Mwendazake kwa hakika amekwisha enda zake, kwa kuwa hayupo tena nasi katika hali ya kimwili ambapo aliweza kuiongoza nchi hii. Ametuacha, ametutoka, ametangulia mbele za haki ama ameenda zake, hilo ni tukio la uhakika ambalo kwalo litamtokea kila mwanadamu aliyezaliwa na mwanamke hapa duniani.
Kuonja mauti ni jambo la hakika kwa mwanadamu awaye yeyote yule, wala sioni shida ama sababu yenye mantiki kwa viongozi wa kidini kuona ukakasi juu ya yule aliyekufa kuitwa mwendazake, kwani kwa sasa hayupo tena nasi katika ulimwengu huu wa kimwili. Neno hili limebamba mno kwa kuwa mwendazake alikufa akiwa kiongozi wa nchi yetu, na katika uongozi wake watu wengi waliathirika kwa aina ya utawala wake, kwa maana ya muelekeo athari hasi ama chanya, ingawaje wale wa upande wa athari hasi ndiyo hupenda hasa kutumia nomino hii ya utambulisho wake kwa sasa.