USHAURI WA KILIMO/MIFUGO
Yamenikuta...Mahindi yanaharibika shambani
Ugonjwa huo unaitwa "Common Smut" na unasababishwa na fungus aitwaye Ustilago maydis .
Huyu fungus anaishi kwenye udongo na anaweza kukaa kwenye udongo kwa miaka mingi.
Huwa anaingia kwenye mmea wa mahindi kupitia vidonda na mbegu zake hukua na kuwa mmea kamili. Huyu fungus hula sehemu za chembe za uhai (cells) za mmea na kuziua. Anashambulia sehemu yoyote ya mmea ikiwa ni shina, majani, masuke, na gunzi. Hutengeneza vinundu fulani ambavyo ukivipasua vinatoa unga mweusi. Unga huo punje zake ndio mbegu za Ustilago maydis.
Ugonjwa huu huenea kwa kusambazwa mbegu zake na upepo,maji,wanyama,nk.
KUDHIBITI COMMON SMUT
Ugonjwa huu wa common smut hauna dawa kwa hiyo njia ya kuudhibiti usitokee au usishambulie kwa kiwango kikubwa ni kama ifutavyo:
1.Tumia mbolea yenye uwiano mzuri wa nitrogen na phosphorus. Udongo wenye nitrogen nyingi hufanya mimea kuwa laini na kukua haraka. Mimea hii hushambuliwa kwa urahisi na ugonjwa huu. Lakini phosphorus ya kutosha huzuia mashambulizi kwa kuwa hufanya mmea kuwa imara na.mgumu. Epuka kutumia samadi nyingi.
2. Epuka kujeruhi mimea. Mimea yenye vidonda hushambuliwa kwa urahisi zaidi.
3.Dhibiti wadudu waharibifu. Wadudu hutoboa mmea na kuujeruhi kwa hiyo hufanya mmea ushambuliwe kwa urahisi.
4. Hali ya ukame hufanya mashambulizi kuongezeka kwa hiyo kama inawezekana epuka kipindi cha ukame kulima mahindi kama hutaweza kumwagilia maji.
5. Acha kupanda mahindi kwenye eneo lenye historia ya kutokeza ugonjwa huu mara kwa mara. Panda mazao mengine
6.Kulima kwa kugeuza udongo ili ule wa juu ufukiwe chini sana kunaweza kupunguza tatizo kwa huwa.huyu fungus huishi kwenye udongo wa juu.
7.Muhimu zaidi: Tumia mbegu zenye kustahimili ugonjwa hasa hybrids.
Ugonjwa wa comon smut hauna dawa ukishaingia shambani lakini hasara unayosababisha haizidi 5%. Ukizingatia njia hizo za kuzuia unaweza ukautokomeza shambani mwako.