Pamoja na uwepo wa mada inayohusu kufungwa kwa kampuni ya Dangote hapa nchini iliyoletwa na Mkuu
Return Of Undertaker, naomba Moderators muuache Uzi huu kwa maslahi ya mjadala na uelewa.
Kichwa pamoja na maudhui ya uzi wa mtajwa hapo juu ni kuleta habari na kutaka kuaminisha umma kuwa Dangote anataka kufunga kampuni yake kule Mtwara na kuondoa uwekezaji wake hapa Tanzania. Katika kuonesha ukweli huo kumeambatishwa habari ya gazeti la the Citizen la leo.
Kwa msomaji makini ataona na kujua kuwa Dangote ndiye anayepinga kufungwa kwa kampuni yake hapa nchini. Hivyobasi, hana nia ya kuifunga na kuondoka. Yeye ndiye aliyepinga na kufanikiwa kuzuia shauri la kufungwa kwa kampuni yake.
Iko hivi kwenye habari hiyo: Kampuni ya Dangote, kama kampuni nyinginezo, iliingia mkataba wa kuletewa fuel na kampuni ya NSK. Katika kufanikisha hilo, kampuni ya NSK ikachukua mkopo kama mtaji kutoka benki ya Standard Chartered wa bilioni 11.1.
Baada ya kushindikana kulipwa kwa mkopo huo, Standard Chartered ikawashtaki NSK na Dangote. Kufuatia shauri hilo, na katika hali ya kujitetea, NSK akapeleka shauri la kufungwa (winding up) kwa kampuni ya Dangote kwa kushindwa kulipa deni lake kwa kampuni hiyo.
Naye Dangote akawasilisha Mahakamani hapohapo Ombi dogo la kusitisha kwa muda shauri la kufungwa kwa kampuni yake. Ombi lake dogo Dangote ndilo lililotolewa uamuzi kwa kusitisha shauri la kufungwa kwa kampuni yake. Ndiyo kusema, Dangote amefanikiwa kwenye maombi yake.
Kwa kifupi, Dangote ndiye anayepinga kufungwa kwa kampuni yake pamoja na deni linalodaiwa kuwepo dhidi ya kampuni ya NSK. Kwenye mashauri hayo yaliyoripotiwa na the Citizen hakuna mahali Dangote na kampuni yake wameonyesha nia ya kufungwa kwa kampuni hiyo na kuondoka nchini.
Ni vyema kusoma habari kwa makini kabla ya kuandika uelewa ambao wakati mwingine waweza kubeba picha ya kupotosha umma. Dangote ndiye aliyepinga kwa nguvu zake zote kufungwa kwa kampuni yake kwenye mashauri matatu yaliyopo Mahakama Kuu yakihusika kampuni yake, kampuni ya NSK na benki ya Standard Chartered.