12 Kwa hiyo, kama kwa mtu mmoja dhambi iliingia ulimwenguni, na kwa dhambi hiyo mauti; na hivyo mauti ikawafikia watu wote kwa sababu wote wamefanya dhambi;
Hayo ni mafunzo ambayo Paulo amejaribu kufunza katika barua zake. Lakini imani aliyofunza Paulo ya Dhambi ya Asili ya kurithiwa inapingwa na vifungu vingine kutokana na Biblia.
Katika Kumbukumbu la Torati, kwa mfano (na hicho ni katika vitabu vitano vinavyohisabiwa kuwa ndiyo Torati inayoaminiwa na Mayahudi na Wakristo) Musa anasema:
Mababa wasiuawe kwa ajili ya watoto wao, wala watoto wasiuwawe kwa ajili ya baba zao; kila mtu na auawe kwa ajili ya dhambi yake mwenyewe.
Kumbukumbu 24.16
Hali kadhaalika tunasoma neno la Mungu katika kitabu cha Yeremia:
Siku zile, hawatasema tena, Baba za watu wamekula zabibu kali, na meno ya watoto wao yametiwa ganzi. Bali kila mtu atakufa kwa sababu ya uovu wake mwenyewe; kila mtu alaye zabibu kali, meno yake yatatiwa ganzi.
Yeremia 31.29-30
Tena Neno la Mungu linaendelea kusema katika kitabu cha Ezekieli kwa uwazi zaidi:
Lakini ninyi mwasema, Kwani yule mwana asiuchukue uovu wa baba yake? Yule mwana atakapofanya yaliyo halali na haki, na kuzishika amri zangu na kuzitenda, hakika ataishi. Roho itendayo dhambi, ndiyo itayokufa; mwana hatauchukua uovu wa baba yake, wala baba hatauchukua uovu wa mwanawe; haki yake mwenye haki itakuwa juu yake, na uovu wake mwenye uovu utakuwa juu yake.
Ezekieli 18.19-20
Ni wazi kabisa kuwa nadhariya ya Paulo ya dhambi ya asili ya kurithiwa inagongana na neno la Mungu kama lilivyo katika Biblia. Na haya yametajwa na Mwenyezi Mungu katika Qur'ani:
Katika Injili pia upo ushahidi ya kuwa Yesu mwenyewe anapinga hiyo nadhariya ya imani ya Dhambi ya Asili, yaani wanaadamu wamerithi dhambi aliyotenda Adam:
Hata (yesu) alipokuwa akipita alimwona mtu, kipofu tangu kuzaliwa. Wanafunzi wake wakamwuliza wakisema, Rabi, ni yupi aliyetenda dhambi, mtu huyu au wazazi wake, hata azaliwe kipofu? Yesu akajibu, Huyu hakutenda dhambi, wala wazazi wake; bali kazi za Mungu zidhihirishwe ndani yake.
Yohana 9.1-3
Kinyume na mafunzo ya Kanisa linalojiita kwa jina lake, ya kwamba watoto wote waliozaliwa wamezaliwa katika dhambi, mwenyewe Yesu Kristo anathibitisha kuwa watoto hawana dhambi.
Tunaona hayo zaidi katika maneno haya yaliyotajwa katika Injili ya Mathayo:
Akaita mtoto mmoja, akamweka katikati yao, akasema, Amin, nawaambia, Msipoongoka na kuwa kama vitoto, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni.
Mathayo 18.2-3