Kwanini Watanzania na Tanzania ni masikini pamoja na rasilimali (resources) tulizonazo?
...Kwa sababu ya kuwa na Viongozi wabovu ambao wanagawa rasilimali (Dhahabu, Almasi, Uranium, Tanzanite, misitu, Wanyama, ardhi n.k) za nchi kwa wachukuaji katika bei ya kutupa mwaka nenda mwaka rudi.

Haingii akilini kabisa nchi yenye utajiri mkubwa kama ya kwetu ishindwe kulipa hata mishahara ya Wafanyakazi wake. Mwaka 2010 mapato ya dhahabu yetu yalikuwa $1.5 billion lakini tulichoambulia hapo ni kidogo sana lakini hao wanaojiita Viongozi hawaoni kabisa tatizo la kugawa utajiri wetu wa nchi huku aslimia kubwa ya wananchi wakiwa wanaishi katika maisha yaliojaa ufukara wa kutisha!!! Shamba la bibi hilo wacha wavunaji wajichukulie.
 
Sli ni zuri sana nami ninakupa pongezi kwa kulileta huku, tusio wavivu wakusoma tumesoma mpaka nukta.

Majibu ya sababu za umasikini wetu:

1. Siasa chafu/uongozi usio makini,
2. Kukosa sera endelevu zinazotokana na kuchanganya siasa, utaalamu, maendeleo
3. Dhana ya kutokukubali kuwa tuna wajibu wakuwajibika katika kujadili chanzo cha umasikini wetu
4. Hisia kuwa Watanzania tunategemea IMF na nchi za magharibi kutatua matatizo yetu
5. Uvivu wa kufikiri, kusoma, kuweka mipango n kujiwekea muda wakufikia ma azimio fulani
6. Mfumo mmbovu wa elimu; kwa mfano kuongeza udahili wa wanachuo bila kuzingatia ubora wa wadahiliwa na uwezo wa vyuo
7. Kushindwa kutumia fursa tulizonazo kigeografia kwa mfano bahari, ardhi yenye rutuba, mito na maziwa kedekede....
8. Kushindwa kujitambuua tunapaswa kufunguka
9. Ubinafsi ie jeshi la mtu mmoja
10. Kukosa vipaumbele kulingana na rasilimali zilizopo eg. kujenga shule za kata zisizokuwa na waalimu wala vifaa, kutambua kuwa un ishi kwa cash burget and yet unawaongezea wanasiasa posho badala yakuzielekeza kwenye sekta nyeti kama elimu, kusheherekea miaka 50 ya uhuru kwa billions of money (65Billion) etc
11. Kushindwa kuwapa watu n afasi kulingana na taaluma zao na uwezo wao wa kuongoza
12. Elimu iliyo na mfumo wa nadharia zaidi na kutokumuandaa mtanzania kuwa na dhana ya kujiajiri
13. Udhibiti mbovu wa mapato na misamaha ya kodi isiyo na tija
 
a. Viongozi wabovu; wachoyo na wanaopenda wananchi wawe maskini ili watawale kirahisi 1961-1985...

b. Viongozi wabovu; wachoyo na wanaopenda kutumia akili za IMF na WB kuliko akili zao na wananchi wao 1985-1995

c. Viongozi wabovu; wachoyo na walafi kuibia wananchi, kuuza mali za umma, kuingia kwenye miktaba mibovu 1995-2005

d. Viongozi wabovu; wachoyo na wanaopenda kutumia akili za IMF na WB kuliko akili zao na wananchi 2005-2015..

Tatizo la kwanza uongozi, la pili wananchi na la tatu technology
 
Hoja nzuri Mkandala,

Sidhani kama watz ni wavivu wa kazi. Ujanja na ubabaishaji ndivyo vinakatisha watu tamaa. Kuna watu wako tayari kwenda hata vijijini wakalime. Lakini hakuna msaada wa serikali. Kuna kundi la marasta waliwahi kutoka Dar wakahamia maeneo ya Kilosa ili wakalime. Sijui wale ndugu waliishia wapi! Utalimaje bila pembejeo? Utalimaje bila soko? Hayo ni majukumu ya serikali. Hebu angalia mahindi yanavyooza kwenye ma-godown kule Songea na Sumbawanga. Mwisho yanananuliwa kwa mkopo, tena kwa bei ya hasara. Wakulima wakiomba wawekewe utaratibu wauze mahindi yao Zambia na DRC, kosa la jinai.

Umaskini wetu ni umaskini wa kimfumo. Hautokani na uvivu hata kidogo. Serikali haijaandalia wananchi mifumo inayowasisimua kufanya kazi. Hebu kumbuka wale wakulima pamba kule Shy? Watu wanafanya kazi mpaka tone la mwisho la damu, lakini mwisho hakuna soko. Tunategemea wafanye nini zaidi? Yaani kutokana na ubabaishaji mwingi serikalini, wananchi wengi, na hasa vijana, wameamua kujikatia tamaa. Wengine wamekata tamaa hata kabla hawajajaribu kwa sababu wanaona wanaojituma wanavyokula hasara.

Hata hii tabia ya kulalamika iliyosambaa kila kona ya nchi inabidi tuiangalie vizuri. Hivi watu watashindwaje kulalamika wakati mambo hayaendi? Malalamiko ni ishara kwamba mfumo hauko sawa. Tunataka wananchi wafanye nini wakikosa dawa hospitalini? Watoto wao wakikosa walimu shule za kata? Wakinyang'anywa ardhi yao bila fidia? Dhahabu yao ikisombwa kila siku na makampuni? Akiba ya nchi ikiporwa mabilioni kwa mabilioni hazina? Hivi tunategemea wafanye nini? Ni lazima watalalamika tu.

Kitu ninachojiuliza kwa watu wetu ni uoga wa kufanya mabadiliko ya kiutawala. Watalia weeeeeeeeeeeee, uchaguzi ukija wanawapa hao hao. Mimi huo ndio upungufu mkubwa ninaouona kwa watz. Hebu fuatilia hata huu uchaguzi mdogo wa Arumeru Mashariki. Nchi iko taabani. Nchi inaporwa. Viongozi wanashindana kujiongezea posho. Wakati huo hakuna dawa hospitalini. Lakini mwisho wa siku utashangaa kuona bado CCM inapata kura. Mimi huwa nikifika hapo huwa ujanja wote unaisha. Inabidi nimuachie Mungu tu.

Tabia hii ndiyo inafanya hata wasomi na wakereketwa wengine waamue kutulia tu au kujiunga na mafisadi. Kwa sababu, hata ukilianzisha, hakuna mtu atakayekuunga mkono. Utaishia kusakamwa binafsi, utaundiwa kesi bandia, n.k. Kazi ipo ndugu zangu. Kwa kifupi, umaskini wetu unatokana moja kwa moja na viongozi wasio na machungu na nchi. Hakuna jitihada binafsi zitakazotutoa hapa bila kujitoa mhanga na kubadili mfumo wa utawala. Vile vile, malalamiko yataendelea tu kwa sababu mambo hayaendi.
 
a. Viongozi wabovu; wachoyo na wanaopenda wananchi wawe maskini ili watawale kirahisi 1961-1985...

b. Viongozi wabovu; wachoyo na wanaopenda kutumia akili za IMF na WB kuliko akili zao na wananchi wao 1985-1995

c. Viongozi wabovu; wachoyo na walafi kuibia wananchi, kuuza mali za umma, kuingia kwenye miktaba mibovu 1995-2005

d. Viongozi wabovu; wachoyo na wanaopenda kutumia akili za IMF na WB kuliko akili zao na wananchi 2005-2015..

Tatizo la kwanza uongozi, la pili wananchi na la tatu technology

Kwahiyo mtazamo wako ni kwamba tatizo kubwa ni uongozi. Fine. Tukianza na seheme ya kwanza hapo juu i.e. 1961 - 1985, Nyerere inaonekana ndio unamlenga hapa. Alipenda wananchi wawe maskini, awatawale kirahisi ili afaidike na nini kama nyerere? Sehemu 'b' contradicts with sehemu 'a' in the sense kwamba sehemu 'a' kulikuwa na self determination, sio WorldBank na IMF. Vinginevyo sehemu b, c, and d, naunga mkono hoja kwa kiasi fulani, ingawa Mwinyi kwa kiasi fulani hakuwa na jinsi.

Ila nina swali - Je, kwa mtazamo wako, sababu kuu ya umaskini wetu ni sababu za ndani tu? Sababu zote za umaskini wetu zipo ndani ya uwezo wetu?
 
Shukran sana umetimiza moja ya sababu za umaskini wetu.. Hatupendi kusoma...Mkuu, nimefanya makusudi kabisa kuandika hivi ili nipate kuona ni wangapi watapenda kuisoma yote na kutambua mapungufu yetu..

Bandiko hilo hapo juu ndilo lilonishawishi kurudi kwenye post ya kwanza ya uzi huu.

Vurugu zote hizo hapo chini nilikuwa najaribu kutafuta kuona kama umekuja na wazo jipya la ufumbuzi wa juu ya swali la msingi ulilouliza katika 'title' ya uzi huu. Nimejitahidi kusoma neno kwa neno na kutafakari kwa muda kila sentensi uliyoandika kwa utulivu. Nasikitika kukwambia/kukuandikia kuwa sikuona jipya. Sikuona suluhisho la swali hilo la msingi. Umeishia kulalamika tu juu ya hali halisi iliyopo hapa nchini. Ninachokijua sifa nyingine ya ziada ya Great thinker akishakuona tatizo,akalitafakari , akaelewa kiini chake anatakiwa aje na suluhisho la tatizo hilo. Suluhusho hilo linatakiwa liwekatika maelezo yanaoeleweka kwa kada zote zinazohusika. Huo ndio mtazamo wangu juu ya namna ulivyoleta mada yako. Ninakuomba unisamehe kama nitakuwa nimekukwaza kwa jinsi nilivyotafakari chapicho/andiko/post yako.

...............
Baada ya kuwa mwanajanvi wa JF kwa muda mrefu sana, kusoma mabandiko mbalimbali na kusoma makala za magazeti, mawazo ya wasomi wetu na kadhalika nimegundua kitu kimoja ya kwamba sisi Watanzania - We are into denial..Ni maskini lakini hatudhani kama sisi ni maskini kweli na tumejenga fikra za kwamba MTU akifanya kazi kwa bidiii kubwa bila shaka ataweza kufanikiwa kutokana na umaskini. Lakini tunasahau kwamba Umaskini ni stage ya mtu kukwama ktk hali na mali na mbinu zinazotumika hapa ni tofauti kabisa na zile za kujiendelea mbele. Sasa unapoweka nguvu kubwa ktk uzalishaji kweli unaweza kujiondoa ktk umaskini hali umaskini unatokana na sababu zake kama vile gari lililokwama tunatakiwa kutazama limekwamba wapi ktk tope, mchanga au shimo na ndipo tutafahamu jinsi ya kujikwamua na sii kuganyaga mafuta kuongeza kasi. Magurudumu yatazunguka tu hatutatoka hapo tulipokwama.

MTU, hili neno pekee linajenga Ubinafsi na kubomoa nguvu ya jumla, inavunja Utaifa na kuelekeza mapambano haya kwa fikra za kila mmoja wetu atachunga mzigo wake kama abiria walikosa matumaini ya usafiri baada ya gari lao kukwama na hivyo kila mmoja wao atafute usafiri wake..Fikra hizi za kila mmoja atafute usafiri wake, ndicho kinachofanyika nchini na ndio sababu tumeshindwa kutoka ktk umaskini maana sote tumeliacha gari la Taifa lilipokwama na kila mmoja wetu anatazama usafiri wake hali tuko katikati ya msitu na pasipo dira..na maskini ya Mungu hatufahamu tunaelekea wapi. Ni kweli kabisa kwamba uongozi mbaya ndio ulotupeleka ktk korongo hili la umaskini na tumekwama lakini sio uongozi mbaya unaotufanya tuchukue maamuzi ya kila mtu abebe msalaba wake..

Je, tunafikiri fikra za kwamba tukipata kiongozi au uongozi mzuri tutaweza kujinasua ktk umaskini tulipokwama? na huyu kiongozi au viongozi wanatakiwa wawe na moyo gani, wananchi wenyewe wanaweka matumaini yapio ikiwa leo kila mmoja wetu anadai maisha magumu aongezewe mshahara na posho ili hali wanajua fika kwamba tumekwama sote. Hivi kweli ikiwa wabunge kujiongezea posho ni makosa basi yatulazimu sisi wote tuombe raha hizo sawa na wao japokuwa tunajua fika kwamba wanayodai viongozi wetu ni makosa makubwa na ndizo sababu zinazotuweka ktk umaskini?..Ndizo sababu zinazotufanya tuwatake waondoke ktk madaraka na mageuzi ya kweli lazima yazingatie kwanza kwamba tumekwama na uzalendo unatakiwa kwanza.

Watanzania wenzangu ifike mahala tufikirie tumetoka wapi na tumekwama wapi, badala ya kuendelea kufikiria tunakwenda wapi.. Tanzania tumekwama ktk umaskini na tumeshindwa kutoka ktk umaskini. Na kibaya zaidi ni kwamba - WE CAN"T HANDLE THE TRUTH!.. bado tupo ktk kuamini kutoamini kwamba tuna watu wachache sana WAZURI (A few good men) ktk ngazi zote za uongozi na uwajibikaji kuweka Uzalendo mbele ya kila kitu. Hivi kweli Utawala wa leo toka Azimio la Zanzibar wamekosa aibu kabisa ya kufikiria Ufisadi mkubwa wanaoufanya kwa wananchi wao huku wakiendesha siasa za chuki baina ya watanzania kwa kutumia mapungufu ya Mtanzania huyo (ujinga, umaskini na maradhi) kama nyenzo ya kumuumiza zaidi.

Tuna msemo wa kwamba TAIFA MBELE? hivi tunaposema Taifa kwanza huwa tuna maana gani? Ni vitu gani vinatangulia ktk kulinda maslahi ya Taifa hadi tuseme TAIFA kwanza hali nafsi zetu zimegawanyika ktk makundi ya Ukabila, dini, rangi wanawake na wanaume, vyama na kadhalika. Hivi tunaposema Utaifa kwanza huwa tunatazama sifa zipi za uzalendo ikiwa kila mmoja wetu anatafuta riziki yake, anapanga malengo yake kwa manufaa ya maslahi yake ikiwa ni haki yake ya kuzaliwa na kama mtu huru?. Nini maana na kipimo cha UTU wa kila mmoja wetu ktk Utaifa wetu na huu utaifa unatokana na mipaka gani?.

Wanabodi lazima tukubali ukweli uliosimama ya kwamba tumeshindwa!...TUMESHINDWA!... na hakuna njia bora zaidi ya kufikiria - Ikiwa kweli tumeshindwa, je tulikosea wapi?... Mada nyingi sana hapa JF zinazungumzia sana matumizi mabaya ya mamlaka kwa viongozi wetu lakini katu tumeshindwa kujitazama sisi wenyewe sote kama ni MASIKINI na tumekwama ktk umaskini kama Taifa na sii mtu au kundi la watu pekee.. Vita ya kujikomboa kutokana na umaskini, ujinga na maradhi imekuwa sii vita ya kitaifa japokuwa tunasema na kulalama siku zote kwamba sisi ni Maskini.

Ebu tufikirie mfano mmoja mdogo sana ktk kutazama mbinu za kidunia ktk ubunifu. Leo hii Somalia wako ktk matatizo makubwa ya Ukame (drought and famine) na wamekwama... Hivi kweli itakuwa busara kwao leo kufikiria kupambana na matatizo haya ya ukame inatakiwa regime change?.. au kila mmoja wao atie nguvu ktk uzalishaji. Kama ndivyo tumewahi jiuliza kwa nini Somalia imeshindwa kuondokana na vita kwa zaidi ya miaka 20 sasa hivi hadi wamefikia hapo walipo!...
- Je, kumpata kiongozi bora inaweza kuwaondolea njaa na ukame ili hali regime change na nguvu ya kumtafuta kiongozi bora zaidi ndio chanzo cha mtafaruku baina yao toka aondolewe Siad Barre na leo wamefikia hapo walipo?..
- Je, sii kweli kwamba ukame ni matokeo ya vita ambayo imetokana na kupoteza UZALENDO unaomfanya kila mmoja wao kuto heshimu na kuwajibika kwa taifa lake kwanza. Somalia wamekwama na hawataweza kujikwamua hata siku moja kama hawatarudi nyuma na kutazama jinsi gani walipoteza Utaifa wao.

Kwa hiyo, wanabodi tuumize vichwa vyetu kutazama tumekwama wapi na sababu zipi zilizotukwamisha na sii wapi tunakwenda ama tunataka kwenda. Ni imani yangu kwamba siku tuloomba Uhuru tulijua fika tunataka kwenda wapi na nadhani hakuna shida ya leo kujua tunataka kwenda wap bvali kuondoka ktk shimo hili la umaskini tulipokwama. Ni lazima tukubali vichwani mwetu kwamba tumekwama ili tupate kufikiria na kutunga mbinu zote za ujasiri, mhanga na uzalendo zilenge ktk kujinasua ktk shimo hili.

Hao Somalia leo hawawezi kufikiria kutafuta chakula kilichopikwa na chef toka hotel za nyota tano kama suluhisho la ukame. Itakuwa ujinga na ulimbukeni mkubwa sana lna bahati mbaya sisi Watanzania tunajaribu sana kutafuta suluhisho la umaskini wetu kwa kutafuta vitu kutoka nyota tano, kutafuta ushauri wa ki nyota tano bila kujali kwamba tumekwama. Huu ni ulimbukenii wa kuficha uchafu wetu wenyewe, ni ulimbukeni wa kujisitir aibu na kamwe hatuwezi kupambana na imaskini kwa majigambo na usanii wa kuweka viraka ktk nguo iliyochakaa. Watanzania wenzangu hatuwezi ondokana na Ujinga umaskini na maradhi ikiwa vita hii ni ya mtu mmoja mmoja kwa fikra kwamba umaskini wetu ni wakujitakia, kila mmoja wetu atabeba msalaba wake wa matatizo.

Sio Ufisadi wala uongozi mbaya ndizo sababu kubwa, bali haya yote ni matokeo ya upungufu ktk imani inayomjenga mtu mmoja mmoja kujinasua ktk lindi la Umaskini, hivyo ktk jitihada za kujikomboa tunajikuta tunakanyagana hovyo kila mmoja wetu akitaka atoke yeye kwanza utafikiri kaa wa bahari waliowekwa ktk kapu wakisubiri kutiwa ktk sufuria la maji ya moto.

Hivi kweli watumishi wa umma hasa wataalam na mabingwa wetu wanaolipwa mshahara chini ya mil 2 lakini hupewa nyumba, wasilipe maji na umeme, wamepewa fursa ya kufanya biashara nje ya ajira walizoajiriwa wakijenga conflict of interest kiutawala kwa taaluma zao ili kujineemesha bado wana haki ya ki UTU kudai wao malipo zaidi kutokana na ugumu wa maisha japokuwa wanajua fika kwamba Tanzania ni nchi maskini na tumekwama kt umaskini. Viongozi wetu ngazi zote za kijamii tafadhali lihurumieni Taifa letu, wahurumieni waja wenu walipa kodi maana mnawaweka ktk nafasi ngumu sana ya kufikia maamuzi ya kinyama maana tofauti baina ya binadamu na mnyama kifikra ni ndogo sana..
 
Tatizo lenu kubwaa amjielewi na wala mbinu sahihi amzielewi. Policies za mfumo wa Ubepari amzielewi, policies za command economy amzielewi worst of policies za mixed economy amzielewi to work on ya advantage; in short your doomed.

Tazameni policies zenu za imported zipo vipi and export zipo vipi and how do you improve you are exports. Tazameni what you import and what are the implications of those goods in your market (do you even make policies based on comparative advantages im thinking in terms of taxes to encourage internal growth), tazameni tax codes zenu za importations in all goods and analyse how do they affect your market.

Socialism growth and capitalism growth require different policies to propel growth, haya jiulizeni mna watu wangapi wakukuza uchumi wenu bila ya kuomba wawekezaji kutoka nje a jinsi mikopo yenu mnavyotoa na interest rates zenu zikoje to encourage businesses s. In short mna mambo mengi na ujinga mwingi maana hapa tukishuka tutafika mpaka kwenye umuhimu wa elimu na risk takings kama mko kwenye capitalism or the need for the government to have adjusted policies that aim boost the economy.I aim tired you people are doomed. Jamani mstifuatile wengine we jus dont give a **** anymore. Saving Tz is a long mission and we are not interested, but it would help if Mustaffa Mkullo was sacked.
 
Kwahiyo mtazamo wako ni kwamba tatizo kubwa ni uongozi. Fine. Tukianza na seheme ya kwanza hapo juu i.e. 1961 - 1985, Nyerere inaonekana ndio unamlenga hapa. Alipenda wananchi wawe maskini, awatawale kirahisi ili afaidike na nini kama nyerere? Sehemu 'b' contradicts with sehemu 'a' in the sense kwamba sehemu 'a' kulikuwa na self determination, sio WorldBank na IMF. Vinginevyo sehemu b, c, and d, naunga mkono hoja kwa kiasi fulani, ingawa Mwinyi kwa kiasi fulani hakuwa na jinsi.

Ila nina swali - Je, kwa mtazamo wako, sababu kuu ya umaskini wetu ni sababu za ndani tu? Sababu zote za umaskini wetu zipo ndani ya uwezo wetu?

Well watu nyerereism lazima muogope kwamba tunamlenga kwasababu ni ukweli; ili apate nini nimesema ili AWATAWALE kirahisi amefanikiwa ndio maana ame-over stay 24 yrs bankrupty country and people ...

Yes sababu kubwa ni ya ndani; na ni uongozi mbovu; kwani uongozi wa ndani unatakiwa ufanye analysis za external effects na kufanya uamuzi ambao ni kwa faida ya wananchi wake..

Umaskini ni tatizo la uongozi mbovu 1961-1985; 1985-1995 to date
 
Bandiko hilo hapo juu ndilo lilonishawishi kurudi kwenye post ya kwanza ya uzi huu.

Vurugu zote hizo hapo chini nilikuwa najaribu kutafuta kuona kama umekuja na wazo jipya la ufumbuzi wa juu ya swali la msingi ulilouliza katika 'title' ya uzi huu. Nimejitahidi kusoma neno kwa neno na kutafakari kwa muda kila sentensi uliyoandika kwa utulivu. Nasikitika kukwambia/kukuandikia kuwa sikuona jipya. Sikuona suluhisho la swali hilo la msingi. Umeishia kulalamika tu juu ya hali halisi iliyopo hapa nchini. Ninachokijua sifa nyingine ya ziada ya Great thinker akishakuona tatizo,akalitafakari , akaelewa kiini chake anatakiwa aje na suluhisho la tatizo hilo. Suluhusho hilo linatakiwa liwekatika maelezo yanaoeleweka kwa kada zote zinazohusika. Huo ndio mtazamo wangu juu ya namna ulivyoleta mada yako. Ninakuomba unisamehe kama nitakuwa nimekukwaza kwa jinsi nilivyotafakari chapicho/andiko/post yako.
Dah ama kweli sasa wewe unafanya ubishi ule ule unaoturudisha nyuma. sasa kama ningekuwa na jibu si ningeandika kichwa cha mada kisomoke - Hili ndilo suluhisho la umaskini wetu?

Hivi huoni kama mada yenyewe ni swali ambalo wewe ulitakiwa kuumiza kichwa chako kama wengine badala yake unamtegemea Mkandara aje na jibu kwanza, wewe hutaki kuumiza kichwa bali utafutiwe majibu kama tunavyotegemea viongozi wetu ndio wenye majibu yote... Mimi nimezisema sababu ya Umaskini na nimeuliza wapi tumekwama jambo ambalo mimi binafsi natafuta wapin tumekwama ingawa najua tumekwama.. Maswala ya Uongozi mbaya, siasa mbovu na kadhalika ndio yote haya yametufiisha ktk shimo, matope au mchanga na tumekwama.

Sasa ili tujikwamue ndipo napokuuliza wewe Mtanzania mwenzangu, wewe great thinker! utueleze maoni yako maana nijualo mimi sii jibu wala sina Utume wa kujua tutajikwamua vipi.. Isipokuwa nilichosisitiza ni kwamba tusikate tamaa na kila msafiri abebe mzigo wake, turudi nyuma tulikwamua gari letu ili tuendelee na safari., nguvu kubwa iwekwe ktk kuliondoa gari letu hapo tulipokwama..

Sasa tukianza kubishana ndio yale yale wanayodai viongozi wetu kwamba sisi wananchi ni wabishi, tuna upishi wa Punda hatuendi bila vikboko na hakika wao hawawezi kutulazimisha kunywa hata maji kwa faida yetu wenyewe. Wengine wanadai sisi ni sawa na kondoo ambao hufuata mkumbo tu lazima tupelekeshwe na mbwa ktk lishe na kurudi ktk makazi yetu tukisubiri kukamuliwa maziwa..Una hoja mkuu wangu andika huna sababu kabisa ya kunukuu niliyoandika wakati unaonyesha wazi hukuelewa kitu. Umetoka mtupu na pengine hili ndio tatizo jingine kuwa tumesoma lakini hatukuelemika. Mkuu wangu tuijadili mada na sio Mkandara mimi nimewakilisha tu hoja inayonisumbua akili.
 
Well watu nyerereism lazima muogope kwamba tunamlenga kwasababu ni ukweli; ili apate nini nimesema ili AWATAWALE kirahisi amefanikiwa ndio maana ame-over stay 24 yrs bankrupty country and people ...

Yes sababu kubwa ni ya ndani; na ni uongozi mbovu; kwani uongozi wa ndani unatakiwa ufanye analysis za external effects na kufanya uamuzi ambao ni kwa faida ya wananchi wake..

Umaskini ni tatizo la uongozi mbovu 1961-1985; 1985-1995 to date

Nadhani unatambua haujajibu swali langu kuhusu Nyerere. Utawala wa kutojilimbikizia au kutumia ikulu kifisadi unakupa raha gani kama Rais, kuwatawala wengine?
 
Binafsi, i would say kwamba asilimia 40 ya matatizo ya umaskini yanatokana na sababu ambazo ni za ndani ya nchi, kama vile uongozi mbovu n.k, ambazo zipo ndani ya uwezo wetu, na asilimia 60 ya kwanini Tanzania Masikini ni kutokana na sababu zilizo nje ya nchi (muundo wa kimataifa), ambazo zipo nje ya uwezo wetu. Pamoja na hayo, uongozi bora unaweza punguza matatizo haya ya nje ingawa sio kwa kiasi kikubwa sana kwani wakubwa wa nje nia yao ni kuhakikisha Afrika inabakia a rural back yard for Europe and North America kwa sababu zile zile za ukoloni - cheap labour; market for their goods, especially cheap, rejected goods, plus obsolete technologies; areas to extract natural resources at low costs; areas to sell their financial instrunments - doing business with our government kwa kutoa mikopo. Duniani kote, hakuna biashara tamu na ya uhakika kama ile na serikali, ndio maana hata Tanzania tunakanyagana kupata tender hata ya kuosha vikombe vya chai mawizarani.

WorldBank ni benki kama NBC au Exim, na wanahisa wa WorldBank ni the big powers wa G8; sasa ili haya yote yaende sawa, lazima nchi zetu zibakie katika hali iliyopo sasa, lakini iwapo tutafanikiwa kupanda ngazi ya maendeleo, basi watahakikisha wanatafuta maeneo mengine ya kuwapa faida hizi hizi, kwani yakiisha, ubepari upo hatarini kufa; viongozi wetu wana wakati mgumu kwani wakikataa madudu haya in a radical way, assassinations zitawakumba; Ndio maana viongozi wengi wanaamua kuwa liwalo liwe, bora waibe tu; Nchi zenye mafanikio ni zile zisizo na rasilimali nyingi, hivyo wakubwa wa nje hawajali sana kuendelea kwa nchi hizi, kwani in the end, watageuka kuwa masoko ya bidhaa zao;

Kwa wale wanaoelewa madudu haya katika mfumo wa kimataifa wa kibepari, watamwona Nyerere alikuwa ni shujaa sana kujaribu to de-link us from this mess. Kwa wale wasioelewa na wanao ona ubepari na soko huria usio na mchujo ndio mambo yote, watamwona Nyerere alikuwa mwendawazimu sana. Lakini na wao watakuwa zaidi ya wendawazimu wasipokuwa na majibu ya msingi kwanini mwanakijiji huko mbinga, maswa n.k, hali yake ipo vile vile chini ya Ujamaa (miaka 18) na Chini ya Soko Huru (miaka 27).
 
Mzee Mkandara mada tamu hii;

Nadhani kabla ya kwenda mbali sana ni lazima kwanza tukubaliane kwanza tunapozungumzia "umaskini" tunazungumzia nini hasa. Kwani bila kukubaliana tunachozungumzia tunaweza kujikuta tunaenda mbali sana au tunajaribu kujibu kitu kisicho sawa hasa. Tunaposema "umaskini" tunazungumzia "poverty" na wakati mwingine tunazungumzia "ufukara".

Umaskini wa Kipato
Kikwete na serikali yake mara nyingi wanapozungumzia Umaskini wa Watanzania wanazungumzia kile ambacho wanakiita "umaskini wa kipato". Hiki kinachoitwa "umaskini wa kipato" bila ya shaka siyo invention ya kina Kikwete bali ni wazo (theory) ambalo linaonekana kukubalika pia katika kada mbalimbali nyingine. Mwongozo wa Zanzibar wa Mpango wa Kupunguza Umaskini wa 2002 unafafanua kwa lugha nyepesi hiki kinachoitwa "umaskini wa kipato" ni nini. Unasema "Umaskini wa kipato ni ule ambapo kaya inapata chini ya dola moja ya kimarekeni kwa siku . Hii ina maana watu hawatokuwa na chakula cha kutosha au dawa na watakuwa na nguo na nyumba za hali za chini. Umaskini wa kipato unatokana na watu kukosa njia za kupata pesa au rasilimali
nyengine. Kama watu hawana rasilimali yoyote kama ardhi ya kutosha na chakula, basi umaskini wa kipato unaweza kudumaza ukuaji na kusababisha kifo cha mapema."

Kimsingi wanaoamini katika "umaskini wa kipato" wanaaminisha kuwa mtu akipata fedha ya kutosha basi ataweza kumudu kununua vitu mbalimbali vya kuboresha maisha yake; ataweza kujielemisha, kula vizuri na hata kulala vizuri. Hivyo, msisitizo wa njia za hawa ni kuwapatia watu kipato na kama mtu mmoja mmoja ni kutafuta fedha zaidi. Hatari ya kukubali "umaskini wa kipato" kama ndio umaskini unaotukabili iko wazi - watu watafanya jitihada kubwa sana kuongeza kipato chao hata kama a. hawazalishi ili kukipata (ufisadi) au kukandamiza wengine (dhulma) ili wao wapate zaidi. Kila mtu mwenye fikra hizi anajitahidi kuhakikisha kuwa kipato chake kinakua na hivyo kuondoa "umaskini wake".

Mpango huo huo wa Zanzibar unaelezea umaskini usio wa Kipato kuwa "ni pale ambapo watu wana pesa kidogo lakini maisha yao hayaridhishi. Wanakosa huduma nafuu za kijamii (kwenda skuli, huduma ya afya, dawa, maji, usafi wa maeneo, usafiri mzuri) na pengine wanaishi kwa wasiwasi majumbani mwao kwa sababu hawana imani na utawala au kwa sababu wanatokana na kundi lisilojiweza (maskini, walemavu, vikongwe)."

Sasa tafrisi zote mbili ni rahisi kuona wapi zinakosea kwa kiasi kikubwa - kwa maoni yangu. Tafrisi zote zinaangalia "kipato" kama msingi wa kuuchunguza umaskini. Hatari ya hili ni kuwa msisitizo mkubwa unakuwa kwenye kipato binafsi (personal income). HIvyo, kila mmoja anajitahidi kuondoa umaskini wake na hili tunawez akuona hatari yake. Mtu mwenye kipato kikubwa anaweza kujenga anakotaka, akaweka jenereta, kisima kikubwa cha maji (na tanki la SIMS), pamoja na kijibarabara cha kufika alipo. Huyo kutokana na kipato chake hawezi kuonekana maskini kwani licha ya nyumba atakuwa ana kazi nzuri, gari, na anaweza kumudu huduma mbalimbali apendavyo. Huyo kutokana na kipato chake atakuwa ametoka kwenye umaskini wa kipato! Hata hivyo anaweza kujikuta kwenye mazingira ya kimaskini! Yaani, kuondoka kwake katika umaskini hakujaondoa mazingira ya kimaskini ya jamii inayomzunguka!

Binafsi - sitaenda sana leo - naamini ni makosa kisayansi kuangalia kipato kama msingi wa kuchunguza umaskini kwani matokeo yake njia zinazopendekezwa kuondokana na umaskini huo zinazunguka kwenye kipato. Ndio maana utaona kuwa fisadi akiiba na baada ya kuiba akatengeneza ajira kwa watu 100 hivi haonekani kama ni mbaya kwa sababu - amewapatia watu kipato! Naamini ili kuweza kutafuta tafsiri nzuri ya umaskini ni lazima tuangalie mambo yafuatayo hivi:

a. Kukosa Nafasi (opportunity)
b. Kukosa Haki (right and justice)
c. Kukosa Usawa (equality of dignity as well as that of opportunity)
d. Kukosa Kutumia (USE)

Ninaamini kuwa umaskini wa kipato - tukiubali kuwa upo - ni dalili tu ya kukosekana kwa vitu hivyo vinne ambavyo ninaamini ndio chanzo cha umaskini hasa na bila kuangalia vitu hivyo na kuvirekebisha haijalishi kama watu watakuwa na kipato (kiwe kidogo au kikubwa) bado wataikuwa aktika umaskini. Na hili linahusu (apply) kwa mtu mmoja mmoja as well as the society at large.

Hivyo basi - naomba tukubaliane kwanza maana kuwa "umaskini ni hali ya mtu au jamii ya watu kukosa nafasi, haki, usawa na uwezo wa kutumia walichonacho kubadilisha maisha yao na kuyafanya yawe bora. Matokeo yake ya ukosefu huu ni ufukara wa kipato, hali duni ya elimu, afya, na mazingira". Mnakubali?

Tukikubaliana kuwa ndicho tunachozungumzia tunaposema "umaskini" - with some variations of course - basi tunaweza kujibu sasa a more specific question - kwanini Tanzania ni maskini?
 
Mkuu Mkandara,
Nakubaliana na wewe kimsingi kwenye maeneo mengi. Mimi naomba tu niuchokoze tu huu mjadala kidogo. Mtazamo kuhusu umaskini wetu umegawanyika katika maeneo mawili:Mtazamo wa ndani na Mtazamo wa Nje. Kwa upande moja, mtazamo wa ndani una jenga hoja kwamba umaskini wetu ni matokeo ya vitu kama uongozi mbovu (especially lack of political will), sera za ovyo, ufisadi na attitude ya watanzania kuhusu ‘kazi' (attitude towards work). Wajenga hoja hii wanadai kwamba haya ni matatizo ambayo yapo ndani ya uwezo wetu. Kwa upande mwingine, mtazamo wa nje unajenga hoja kwamba umaskini wetu ni matokeo ya ukoloni mamboleo ambao umetufunga nchi maskini kwenye mfumo wa kibepari wa kimataifa usiotendea haki mataifa madogo kama Tanzania. Wajenga hoja hii wanadai kwamba haya ni matatizo yaliyo nje ya uwezo wetu.

Nadhani mjadala ungekuwa na afya zaidi iwapo tungejaribu kutenganisha mitazamo hii kabla ya kuichanganya pamoja ili kubaini majibu sahihi.
Mkuu wangu nashukuru sana kuungana nami ktk kuumiza kichwa ktk swala hili. Nadhani tumepata majibu mengi sana kuhusiana na sababu zilizotufanya tufike hapa tulipo.

Lakini bado nazongwa na hoja moja kubwa zaidi ya kwamba tumejifunza na pengine tutajifunza kutokana na makosa yaliyotangulia iwe toka utawala wa Nyerere, Mwinyi, Mkapa au JK hawa wote kwa ujumla wao iwe ni wao ama pamoja nasi tumefika ktk korongo hili na tumeshindwa kutoka nje..Je, tufanye nini ili tuondoke hapa tulipokwama?.. Hatuwezi kumrudisha Nyerere, Mwinyi wala Mkapa kuanza kuwapiga singe za tosi kwamba wao ndio sababu bali tunachotakiwa sasa hivi ni kufikiria jinsi gani tutatoka hapa tulipo na kwa nini bado sisi maskini japokuwa tumekwisha orodhesha makosa mengi sana yaliyotangulia hadi tukafika hapa.

Kama sababu ni mtazamo wa ndani ndio unatufanya tusiondoke hapa ndipo nami nimeuliza UZALENDO wetu uko wapi?.. Kwa nini tunashindwa kujitoa ktk hali hii ili hali tunafahamu kabisa kwamba tumekwama na hatua jinsi isipokuwa kufuata hatua kadhaa kujikwamua. Kama ni uongozi mbaya, je tunataka uongozi upi na kutoka hapa tulipokwama?.

Nawasoma wabunge na viongozi wengi wakijadili mikakati ya kuondoa Umaskini, wakilenga kundi la watu maskini kwa misaada ya Millenium (IMF & WB) lakini kweli tunaweza ondoka ktk umaskini kwa kulenga kundi la watu ambao kwa maelezo yao ni asilimia 30. Na tunawawezesha vipi hao maskini watoke ktk umaskini wasirudi tena ktk bonde lile lile.. Je, ni kweli kuna baadhi ya watu tu ndio waliokwama wakati tunajulikana kama nchi maskini tena ktk kumi la mwisho duniani na huenda nchi za nje na kutangaza kuwa nchi yetu ni maskini watupe misaada?.

Hivi kweli sisi wananchi na viongozi wetu tunatambua kwamba sisi ni maskini au tunafanya mzaha na Utaifa wetu!... Na kama ni nguvu za nje ijnakuwaje bado tunaendelea kuzitumia wakati tunajua fika kwamba haziwezi kutusaidia?.. Mimi nimefanya uchunguzi wangu binafsi na kugundua kwamba ktk nchi ambazo zimeshinikizwa kubadilisha uongozi na western world - Regime change - kama Iraq, Libya, Afghanstan, Liberia, Somalia kote nchi hizo zimeshindwa kabisa ku recover kiuchumi wala kuweka uzalendo mbele. wanauana hadi kesho lakini nchi ambazo wananchi wake wenyewe wamevumbua matatizo yao hata iwe kubadilisha utawala (China, India, Kenya, Malawi, Msumbiji, Zambia, Ethiopia, Rwanda, Kuvunjika kwa Yugoslavia, Russia na kadhalika) hawa wamefanikiwa na wanaendesha chumi zao vizuri zaidi. Kwa hiyo suluhisho lipo ndani ni sisi watanzania tunaweza kujua tumekwama wapi na sisi wenyewe tunaweza kutanzua matatizo yetu..
 
Mkandara, kwanza nisamehe kwa kuwa nilipofunguwa nyuzi yako nikaanza kucheka, nimecheka kwa kuwa ni ndefu sana, sikupitia kwa kina yote nime "peruse" tu, lakini nna uhakika nimekuelewa.

Kwanza napenda ufahamu kuwa viongozi wanatokana na wananchi wanaowatumikia. Ikiwa wananchi wajinga, wazembe, wavivu, waongo, wazandik, wachawi, mafataani, wapenda vya bure, omba omba, roho mbaya, husda, chuki, hawana uaminifu, wazikaji, matapeli, hawapendi wenzao wafanikiwe, wala rushwa na watowa rushwa, wazinzi, waficha maovu, wanaogopana, wanalindana uovu, na kila sifa mbaya uijuwayo.

Sasa fikiri. Hiyo ndio jamii ya Watanzania walivyo na hiyo ndivyo uongozi wa mwanzo ulivyoiacha ikawa hivyo kwa kuweka misingi mibovu na kutokujuwa walifanyalo na kuifanya nchi ni "lab" ya kufanyia majaribio. Hivyo ndivyo 90% ya Watanzania walivyo. Kuwabadilisha kwa haraka haraka si rahisi. Kubomoa ni rahisi kuliko kujenga. Nyumba inayojengwa miaka mitano mpaka 10 inabomolewa kwa dakika moja tu. Sisi tumebomolewa kwa miaka 24 mfululizo, chukuwa hiyo halafu kila mwaka mmoja tuliobomolewa uupe miaka mitano tu ya kutengeneza, itatuchukuwa kwa uchache miaka 120 toka tulipoanza kutengeneza, imepita miaka 26 toka matengenezo yaanze bado tuna miaka 94 kwa uchache.

Usitegemee neema zote mpaka baada ya miaka hiyo kuanzia leo. Tunajitahidi na dalili zinaonekana na "improvements" zipo. Toka tulikuwa tunatowa wahitimu wachache wa vyuo vikuu sasa wamezidi maradufu, toka tulikuwa tukitaka hata kwenda Mwanza tupitie Kenya, sasa hakuna tena hilo. Toka ilikuwa hatuwezi kumiliki majumba, sasa tunaweza kumiliki majumba na maroshan. Tutafika, lakini hesabu zake ndio hizo.

Siku ntakayoona Tanzania kuna kiwanda cha kutengeza sindano za cherehani ndio siku ntajuwa sasa tunaanza kuendelea, kabla ya hapo ni bado kabisa.
 
Mzee Mwanakijiji, nadhani umaskini wetu hauna tafsiri kubwa zaidi ya maisha tunayoishi sisi. Pato la Tanznaia nzima iwe exports ni sawa na pato la wilaya ya Marekani au nchi za Ulaya, hata hiyo Ugiriki illofilisika pato lake linaweza chukua nchi kama 20 za kiafrika hali tunataka tuishi kama wao. Na hilo la umaskini wa kipato ni changa la macho kwa sababu kinachotazamwa ni sales against total number of population. yaani Kama Tanzania tunauza nje Billioni 50 wanagawanya kwa wananchi wake bila kujali kwamba asilimia 50 ya mauzo hayo hazikanyagi Tanzania.. Sasa iweje tunaweza kuzungumzia umaskini wa pili ikiwa tayari wa kwanza tumebigwa bao?..

Na sidhani kaa umaskini unaweza kuutafsiri kwa hivyo, maana Nchi kama Brunei, Guinea Bissau, na kadhalika hazipo ktk umaskini kama wetu wakati hayo yote uliandika hapo juu wananchi wake hawapati afadhali yetu sisi mara 10. Maskini ni maskini tu awe fukara au kilema cha hali na mali ni mtu unayetakiwa kusaidiwa hujiwezi...na hutaweza kuondokana na umaskini huo unless unatafuta solution ya hali ulokuwa nayo badala ya kuridhika na umaskini huo kama ombaomba wa misikitini.

Mimi Mhafidhina na siamini kabisa kwamba binadamu tumeumbwa na tabaka za utajiri na umaskini bali sisi wenyewe ndio hufikia hatua hizo kutokana na maamuzi yetu. Tunaweza kabisa kuondokana na umaskini maana Mungu kaiumba dunia hii kama - LAND OF OPPORTUNITY.. Leo sisi tuna ardhi bora ktk ukulima, uvuvi na ufugaji, gas na madini ya kila aina yamejazana lakini tunalaani vitu hivyo na kuomba tujaliwe mafuta!. Fikiria kama Saudia au nchi za kiarabu wasingepewa hayo mafuta wangekuwaje wao?
 
Mkandara, kwanza nisamehe kwa kuwa nilipfunguwa nyuzi yako nikaanza kucheka, nimechaka kwa kuwa ni ndefu sana, sikipitia kwa kina yote nime "peruse" tu, lakini nn uhakika nimekuelewa.

Kwanza napenda ufahamu kuwa viongozi wanatokana na wananchi wanawatumikia. Ikiwa wananchi wajinga, wazembe, wavivu, waongo, wazandik, wachawi, mafataani, wapenda vya bure, omba omba, roho mbaya, husda, chuki, hawana uaminifu, wazikaji, matapeli, hawapendi wenzao wafanikiwe, wala rushwa na watowa rushwa, wazinzi, waficha maovu, wanaogopana, wanalindana uovu, na kila sifa mbaya uijuwayo.

Sasa fikiri. Hiyo ndio jamii ya Watanzania walivyo na hiyo ndivyo uongozi wa mwanzo ulivyoiacha ikawa hivyo kwa kuweka misingi mibovu na kutokujuwa walifanyalo na kuifanya nchi ni "lab" ya kufanyia majaribio. Hivyo ndivyo 90% ya Watanzania walivyo. Kuwabadilisha kwa haraka haraka si rahisi. Kubomoa ni rahisi kuliko kujenga. Nyumba inayojengwa miaka mitano mpaka 10 inabomolewa kwa dakika moja tu. Sisi tumebomolewa kwa miaka 24 mfululizo, chukuwa hiyo halafu kila mwaka mmoja tuliobomolewa uupe miaka mitano tu ya kutengeneza, itatuchukuwa kwa uchache miaka 120 toka tulipoanza kutengeneza, imepita miaka 26 toka matengezo yaanze bado tuna miaka 94 kwa uchache.

Usitegemee neema zote mpaka baadaa ya miaka hiyo kuanzia leo. Tunajitahidi na dalili zinaonekana na "improvements" zipo. Toka tulikuwa tunatowa wahitimu wachache wa vyuo vikuu sasa wamezidi maradufu, toka tuliwa tukitaka hata kwenda Mwanza tupite Kenya, sasa hakuna tena hilo. Toka ilikuwa hatuwezi kumiliki majumba, sasa tunaweza kumiliki majumba na maroshan. Tutafika, lakini hesabu zake ndio hizo.

Siku ntakayoona Tanzania kuna kiwanda cha kutengeza sindano za cherehani ndio siku ntajuwa sasa tunaanza kuendelea, kabla ya hapo ni bado kabisa.


Je, unaweza kutenganisha internal factors na external factos kama source za mafanikio hayo unayoyataja?

Na je, haya anayoyataja Mwanakijiji kama njia sahihi ya kutafsiri maana ya umaskini:
a. Kukosa Nafasi (opportunity)
b. Kukosa Haki (right and justice)
c. Kukosa Usawa (equality of dignity as well as that of opportunity)
d. Kukosa Kutumia (USE)

Je, una maoni gani juu ya haya in the context ya hiyo miaka 24 ambayo nadhani unamzungumzia BABA WA TAIFA na pia miaka baada ya BABA WA TAIFA kung'atuka?
 
Back
Top Bottom