SHULE ya Msingi Nkweshoo iliyoko Kijiji cha Nkuu Ndoo, Kata ya Machame Mashariki, Wilaya ya Hai, Kilimanjaro, ambayo ina walimu watatu pekee wanaofundisha wanafunzi 175, walimu wote wameandika barua ya kuomba uhamisho.
Walimu hao wanadaiwa kutoridhishwa na vitendo vya baadhi ya wazazi kutaka shule hiyo, wanafunzi wake wafundishwe na walimu wazawa.
Kutokana na madai hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Dionis Myinga, amekemea vikali hali hiyo, akisema serikali haihitaji ukabila, na wala haiendekezi hali hiyo, kwa kuwa Tanzania ni ya wote, mtu yeyote anaweza akafanya kazi kokote.
Akizungumza jana na Nipashe, mmoja wa wananchi wa Nkuu Ndoo (jina limehifadhiwa), amesema Ijumaa ya wiki iliyopita, Halmashauri ya Kijiji hicho, wazazi na wananchi, walikutana kutafuta ufumbuzi wa malalamiko ya mmoja wa walimu kufanyiwa vitendo vya kishirikina.
Alipotafutwa kuzungumzia jambo hilo kama lina ukweli, Mwenyekiti wa Kamati ya Elimu, Kijiji cha Nkuu Ndoo, Elimwaria Mbora ameisema, hilo la kuomba kuhama, ni kweli waliomba; kwa sababu ya kero ambazo zilitokea.
Amesema kuna mzazi, mtoto alichapwa, baada ya huyo mtoto kuacha begi uwanjani Ijumaa. Mwalimu akaliokota, Jumatatu yake wakati anamkabidhi mtoto begi akamwadhibu.