JE, NAMBA 666 INAMHUSU PAPA?
Hili ni moja ya maswali yaliyopatwa kuulizwa na kujibiwa na Waseminari wa Seminari Kuu ya Peramiho kwenye Kipindi cha IJUE BIBLIA-REDIO MARIA
Swali hili limeulizwa na watu zaidi ya mmoja, kwanza limeulizwa na Catheline Lacha, yeye anauliza hivi; Kitabu cha Ufunuo kinamaanisha nini juu ya namba 666? Na je, Kaisari Nero aliyewatesa Wakristo wa mwanzo anahusianaje na namba 666? Pili, limeulizwa na makatekista wa Dekania ya Konsolata-Iring
a wakisema; Tunaomba tupate maelezo juu ya namba 666 inayozungumziwa katika kitabu cha Ufunuo. Tatu, limeulizwa na wana TYCs wa Songea Boys wakisema; Kitu gani kinaonesha kwamba maneno NERON KAISAR alikuwa memba wa Freemason? Na je, ni kweli herufi hizo zipo katika kofia ya Papa? Na zina maana gani?
Wapendwa mliouliza swali hili, napenda niwapongeze kwa swali lenu zuri kabisa, ambalo limeulizwa mara nyingi na kujibiwa mara kadhaa na wataalamu wa Maandiko Matakatifu. Hata hivyo tutalijibu ili tuendelee kuifahamu vizuri Biblia Takatifu na kujiimarisha katika imani yetu Katoliki. Na hivi naomba tufuatane kwa makini ili tupate kueleweshana na kuwekana vizuri kabisa, kwani siyo ninyi tu mnaopatwa na utata huo, wapo wengine ambao wao wamevuka mipaka ya kuuliza, wakuamua kutoa shutuma kwamba namba hiyo 666 inamhusu Papa au Baba Mtakatifu na imeandikwa kwenye mavazi yake, kitu ambacho si kweli kabisa.
Wapendwa wauliza swali, nanyi wasikilizaji wote wa Redio Maria, kimsingi swali hili ni moja lililoulizwa kwa namna tofauti tofauti, kwani linahusu namba 666 iliyoandikwa katika kitabu cha Ufunuo sura 13:18, na hivi naomba nitoe majibu ya pamoja kwa maswali yote matatu. Basi, namba yenyewe 666 inapatikana katika kitabu cha Ufunuo sura 13:18, hapo imeandikwa hivi; “Hapa ndipo penye hekima. Yeye aliye na akili, na aihesabu hesabu ya mnyama huyo; maana ni hesabu ya kibinadamu. Na hesabu yake ni mia sita, sitini na sita” (Ufu 13:18).
Mpenzi msikilizaji wa Redio Maria, kwa nukuu hiyo mwandishi wa kitabu cha Ufunuo alimaanisha jina la kiongozi wa dola ya Kirumi zamani zile, yaani Kaisar Nero. Hivi ni kweli kwamba Kaisar Nero aliyewatesa Wakristo wa mwanzo, anahusika moja kwa moja na namba 666, kwani namba hiyo ni hesabu ya jina lake ukikokotoa kwa kigematria, maneno NERON KAISAR kwa Kiebrania.
Hivyo namba hiyo, 666 ilimhusu na bado inamhusu kiongozi huyo wa dola ya Kirumi zamani zile na wala siyo kiongozi mwingine kama Baba Mtakatifu, na wala haikuandikwa kwenye mavazi yake, kama wanavyodai wale ambao wanasoma kwa makengeza kitabu cha Ufunuo, huku wakiwa na mawazo yao binafsi.
Na pia kinachoonesha kwamba Neron Kaisar alikuwa ni memba wa Freemasoni ni namba hiyo 666 ambayo ni namba ya Freemasoni na kuhusu suala la kuwatesa Wakristo na kutaka kuangamiza Ukristo ambalo ndilo lengo la Freemasoni pia.
Wapendwa wauliza swali, ili tuelewe vizuri sura hiyo ya 13 ya kitabu cha Ufunuo, ni vema na haki kabisa, tuzingatia kwamba kitabu cha Ufunuo wa Yohane, kina mazingira yake ya kihistoria ambayo ni muhimu kuyaelewa vizuri katika kujibu swali letu hili, na mazingira hayo ni ya historia ya dola ya Kirumi.
Mpenzi msikilizaji wa Redio Maria, kama nilvyosema ili tuelewe vizuri majibu yetu, hebu tutazame kwa kifupi maana, sifa na mazingira ya kitabu hiki cha Ufunuo. Ufunuo wa Yohane ni maandishi ya “kiapokaliptiko”. Apokalipsisi ni neno la Kiyunani lenye maana ya Ufunuo. Na hivi maandishi yote ya kiapokaliptiko ni aina ya ufunuo, kwani Mungu humfunulia mtu fulani mambo yaliyofichika ambayo mpaka sasa yamejulikana na Mungu tu. Mambo hayo yanahusiana hasa na siku za usoni. Si rahisi kuona hitirafu kati ya ufunuo waliojaliwa manabii na vitabu vya kiapokaliptiko.
Tofauti ni kwamba manabii wa zamani waliyasikia maneno ya Mungu na kuyakariri walipoyahubiri. Kumbe waandishi wa funuo za kiapokaliptiko hupewa funuo zao kwa njia ya njozi, na hatimaye huziandika njozi hizo katika vitabu fulani. Waandishi wa funuo za kiapokaliptiko huona njozi za mifano, hawaoni tukio lenyewe la siku za usoni. Hivyo mambo yote hufahamika katika njozi kama mfano wa kitu kingine. Kwa mfano huona vitu mbalimbali kama tarakimu, viungo mbalimbali vya mwili, wanyama na watu, na vinginevyo vinavyotajwa.
Hivi kitabu cha Ufunuo ni kitabu chenye habari zilizofunuliwa kwa mwandishi juu ya mipango ya siri za Mungu. Maandishi haya ya “ufunuo” yanapatikana pia katika Agano la Kale, kwa mfano katika kitabu cha nabii Danieli 7-12; Ezekieli 26-35 na Zekaria 9-14). Basi, kwa kawaida vitabu vya Ufunuo vinazingatia mfumo maalum wa uandishi wenye vipengele vifuatavyo; Mosi, utumiaji wa jina bandia, yaani mwandishi hajitambulishi kwa jina lake halisi, bali hutumia jina la mtu maarufu aliyeishi enzi za kale. Pili, maono, ni katika mazingira ya maono au ndoto mwandishi anapata fursa ya kuona siri za mipango ya Mungu.
Tatu, utumiaji wa ishara. Ni vema tujue kuwa, vitabu vya Ufunuo hutumia ishara mbalimbali kuwakilisha au kufikisha ujumbe uliokusudiwa kwa watu. Na katika kitabu cha Ufunuo wa Yohane kuna ishara za aina tatu, nazo ni; Mosi, ishara za vitu: kama macho (19:2), pembe (12:13), kiti cha enzi (4:4), kanzu ndefu (28:4), mabawa (4:8), lulu (17:4), upanga (6:4).
Aina ya pili ya ishara ni nambari. Nambari zinazotajwa mara nyingi katika Ufunuo wa Yohane ni namba nne (7:1), namba saba (1:12), namba kumi (2:10) na namba kumi na mbili (21:12). Aina ya tatu ya ishara ni rangi ya vitu kama nyeupe (3:5), nyekundu (6:4; 17:3-4). Nne na mwisho ni maelezo ya ishara. Maana ya ishara hutolewa na malaika wa Mungu kwa yule anayepata maono. Tano, mpangilio maalum wa mada. Mada moja hurudiwa mara kadhaa katika mtiririko uleule, lakini kila mara kwa kutumia lugha na ishara tofauti.
Na walengwa wa kitabu hiki cha Ufunuo walikuwa ni Wakristo walioteswa vikali kwa sababu ya imani yao (2:10). Baadhi ya waamini walikwisha kumwaga damu kama mashahidi (2:13; 6:9; 20:4). Madhulumu hayo yaliendeshwa rasmi na vyombo vya dola ya Kirumi. Kihistoria inajulikana kwamba watawala wa dola ya Roma walioitwa Makaisari waliwadhulumu sana waamini Wakristo kutokana na imani yao. Na Kaisari Nero aliyetawala tangu mwaka 54BK hadi 68BK alikuwa wa kwanza kuendesha madhulumu dhidi ya Wakristo walioishi mjini Roma.
Kiongozi mwingine aliyeendesha madhulumu ni Kaisari Domitiani aliyetawala kati ya mwaka 81BK na 96BK. Huyo alikuwa mtu katili sana na alijihisi ana hali za kimungu. Na hivi raia wote katika dola yake walipaswa kuungama kama kanuni ya imani maneno haya: “Kaisari ndiye Bwana.” Na pia wakati Domitiani alipoingia katika ukumbi wa mkutano, wote waliokuwemo ndani walitakiwa kumsalimu kwa maneno haya; “Salamu kwako wewe Bwana wetu na kwa mkeo.”
Na hivi Wayahudi na Wakristo waliokataa kumtii Domitiani waliadhibiwa vikali sana, na Wakristo waliokataa kutolea sadaka kwa heshima ya Domitiani ndiyo waliolazimika kumwaga damu yao, yaani kufa kifo cha kishahidi. Katika hali hiyo kuzingatia dini ya Kikristo iliyokataa kabisa kumtolea sadaka mwanadamu mtawala lilikuwa jambo la kijasiri na fundisho kwetu kuwaabudu na kuwasujudia wanadamu kwani hiyo ni heshima anayestahili apewe Mungu pekee.
Basi, Wakristo walipokuwa wakidhulumiwa na dola hiyo, mtume Yohane alichukua kalamu na kuandika ujumbe wa matumaini ili kuwaliwaza, kuwapa nguvu, na kuwafariji ndugu zake waliokuwa wakiteseka pamoja naye, chini ya utawala wa Kirumi.
Maandiko Matakatifu yanasema hivi, “Mimi Yohane, ndugu yenu na mwenye kushiriki pamoja nanyi katika mateso na ufalme, na subira ya Yesu Kristo, nalikuwa katika kisiwa kiitwacho Patmo, kwa ajili ya Neno la Mungu, na ushuhuda wa Yesu.
Nalikuwa katika Roho, siku ya Bwana, nikasikia sauti kuu nyuma yangu, kama sauti ya baragumu, ikisema, haya uyaonayo uyaandike katika Chuo, ukayapeleke kwa hayo Makanisa saba’ Efeso, na Smirna, na Pargamo, na Thiatira, na Sardi, na Filadelfia, na Laodikia” (Ufu 1:9-11).
Basi ndugu zangu, wakati Yohane anandika kitabu hicho, akawa anatumia lugha ya mafumbo, ili kusudi watesi wao wasifahamu wanayosemwa na kumwangamiza. Ndipo basi, utaona kisa cha joka kuu lenye pembe kumi na vichwa saba na juu ya vichwa vilemba saba nakadhalika. Katika maapokeo ya Wayahudi joka ni mfano wa kila enzi mbaya na adui wa Mungu na wa taifa lake, ndipo hapa, joka linamaanisha dola ya Kirumi, na mkubwa wa dola ya Kirumi naye akapewa jina la kupachikwa, ua jina la kupanga, yaani jina la kifumbo kwa mtindo wa kucheza na namba za jina lake ambapo tumesema ukikokotoa kigematria kwa Kiebrania unapata namba 666.
Mpenzi msikilizaji wa Redio Maria, ili kuonesha maana ya sura 13:18 ya kitabu cha Ufunuo na namna namba 666 inavyohusiana na Neron Kaisar aliyewatesa Wakristo wa mwanzo, nakualika tuone kwa pamoja ufafanuzi au tukokotoe kigematria hesabu ya jina hilo inayohesabiwa kwa konsonanti za Kiebrania NERON KAISAR.
Hapa katika maneno hayo mawili, Neron Kaisar, zipo herufi N-ambayo kwa Kiebrania ni Nuni, nayo thamani yake ni 50, ipo herufi R-ambayo kwa Kiebrani ni Reshi, nayo thamani yake ni 200, kuna herufi W-ambayo kwa Kiebrania ni Vavu, nayo thamani yake ni 6, ipo herufi Q-ambayo kwa Kiebrania ni Kofu, nayo thamani yake ni 100, na pia ipo herufi S-ambayo kwa Kiebrania ni Sini, ambayo thamani yake ni 60.
Na hivyo hesabu yetu inakuwa kama ifuatavyo; NERON KAISAR linazo herufi za Kiebrania
N(50)+R(200)+W(6)+N(50)+Q(100)+S(60)+R(200)=(666), na jumla yake ndiyo tunapata namba 666.
Basi pia ukikokotoa kigematria kwa maneno ya Kigiriki KAISAR THEOS, yaani Kaisar Mungu pasipo kuzungukazunguka utapata namba 616. Hii tafsiri ya KAISAR THEOS, yaani Mungu Kaisari ndiyo inayopatikana kwenye Biblia zile zenye kuandika jumla ya namba 616.
Lakini vile vile 616 inaweza kupatikana kwa kuondoa konsonanti N, ya mwisho kwenye jina Neron Kaisar katika Kiebrania kama tulivyokokotoa wote hapo awali. Hivyo basi ukikokotoa kigematria kwa kutumia konsonanti za Kiebrania NERON KAISAR, yaania Kaisari Neron unapata jumla ya namba 666 na ukikokotoa kigematria kwa Kigiriki maneno KAISAR THEOS, yaani Mungu Kaisari utapata jumla ya namba 616.
Hivyo ndugu yangu ukishaelewa kukokotoa kigematria jina hilo Neron Kaisar huwezi kupata shida na kuwabambikizia wengine jina lisilo lao. Na hivi kwa Wakristo wa mwanzo namba 666 au 616 ilipomtaja Neron Kaisar, ilisema pia kwamba ni mpinga Kristo kwani alikuwa ni kunyume cha ukamilifu. Unajua ukitazama kinambari kwa Wakristo utimilifu ni namba 777, nayo inapatikana ukikokotoa kigematria jina la Yesu, kumbe kwake yeye Neron namba yake ni pungufu ya ukamilifu, kwani hesabu yake ni 666 ambayo ni 777 ya ukamilifu kutoa 111. Na hivi kwa kuzingatia maelezo hayo, namba 666 inasimama badala ya Neron Kaisar na siyo mtu mwingine kama Baba Mtakatifu kama wengine wanavyosema.
Mpenzi msikilizaji wa Redio Maria na kipindi hiki cha Ijue Biblia, katika kusoma Biblia Takatifu, hakuna mahali popote ambapo msomaji ameombwa kutumia akili isipokuwa katika kitabu cha Ufunuo hususani sura ya 13:18, kwa kuwa ili kuipata hesabu hiyo kunahitaji mtu atumie au achezeshe ubongo ipasavyo, yaani akokotoe kigematria, na hivi wasomaji wote wa kifungu hiki, walialikwa na hivi hata sisi leo tunaalikwa kutumia akili katika kupiga hesabu hiyo. Ndiyo maana Maandiko Matakatifu yanasema hivi, “Hapa ndipo penye hekima. Yeye aliye na akili, na aihesabu hesabu ya mnyama huyo, maana ni hesabu ya kibinadamu. Na hesabu yake ni mia sita, sitini na sita” (Ufu 13:18).
Kumbe ndugu zangu, kinyume na matumizi ya akili, katika kifungu hiki, basi ndipo utakapoona wasomaji wengi “huingia mkenge” au hupoteza vichwa, yaani wasomaji wasipotumia akili zao hupotea na kushindwa kuelewa maana yake na hatima yake huishia katika ulalamishi, ubishi na utoaji wa majungu na uzingiziaji tu. Basi msikilizaji wangu, nakualika usomapo kitabu cha Ufunuo, sura 13 aya 18, utumia akili ili nawe usipotee katika kuelewa ujumbe wake ipasavyo.
Hapa wapo watu chungu nzima waliosoma kifungu hicho kwa makengeza ya akili zao, na hivyo kushindwa kuelewa maana yake na kuanza kueneza tafsiri potofu ama tafsiri isiyo sahihi ya namba 666, kwamba inamhusu kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, yaani Baba Mtakatifu na imeandikwa kwenye mavazi yake, kitu ambacho siyo kweli, kwani ni namba ya jina la Kaisar Neron aliyekuwa kiongozi wa dola ya Kirumi wa zamani zile, aliyewatesa Wakristo wa mwanzo.
Mpenzi msikilizaji wa Redio Maria, tukiendelea kujibu swali letu, naomba tujiulize, hivi ni nani, katika karne ya kwanza aliyekuwa adui wa Wakristo na jina lake linazaa namba 666? Bila shaka kama tulivyosema, alikuwa ni Kaisar Neron ambaye ukikokotoa kigematria jina lake unapata namba 666.
Tukitafsiri Biblia kwa usahihi huo, tunaona kuwa mtesi wa walengwa wa kitabu cha Ufunuo, aliyekuwa akifumbiwa katika sura 13:18, kwa hesabu ya jina lake kigematria, hawezi kuwa mtu wa karne ya tano au ya ishirini na moja. Ukweli ni kwamba walengwa wa kitabu cha Ufunuo walikuwa ni Wakristo wa karne ya kwanza na adui yao mkubwa alikuwa akiishi pamoja nao katika wakati huo, naye si mwingine bali ni Kaisar Neron.
Na hivi lengo la kitabu cha Ufunuo lilikuwa ni kuwatuliza waamini katika mateso yao, kuwahimiza waendelee kuzingatia imani yao. Kitabu kizima kinasema hivi, kwa kifupi, licha ya madhulumu makali mnayopata sasa hivi, hatimaye mtashinda. Muwe waaminifu kwa Yesu Kristo ambaye pia alimwaga damu yake, hivyo nanyi msikubali kusalimu amri inayowataka kumwabudu binadamu, kwani siku itafika Mungu atakapowaadhibu wale maadui zao.
Hapa, Wakristo waliyakumbuka maneno ya Yesu yaliyopo katika Injili ya Yohane sura 16:33, alipowaambia kwamba, “Hayo nimewaambieni mpate kuwa na amani ndani yangu. Ulimwenguni mnayo dhiki; lakini jipeni moyo mimi nimeushinda ulimwengu”. Na hivi Yohane katika kitabu cha Ufunuo anawafariji katika masumbuko hayo akisema kwamba yote yatabadilika na mambo yatakuwa shwari. Katika kueleza njozi zake Yohane anatumia mfano uliotumika na manabii wa zamani walipoeleza “Siku ya Bwana” (Amo 5:18).
Zamani hizo taifa teule lilidhulumiwa mara nyingi na Waashuru na Wakaldayo na Wayunani, na kuhamishwa mbali na nchi yao. Katika taabu hizo manabii walitabiri siku ya wokovu kwamba ipo karibu, na kwamba taifa hilo teule litajitawala na Mungu atawaadhibu maadui zao, hayo yote yatatokea siku ya Bwana. Yohane naye anatumia mfano huohuo katika kuelezea historia ya Kanisa, taifa jipya na teule, kwamba taifa hili jipya linadhulumiwa kama ilivyokuwa taifa teule zamani zile. Wakristo wengi wanauawa kwa sababu ya imani yao kama tunavyosoma katika Ufunuo 13; 6:10-11. Na madhulumu hayo yanafanyika na Warumi (Mnyama ailiyetajwa katika sura 13:1, na nyuma ya Warumi ni shetani, adui mkubwa kupita wote wa Kristo na taifa lake. Haya tunasoma katika kitabu cha Ufunuo sura 12 na 13: 2, 4.
Katika kufikisha ujumbe huo, ili watesi wa Wakristo wasiambulie chochote hata wakisoma kitabu hicho, ndiyo sasa mwandishi anatumia majina ya mafumbo au majina ya kupanga. Unajua ndugu yangu, watu hawatoi majina ya kupanga kwa watu wasio wafahamu, yaani huwezi kumpa jina la kupanga mtu ambaye hayupo au hajazaliwa bado. Wala hawatoi majina ya utani kwa watu wasiowajua au watu wasiowadhuru.
Hiki kitakuwa ni kituko ambacho ni sawa na kufukuza upepo wakati hufahamu unatoka wapi wala unaelekea wapi! Basi watu, hutoa majina ya kupanga au ya utani kwa watu wanaowafahamu na wanaowadhuru. Na hivi kufuatana na ukweli huo, walitoa jina hilo kwa Kaisar Nero aliyejifanya Mungu na kuwatesa Wakristo na hivyo kupewa jina la kupanga ambalo ukikokotoa kigematria jina lake kwa Kiebrania unapata jumla ya namba hiyo 666.
Tukizingatia mazingira ya kitabu cha Ufunuo, namba 666 au 616 haiwezi kusimama kwa ajili ya mtu mwingine kama Hitler, mtume Muhammad, Mussolini au Baba Mtakatifu. Hawa wote hawakuwepo enzi zile kilipoandikwa kitabu cha Ufunuo, na zaidi hawakuwa maadui wa Wakristo na hivyo wapewe majina ya kimafumbo. Naomba tuelewe vizuri kuwa hata wale wanaotoa shutuma kwamba namba hiyo imeandikwa kwenye mavazi ya Baba Mtakatifu, kwamba haipo na pia hakuna anayeweza kuonesha vazi hilo kwa ushahidi, kama ni maandishi ni mitra yake tu, yaani Kofia ile ya kiaskofu ambayo ina herufi mbili tu, nazo ni A na W ambazo ni Alfa na Omega kwa Kigiriki, yaani mwanzo na mwisho, ambayo tunapata katika sura ya 1:8, 17. Hivyo ndugu zangu kama tunatafuta uzima wa milele, basi tuache uongo na majungu kama haya ya kuwabambika watu majina yasiyo yao.
Hapa wapo pia wanaombambika Baba Mtakatifu namba 666, wakidai kuikokotoa namba hiyo katika majina matatu tofauti, yaani jina la Kilatini, VICARIUS FILII DEI (yaani Kaimu wa Mungu, jina la Kigiriki LATEINOS (yaani Mlatini) na jina la tatu ni la Kiebrania ROMIITH (yaani Mrumi), ukikokotoa majina hayo kigematria utapata namba 666 kadiri yao. Lakini tukumbuke kwamba kwa misingi halali ya kusoma Biblia hatuwezi kuyapokea majina hayo na kuyafanyia tahakiki ya kihistoria, kwani majina haya hayajawai kutumiwa na Baba Mtakatifu yeyote katika historia ya Kanisa, sembuse na karne ya kwanza baada ya Kristo wakati ambapo hata upapa wenyewe ulikuwa bado haujakua na kuanza kutumika.
Hakuna Papa ambaye aliwahi kuwa hatari na adui wa Wakristo, kwani Papa au Baba Mtakatifu ni Halifa wa Mtume Petro, askofu wa Roma, wakili wa Yesu Kristo duniani na mkubwa wa Kanisa Katoliki. Sasa kama ni wakili wa Yesu Kristo duniani, je, atakuwaje kinyume kwa kuwatesa wale walio wafuasi wa Yesu anayemwakilisha? Bila shaka hilo haliwezekani. Zaidi ni kwamba watu wasio hatari wangalipewaje majina ya kupanga ama ya siri? Ndugu zangu kwa hilo haiwezekani. Pia wale wasomaji wa kitabu cha Ufunuo wangelielewaje aya ngumu inayotaja kitu kisichojulikana kwao? Wangelifanyaje hesabu za kigematria kwa kutumia majina wasiyoyajua?
Hapa wapo ndugu zetu Wasabato na mafundisho yao ya Bibi Ellen White, ambaye katika kitabu chake kiitwacho VITA KUU, ametumia Biblia kufundisha na kuthibitisha chuki yake kinyume na ukweli, kwani katika kitabu hicho Ukurasa wa 18, amemtaja Papa kama ndiye aliyejitwalia majina ya Mungu. Pia Ukurasa wa 21, wa kitabu hicho VITA KUU, Bibi Ellen White anasema yule mdanganyifu mkuu (yaani shetani), alikuwa hajamaliza kazi yake. Aliazimia kukusanya jamii ya Wakristo wote chini ya uongozi wake, na kutumia nguvu zake kwa njia ya Askofu wa Rumi mwenye kujivuna na kujidai kuwa ni makamu wa Kristo. Kwa kifupa Bibi white anadai kuwa Papa ni mtumishi wa shetani.
Zaidi katika Ukurasa wa 24-wa kitabu hichi VITA KUU, Bibi White anasema mwanzo wa utawala wa Kanisa la Rumi ulikuwa mwanzo wa zama za giza. Kwa mafundisho hayo ya Bibi Hellen White, Wasabato wanaadai kwamba “mnyama” anayetajwa katika kitabu cha Ufunuo 13:1, ndiye Papa au Baba Mtakatifu.
Kwa mafundisho hayo tunaona wazi elimu ndogo ya Biblia aliyonayo Bibi Ellen White, kwani pia anatumia kitabu cha nabii Danieli na maelezo ya ndoto ya mfalme Nebukadreza, akidai kwamba maelezao hayo yanamhusu Papa. Lakini ukweli ni kwamba mwandishi wa kitabu cha Danieli hakuwa na wazo la kusema chochote kuhusu Papa.
Ndugu zangu, hapa wapo pia Wakatoliki ambao wameamua, kuyavulia maji nguo na kuyaoga ama kuwatolea uvivu wale wanaowasema kuhusu imani yao, hao wanapenda malumbano na hivi katika kujibu malumbano ya chuki na uadui, wametoa tafsiri mpya ya namba 666 kwa Wasabato.
Ndugu zangu matusi watu hawasomei darasani kiasi kwamba aliyefika darasa la juu au aliyechukua stashahada, ndiye mwenye uwezo wa pekee kuyapata matusi makubwa kabisa. Tukikumbuka hili, tuangalie mfano huu jinsi namba 666 inavyoweza kugeuzwa kwa yeyote. Madhalani, ukichukua kauli mbiu za Wasabato, namba 666 ni yao kwa nambari za Kilatini. Kwa mfano maneno ya Wasabato CURE VITAL SEVENTH DAY, ukikokotoa kigematria utapata namba 666, pia kauli mbiu inayosema CURATUS VITALE SABBATA DIES, ukikokotoa kigematria utapata namba 666. Tena Wasabato wanayo kauli mbiu nyingine inayosema SALVUS, CURARE SABBATA DIES, kigematria ni namba 666. Na maneno yao mengine yanasema, DEAL AXE VIE PAPACY, ukikokotoa nayo kwa kigematria utapata jumla namba 666. Mwisho kauli mbiu ya Wasabato inayosema SALVATION, CURE SEVENTH DAY, ukikokotoa kigematria utapata jumla ya namba 666 kwa nambari za Kilatini.
Wakatoliku hao wanadai kwamba kwa kadiri ya maandiko, mnyama anayetajwa katika kitabu cha Ufunuo na kidogo katika kitabu cha Danieli ni Kanisa la Wasabato. Wakianza na ufunuo 12:18, wanaonesha kwamba ni Wasabato na makanisa mengine yaliyosimama ufukoni maana yana makao makuu mjini New York, Chikago ua Los Angeles, miji ambayo imejengwa ufukoni na siyo Roma kwani Roma ipo kilomita 16 kutoka baharini.
Pia Ufu 18:4-5, inawahusu Wasabato na 13:4, inasema mnyama amepata kiti cha mamlaka yake kutoka Roma. Neno hili linawataja Wasabato kwani nguvu yao inatoka kwa taaifa kubwa la Marekani ambalo ndiyo Roma ya siku hizi.
Imeandikwa mnyama anatawala dunia miaka 1260, ndivyo ilivyo kwa Wasabato, kwani namba hiyo inapatikana kwa kuzidisha tarakimu za mwaka 1546 aliozaliwa, Martin Luther, mwanzilishi wa mageuzi karne ya 16, kwa idadi ya makanisa maarufu yaliyotokana na mafundisho yake, yaani Walutheri, Wakalvini, Wazwingli na nusu kanisa yaani Wasabato, na hivyo kufanya namba 3.5. Ndipo basi 15x4x6x3.5=1260.
Ya kwamba mnyama alipata dondo ambalo limepona (Ufu 13:3), ni Wasabato na wakubwa wao, kwani wamekuwa wakijaribu kutabiri mwisho wa dunia bila mafanikio, hadi mwaka 1980 walipaacha. Miaka waliyotabiri kuwaa mwisho wa dunia bila kutokea lolote ni 1874, 1878, 1914, 1925, 1932, 1939 na mwisho 1975.
Ya kwamba nguvu ya kisiasa na kidini inayoabudiwa inatimia tena kwa Wasabato, kwa maana wao ni kikundi cha kidini kinachosaidiwaa sana na taifa babe la Marekani.
Pia kwamba mnyama ametibua amri ya Mungu (Dan 7:25), inatimia tena kwa Wasabato kwa sababu badala ya kukazia amri mpya iliyoachwa na Yesu ya upendo (Yn 13:35, Mt 22:34-40), wao wanakazia amri ya kushika sabato iliyoachwa na Bibi Ellen White.
Basi Wakatoliki wanaopenda malumbano wanaendelea kujibu wakisema, kuwa wana kiongozi anayedai hadhi ya Mungu, inatimia kwa wasabato, ambapo wanmtukuza “nabii mke”, Bi Ellen White ama Charles Taze au Jonathan Cuming. Na dhambi wanayosamehe wao ni siasa, kwani waanajidai hawajihusishi nayo kabisa.
Zaidi ya hapo ni kwamba mama Kanisa kwa vile mabinti wametoka kwake (Ufu 17:5), inatimia kwa wasabato kwa sababu nabii Bi Ellen White ni kweli mwanamke wa kuzaa kama mama na kutokana na mafundisho yake kunazaliwa makanisa mengi kila siku.
Tena kwamba nguvu ya dunia inayoajabiwa (Ufu 13:3-4), inatimia sasa kwa wasabato kwani ijapokuwa wapo kidogo kiitikadi, hawaogopi kugombana na waamini wengine popote pale duniani.
Kwa kuongeza tu ya kwamba amefanya vita dhidi ya watakatifu (13:7), inatimia kwa Wasabato sasa, kwa sababu kwa vile wao hawalali usingizi katika kuwapiga vita Wakatoliki (ndiyo watakatifu wa Mungu, wavumilivu).
Ndugu zangu matusi watu hawasomei darasani kiasi kwamba aliyefika darasa la juu au aliyechukua stashahada, ndiye mwenye uwezo wa pekee kuyapata matusi makubwa kabisa. Tukikumbuka hili, tunaona pia mfano huu jinsi namba 666 inavyoweza kugeuzwa kwa yeyote. Madhalani, ukichukua kauli mbiu za Wasabato, namba 666 ni yao kwa nambari za Kilatini. Kwa mfano maneno ya Wasabato CURE VITAL SEVENTH DAY, ukikokotoa kigematria utapata namba 666, pia kauli mbiu inayosema CURATUS VITALE SABBATA DIES, ukikokotoa kigematria utapata namba 666.
Tena Wasabato wanayo kauli mbiu nyingine inayosema SALVUS, CURARE SABBATA DIES, kigematria ni namba 666. Na maneno yao mengine yanasema, DEAL AXE VIE PAPACY, ukikokotoa nayo kwa kigematria utapata jumla namba 666. Mwisho kauli mbiu ya Wasabato inayosema SALVATION, CURE SEVENTH DAY, ukikokotoa kigematria utapata jumla ya namba 666 kwa nambari za Kilatini.
Basi ndugu zangu tuache ubishi, na tubaki na ukweli mmoja kwamba sura ya 13:18 ya kitabu cha Ufunuo ilizungumzia jina ambalo wasomaji wake walikuwa wakilijua kama ni jina la adui yao, yaani Kaisar Neron aliyekuwa akiwatesa na kuwadhurumu Wakristo wa mwanzo na siyo jina la ndoto au majungu ya karne ya ishirini na moja ama karne hii tuliyonayo sasa. Wapendwa wasikilizaji naomba tukumbuke kwamba, watu wanapotukana, kila mmoja anaweza kulipa tusi kubwa na kumtukania mwenzake.
Hivyo ndugu zangu kwa heshima ya Maandiko Matakatifu, tuitafsiri namba 666 kwa kukokotoa kigematria asili na kukomea hapo. Tusiende mbali na kuingiza majungu na ubunifu wa uongo. Tusiihamishe namba hiyo na kuwapachika watu wasio na hatia. Kufanya hivyo ni kujiongezea majungu na ni dhambi ambayo kwa Mkristo anayeitafuta zawadi ya uzima wa milele haifai.
Basi, ndugu zangu tunapolisoma Neno la Mungu ili lituambie tunachopaswa kufanya au kukiacha ili tupate uzima wa milele, badala yake tukaichukua Biblia kupigania, hivi ndivyo tunavyoweza kugeuziana matusi. Kumbe kufanya hivyo itakuwa ni kumkasirisha Mungu.
Sasa tuelewe kuwa Mungu ametupatia sisi watoto wake, Wakristo, Biblia kama tunda, mamoja liwe chungwa, embe au ndizi na mengine. Tukiwa watoto wema tutalila hilo tunda ili tujipatie vitamin C tunayohitaji sana kwa afya zetu. Kumbe, tukiwa watoto wabaya Biblia itakuwa ni silaha ya kupigania na hivyo kuwa sumu ya kutuingiza motoni mwa milele.
Basi hili la pili tumuombe Mungu atuepushe mbali nalo, ili sisi tubaki watoto wema wa Mungu na hivyo tufaidi tunda tulilopewa na Mungu ili tuurithi uzima wa milele.
Tusimwangushe Mungu kwa kugombana na kusemana sisi wa sisi huku tukitumia Biblia kwa kuupotosha ujumbe wake.
Kwa kukazie tuseme namba 666 au 616 haimhusu Papa wala Baba Mtakatifu yeyote, na ukimwona mtu anadai hivyo ujue kwamba kama ulikuwa hujakumbana na mbeya ndiyo sasa umekutana naye katika nafsi ya mtu huyo, haijalishi awe askofu, padre, mhubiri, mchungaji au mwinjilisti.
Na wewe Mkristo mwenzangu, umbeya siyo suala lako, achana naye, na uisome Biblia Takatifu yako na kuitafsiri kwa utulivu, huku ukimwomba Mungu Roho Mtakatifu akusaidie kuelewa vizuri ujumbe wake na siyo kwa majungu na ulalamishi wa kusemana kama vile tungelikuwa watoto wa shetani., wakati sisi ni watoto wa Mungu.
Mpenzi msikilizaji wa Redio Maria, hadi hapa naomba nihitimishe jibu langu kwa swali lililoulizwa, kwanza na Catheline Lacha akisema hivi; Kitabu cha Ufunuo kinamaanisha nini juu ya namba 666? Na je, Kaisari Nero aliyewatesa Wakristo wa mwanzo anahusianaje na namba 666? Pili, limeulizwa na makatekista wa Dekania ya Konsolata-Iring
a wakisema; Tunaomba tupate maelezo juu ya namba 666 inayozungumziwa katika kitabu cha Ufunuo. Tatu, limeulizwa na wana TYCs wa Songea Boys wakisema; Kitu gani kinaonesha kwamba maneno NERON KAISAR alikuwa memba wa Freemason? Na je, ni kweli herufi hizo zipo katika kofia ya Papa? Na namba hizo zina maana gani?
Basi, kama tulivyosema katika jibu letu la msingi, ni kwamba mwandishi wa kitabu cha Ufunuo katika sura 13:18, alimaanisha jina la kiongozi wa dola ya Kirumi zamani zile, yaani Kaisar Nero, na hivi Kaisar huyo ndiye anayehusika moja kwa moja na namba 666, kwani namba hiyo ni hesabu ya jina lake, na namba yenyewe 666 inapatikana katika kitabu cha Ufunuo sura 13:18, hapo imeandikwa hivi; “Hapa ndipo penye hekima. Yeye aliye na akili, na aihesabu hesabu ya mnyama huyo; maana ni hesabu ya kibinadamu. Na hesabu yake ni mia sita, sitini na sita” (Ufu 13:18).
Ukikokotoa kigematria maneno Neron Kaisar kwa Kiebrania kama tulivyosema hapo awali utapata jumla ya namba 666 na ukikokotoa kigematria kwa Kigiriki maneno KAISAR THEOS, yaani Mungu Kaisari utapata namba 616 kwenye Biblia zinazoandika hivyo. La msingi tujue iwe ni namba 666 au 616 zote zinamhusu Kaisar Nero aliyekuwa mtesi wa Wakristo wa mwanzo.
Mpenzi msikilizaji wa Redio Maria, kwa nukuu hiyo katika kitabu cha Ufunuo sura 13:18, mwandishi alimaanisha jina la kiongozi wa dola ya Kirumi zamani zile, yaani Kaisar Nero. Hivi ni kweli kwamba Kaisar Nero aliyewatesa Wakristo wa mwanzo, anahusika moja kwa moja na namba 666, kwani namba hiyo ni hesabu ya jina lake ukikokotoa kwa kigematria, maneno NERON KAISAR kwa Kiebrania.
Hivyo namba hiyo, 666 ilimhusu na bado inamhusu kiongozi huyo wa dola ya Kirumi zamani zile na wala siyo kiongozi mwingine kama Baba Mtakatifu, na wala haikuandikwa kwenye mavazi yake, kama wanavyodai wale ambao wanasoma kwa makengeza kitabu cha Ufunuo, huku wakiwa na mawazo yao binafsi. Na pia kinachoonesha kwamba Neron Kaisar alikuwa ni memba wa Freemasoni ni namba hiyo 666 ambayo ni namba ya Freemasoni na kuhusu suala la kuwatesa Wakristo na kutaka kuangamiza Ukristo ambalo ndilo lengo la Freemasoni pia.
Na huo ndio mwisho wa jibu langu kwa swali linalohusu ufafanuzi wa namba 666 inayopatikana katika kitabu cha Ufunuo sura 13 aya 18. Asanteni sana kwa kunisikiliza, Mungu mwema awabariki!