Haya masuala ya mipaka ardhi ukiyachunguza kwa undani ni tamaa, upumbavu, ujinga, ubinafsi, wivu, uwelewa mdogo na roho mbaya tu kati ya mtu na mtu na wala hayahusiani na kazi, kabila, dini wala elimu ya mtu.
Kuna rafiki yangu mmoja wapo familia mbili jirani (mojawapo ni ya rafiki yangu) wamejenga wamefuatana lakini barabara ya kufika kwao inapita ubavuni kwenye kiwanja cha jirani yao ambaye ni kijana wa makamo tu ambaye ameenda shule vizuri na mkristo safi anatokea kanda ya Ziwa na mkewe anatokea kanda ya Kaskazini. Japo hizo familia mbili ndio zilizotangulia kujenga na kuhamia jamaa alipofika akajenga halafu akaweka ukuta kwenye usawa kabisa wa barabara. Jamaa ndani ya ukuta wake akaweka vyumba vya kupanga halafu akatoboa milango kwenye ukuta kwa hiyo mpangaji akifungua tu mlango kutoka nje yupo barabarani kabisa. Kama haitoshi akaongeza vijibaraza vya ngazi barabarani kiasi wakikaa nje gari ikipita inawabidi wainuke ili gari ipite. Barabara ilikuwa kubwa ya kupishana gari mbili sasa inapitisha gari moja tu hamna kupishana. Na ujinga wa kutamani kiwanjani chake kitanuke wakati ardhi haitanuki kajenga geti lake la kuingilia mwishoni kabisa mwa kiwanja matokeo anakuja kujenga kile kipaa kikawa kichekesho kimeingia kabisa barabarani ili kisigongwe na magari ikabidi akiinue juu kabisa kama mti wa mnazi.
Siku moja rafiki yangu alijaribu kumuuliza jirani yake kama anaona anachokifanya ni sahihi maana alikuwa ameweka tofali zake barabarani magari yakawa yanapita kwa shida. Jamaa akaja juu sana rafiki yangu akaachana naye sio kwa kumuogopa bali jama yangu ameshika sana dini na hapendi kabisa ugomvi. Na siku zote msemo wake ni kuwa ukitaka ushindi wa muda mfupi na laana ya muda mrefu basi dhulumu mtu ardhi hata hatua moja tu.
Kiukweli watu wengi wanaponunua hivi viwanja ndio uwezo wao kwa wakati huo. Lakini wakija kupata pesa zaidi baadaye badala ya kutumia akili wakanunue maeneo makubwa zaidi nje ya mji wanatamani eneo lile walipo liongezeke wakati ardhi haitanuki ndipo hapo sasa ugomvi wa mipaka na majirani unapoanzia.