Tatizo kubwa la serikali ni la kutokufanya maamuzi sahihi kwa wakati sahihi. Hali hii hupelekea tatizo la kisheria kutotatuliwa kwa muda mrefu, na hatimaye wananchi wanafikia kujiona wapo kisheria ijapokuwa kiuhalisia huwa wanavunja sheria.
Mifano ipo mingi sana, ambapo wananchi wanaendesha biashara ama kujijenga kimaisha hali serikali ikinyamazia uvunjaji na ukiukwaji wa sheria. Mathalani, tumeshuhudia ujenzi wa makazi katika maeneo hatarishi, yaliyotengwa kwa matumizi maalum, ama katika hifadhi za barabara, viongozi wa serikali na mamlaka wakiwa wapi kimya kama vile hawaoni kitu kinachoendelea.
Ujenzi ama shughuli za kibiashara, pale zinapoanza kuibuka, kunakuwa hakuna onyo ama katazo lolote linatolewa. Kibaya zaidi vibali vya huduma muhimu kama umeme, maji, elimu, simu n.k hutolewa hali ikifahamika vinakwenda kinyume kabisa na sheria.
Hili suala la Maasai kuvamia maeneo ya hifadhi ya Ngorongoro halijatokea kwa siku moja, ni jambo ambalo limepuuziwa na kuacha likikuwa mpaka limefikia kiwango hiki cha malumbano. Maasai waliachwa kwa makusudi wavunje sheria ili kuvitia zaidi biashara ya utalii.
Kuonekana kwao kama kabila duni lenye kuweza kuishi maisha "primitive" na wanyama hayawani wa mwituni ilionekana ni kichocheo cha kuwaacha wafanye shughuli zao za ufugaji katika hifadhi hii. Sasa ongezeko lao na ukubwa wa shughuli zao leo ndiyo vinaonekana kuwa hatarishi.
Ni lazima muafaka wenye kuzingatia masuala ya kiutu ufanyike. Ndiyo! Ukubwa wa tatizo sambamba na athari zake zimethibitika, lakini ukweli ni kwamba uvamizi huu haukutokea kwa siku moja. Ni lazima serikali iwaelimishe kwanza kabla ya kuanza matumizi ya nguvu ya kuwatoa hapo na kuwaamishia maeneo mengine ambayo hayajaandaliwa vyema kwa ajili ya maisha yao ya kifugaji.