemea vikali suala hili.
Kwa msingi huu tunatumia fursa hii kumuusia kila asomaye Makala haya kuwa maiti hanufaiki na na wala hana haja na vitu vya duniani, si vigae, marumaru, wala jengo la aina yoyote katika kaburi, bali anachohitaji zaidi maiti ni du’aa yako. Mkumbuke, kisha muombee msamaha kwa Allaah Ampunguzie adhabu za kaburi bila kutumia utaratibu maalum, hapo utakuwa umemfanyia jambo kubwa sana.
Kuwekea Alama Makaburi
Je, ni namna gani unaweza kulitambua kaburi au kuliwekea alama kaburi? Hilo linajibiwa katika Hadiyth iliyosimuliwa na Swahaba mtukufu Al-Mutwallib bin Abi Wadaa (Allaah amuwie radhi) kuwa, pindi alipokufa ‘Uthmaan bin Madh’uun, ndugu wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa kunyonya ziwa moja, baada ya kumaliza kufukia kaburi, Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alibeba jiwe na akaliweka upande wa kichwani kisha akasema,
“Nimeliweka jiwe hili ili nipate kulijua kaburi la ndugu yangu na nizike pembeni yake atakayekufa katika jamaa zangu”
Allahu Ya'alam (Mwenyezi Mungu ndiye mjuzi zaidi)