Sipingi kuwa sisi binadamu tunahitajiana kwa ajili ya masuala ya kijamii. Ila jambo muhimu hapa, Je ni suala lipi la kijamii unahitaji kushiriki kulingana na uwezo wako kiuchumi.?
Haiingii akilini mtu analipwa Tshs. 450,000 kama mshahara wake kwa mwezi, halafu umtake mtu huyo kuchangia zaidi ya michango mitatu ya harusi kila mwezi yenye kuanzia Tshs. 50,000/= - 200,000/=.
Je, tunafahamu vipaumbele vyetu kimaisha kulingana na uwezo wetu kiuchumi.?
Maisha haya ya kiafrika tuliyonayo, ambayo kwa kiasi kikubwa vipato vyetu ni duni, inahitaji sana kuwa na vipaumbele katika matumizi yako ya fedha unazofanikiwa kuzipata.
Kwa maoni yangu, miongoni mwa vipaumbele muhimu ni pamoja na chakula, matibabu, mavazi na malazi.
Sasa unakuta mtu hata tu kuwa na kipato cha kumudu chakula kwa mwezi hana kisha umtake achangie michango ya harusi yenye thamani kuanzia laki moja kwa mwezi, Je, huu ni uungwana.? Achilia mbali kuhusu uwezekano wa kumudu mahitaji mengine muhimu kama mavazi, matibabu na malazi. Hapo nimeongelea chakula tu.
Najua wapo watu watasema, si uwe unaacha kuchangia kwani unalazimishwa.? Hivi utajisikiaje mtu unayefanya naye kazi ofisi moja, mwingine umesoma naye, mwingine umekutana naye katika matukio muhimu na kisha kufahamiana naye, utajisikiaje akikupa kadi ya mchango na kisha kumchunia tu bila kumchangia.?
Nini Kifanyike.?
Utamaduni wa kufunga ndoa na kufanya sherehe si utamaduni mbaya lakini uendane na kipato cha muhusika.
Kama jamii unayoishi ipo katika nafasi nzuri kiuchumi, ni jambo zuri kuishirikisha jamii hiyo ili wakuunge mkono kwa namna moja au nyingine maana jamii ya watu wenye kipato kizuri cha fedha inamanisha imeshatoka kwenye kiwango cha kumudu mahitaji muhimu na kuelekea kwenye matumizi ya ziada kama vile anasa n.k
Kama jamii unayoishi ni ile yenye kumudu matumizi ya mahitaji ya msingi kama vile chakula, malazi, matibabu na mavazi basi usiishurutishe jamii hiyo kukuchangia ilihali unafahamu kabisa hata wakichanga watachanga huku wakiumia moyoni. Katika hili tusipeane moyo kuwa kutoa ni moyo na usambe si utajiri.Moyo upi huo wa kutoa laki moja kufanikisha sherehe ya harusi ya mtu huku nyumbani kwako hakuna chakula.?
Ni vema tuwe na utamaduni wa kufanya maandalizi mapema kupitia rasilimali zako mwenyewe kama unaona ni lazima ufanye sherehe yako ya ndoa. Ili badala ya kuwachangisha watu kisha wewe ndiye utoe fedha zako za akiba na kuwakaribisha watu kushitriki sherehe hiyo bila kuwalazimisha kukuchangia kwanza.
Ni vema tukazingitia kuwa, kufunga ndoa si lazima ufanye sherehe. Bado utahesabika umeoa/kuolewa hata kama ulimefunga ndoa bila kufanya sherehe.
Mbaya zaidi, unatoa mchango wa harusi laki moja, mbili, au hata tano ila linapokuja suala la kumchangia mgonjwa anayehitaji matibabu unaona anastahili Sh 2000/= au 5000/=
Je, huu ni uungwana.???