Tukiangalia ukweli halisi juu ya umiliki wa mahospital na huduma za afya nchi, sio tatizo kwa mazingira ya sasa Serikali kuendelea kutoa ruzuku katika mahospital ya taasisi za kidini. Labda ingekuwa vizuri uigo huo ukapanuliwa na kuhusisha taasisi zote zisizo za kiserikali zinazomiliki mahospital na vituo vikubwa vya afya nchi. Yawezekana kutokana na uchache wangu wa taarifa nikawa sina ufahamu sana namna serikali inavyosaidia taasisi nyingine zisizo za kiserikali zilizowekeza katika huduma ya afya. Nachotaka kusema hapa ni kwamba badala ya kuendelea na utaratibu wa sasa wa kusainiwa MOU katika ya serikali na taasisi hizo ni bora suala hili likatamkwa katika sheria. Kutamkwa kwa suala hili katika sheria kutaona hisia za kidini zinazojitokeza. Maana, kama sheria ikitamka rasmi haki ya mahospitali ya taasisisi zisizo sa kiserikali yakiwemo mashirika ya kidini kupata ruzuku na ikaweka vigezo maalumu, hapatakuwa na mwanya wowowte wa kulitizama suala hili katika jicho la kidinidini. Litatizamwa kama suala la kawaida la huduma za afya bila kujali nani anatoa huduma hizo ili mradi zinawanufaisha watanzania.
Nikirudi katika huduma za kiafya, mimi naona maafikiano yaliyomo katika MOU hayakidhi matakwa ya mazingira ya sasa kwa sababu kadhaa. Kwanza, maafikiano ni ya kiujumla sana. Hayatoi ufafanuzi huduma za elimu katika hatua gani na wala hayaweki wajibu katika taasisi za kidini. Ni vigumu kujua kama ruzuku inapaswa kutolewa kwa vyuo vikuu, sekondari au shule za misingi? Je itahusu shule zinazotoa huduma kwa watu wote au hata shule za seminari zinazotoa huduma mahususi kwa waumini wa dhehebu husika? Je Serikali kwa kutoa ruzuku itakuwa na haki kwa mujibu wa walipa kodi kudhibiti ada zinazotolewa na mashule yanayomilikiwa na taasisi za kidini? Sababu nyingine ni kwamba kutokana na kuwepo mashule mengi ya sekondari ya kata na mengine yanayomilikiwa na taasisi zingine za kidini zisizo za kikistristo, suala la serikali kutoa ruzuku katika mashule na vyo vya elimu vya kidini halina maana ile ile ambayo pengine lingekuwa nayo katika miaka ya 80. Ni bora hizo pesa za ruzuku zikatumika kuboresha shule za kata ambazo huko mbeleni zinaweza kuwa mkombozi mkubwa kwa walala hoi na watoto wa wakulima.