Pole mkuu hayo ni mapito tu yatapita na utasahau.
Ushauri wangu wa bure kwako na kwa vijana wengine hapa jamvini:-
1. Hata siku moja usiruhusu wafanyakazi wenzako wakajua mambo yako binafsi na hata kufika nyumbani kwako. Wafike nyumbani kwako pale inapobidi tu labda kama una unaumwa/msiba hapo hauna ujanja. Lakini sio birthday, kipaimara, graduation ya mtoto, n.k. unawaalika wafanyakazi wenzako litakukuta jambo. Na mbaya zaidi watakaokuharibia ni wale wafanyakazi wenzio mliopo kitengo kimoja. Nalisema hili nikiwa na ushahidi wa watu wengi niliowaona wakipitia magumu makazini baada tu ya kuwakaribisha wafanyakazi wenzao nyumbani. Ukitaka kuwaalika wafanyakazi wenzako kama una uwezo fanyia hizo sherehe ukumbini basi.
2. Kwa umri wa miaka 31 na ukiwa tayari umeshamleta mtoto duniani ambaye haelewi chochote zaidi ya kukutegemea wewe umpatie mahitaji yake inabidi uwe mpambanaji kweli kweli. Sasa maelezo yako yananishangaza unaonekana bado haujaikubali hiyo hali ya kufukuzwa kazi na haujui mahitaji yako kwa sasa. Wewe sasa hivi unachotakiwa kwanza ni kukubali kuwa ile kazi haipo tena. Na mahitaji yako sasa hivi kwanza ni kubadili kabisa mtindo wa maisha uliokuwa unaishi. Pili unachotakiwa kwa sasa ni kutafuta kwanza pesa ya kula tu wewe na mkeo na mtoto wako hao wengine wote waeleze ukweli na watake wasitake itabidi wasubiri tu mpaka mambo yako yatulie. Kwa kifupi tu upo vitani kwenye uwanja wa vita bila kutangaziwa vita. Kama ulikuwa unafanya kazi kwa kutumia labda kalamu au laptop mzee sasa ni tofauti hela ya kula mtaani inatafutwa kwa nguvu, juhudi na maarifa na kujitoa ufahamu kwa kiasi fulani. Kwa mfano unaweza kuwa unatembelea "site" za ujenzi unaomba vile vibarua vidogo vidogo kwanza ukizoea ndio utaanza kufanya zile kazi ngumu. Huo ni mfano mmoja tu fursa nyingine jiongeze mwenyewe. Kuna jamaa yangu mmoja alikuwa na kazi nzuri tu yakamkuta kama yaliyokukuta. Hauwezi amini jamaa alitupa aibu zote akaweka usomi wake pembeni akakamata TOYO tena ya mkataba. Kwa hasira bila kujali ndugu, jamaaa na majirani wanasema nini alipiga kazi kama kichaa alikuwa analala masaa machache sana. Ndani ya miaka miwili na nusu tu sasa hivi anamiliki TOYO mbili na bajaj moja anakula hesabu ila sasa hivi yeye ameacha kuendesha TOYO japo anasema kwa mtu mwenye malengo inalipa sana. Kwa sasa anafanya biashara nyingine baada ya kukusanya mtaji ila anatoa angalizo kwa wengine kuwa si kazi rahisi kwa sababu anasema amekoswa koswa sana na ajali sana lakini kikubwa familia yake haikuadhirika kwa kukosa chakula au kuomba kuomba na anamshukuru Mungu kwa kumepusha na ajali. Kwa kifupi mzee weka aibu pembeni rudi chini na usijali watu wanaokufahamu watasema nini wakikukuta unatafuta ugali wa familia yako kikubwa wewe zungumza na Mungu wako.
3. Ongea na waifu kwa kina juu ya hali manayopitia sasa. Na yeye aondoe aibu atafute shughuli ya kufanya ili asaidie kupatikana chakula mezani. Tena wakinamama shughuli zao zipo nyingi sana na mitaji inayohitajika ni midogo sana kama kutembeza matunda mitaani, kufua nguo za majirani, kuuza mboga mboga, kutembeza nguo na viatu vya mitumba mitaani, n.k.
4. Hiyo 2 na 3 ikifanyika kwa ufasaha hilo wazo la kuuza nyumba litafutika kabisa. Sasa kwa upande wa nyumba maadam imeshaezekwa na wewe una shida chakufanya hapo ziba baadhi ya madirisha hata na mabati. Jitahidi upate tu pesa kidogo weka mlango wa mbele na wanyuma hamia. Choo jenga tu huko nje cha "temporary". Na hii sio nadharia siku tukisema kuna "challenge" hapa jamvini ya kila mtu kuelezea alihamiaje hamiaje kwenye nyumba yake ya kwanza ndugu utajiona wewe una nafuu sana kwani mpaka umeshapaua. Ukiliweza hili basi utakuwa umeokoa pesa ya kodi ambayo itafanyia kazi nyingine.
5. Mwisho wewe waeleze ndugu zako kwa utulivu wa hali ya juu kuwa kwa sasa huna kazi na huku ukionyesha ujasiri wa hali ya juu kuwa unapamabana kutafuta kazi nyingine kwa hiyo wakuvumilie kidogo wala wasiwe na wasiwasi mambo yatakaa vizuri. Na mkeo awaeleze ndugu zake waujue ukweli huo. Hili litawasaidia sana msibebshwe mizigo mingine mikubwa na wanafamilia katika kipindi hiki cha mpito. Lakini wakati hayo yote yanaendelea suala la wewe na waifu kutafuta kazi liwe kipaumbele kila siku iendayo kwa Mungu na wala msichague kazi kwa sasa.
Ni mtizamo tu,