Wahenga walisema "Mtoto Ni Mtoto Kwa Mama Hakui", huwezi kulinganisha hasira na msongo wako wa mawazo ulionao na ile hali aliyokuwa nayo mama yako wakati anakulea ulipokuwa mdogo, tena bila baba yako kuwepo. Unajua alipitia mangapi kukulea wewe akiwa peke yake (Single Mother) bila baba yako? Unajua aliamka mara ngapi usiku wa manane kila mara pale wewe ulipoamka, ulipolia, au kila ulipoumwa, uliposikia njaa au kiu? yeye kukuambia wewe ni mzembe haingii hata chembe ukilinganisha na aliyoyapitia yeye wakati anakulea. Lakini pia kwanini ukereke na kauli kwamba wewe ni mzembe wakati wewe si mzembe!!?? Shida iko wapi au kweli wewe ni mzembe?! Mtu akikuita wewe ni mjinga wakati unajijua kwamba wewe si mjinga, tatizo liko wapi? Ukikereka na kauli kwamba wewe ni mzembe, huenda kuna ukweli kidogo kwamba wewe ni mzembe.
Kwa sasa wewe una hasira na msongo kwasababu mambo yako hayajakaa sawa kama ulivyotarajia, sio kosa la mama ingawa hasira zako wewe sasa unamtolea mama kwasababu ndiye aliye karibu na wewe, hata ungekuwa na mke, rafiki au ndugu aliye jirani na wewe lazima hasira zako ungemtolea huyo mke/ndugu au rafiki, na yeye mama pia ana hasira na msongo na anasikitika kwasababu anaona mwanawe mambo yake hayajakaa sawa na hilo linamsikitisha.
Maneno anayoyasema mama kwako, hiyo ni namna yake ya kuelezea hasira zake, kwa malezi aliyokulia na kwa uzoefu wake hapo yeye anajiona yuko sawa, tambua wewe ni mtoto wake (Hata uwe na miaka mingapi) bado wewe ni mtoto kwake, ana wajibu wa kukusema haijalishi ulimfanyia nini huko yuma - kumbuka mtoto ni mtoto kwa mama hakui. Usithubutu kumsema mama yako vibaya - usithubutu.
Shida iliyopo au shida mliyonayo wewe na mama ni kwamba nyote kila mmoja wenu ana hasira, msongo n,k lakini mmevibeba kichwani mwenu, hakuna anayemwambia mwenzake yanayomsibu au kilichomo akilini mwake na mipango na mikakati yako ya kuondokana na hali hiyo (Badala yake wewe umekuja hapa Jamiiforum badala ya kuongea na mama yako)
Kukimbia, kuuza nyumba au shamba au kumsema au kumwambia kwamba anakusimanga (Haya ni mawazo ya kichwani mwako) sio ufumbuzi. Mnahitaji kuboresha sana mawasiliano kati yenu wewe na mama, kila mmoja bila hasira amweleze mwenzake kinachomsibu kichwani mwake na mipango na mikakati anayopanga ya kuchomoka kimaisha. Hata kama una mipango ya kuondoka lazima kwanza uzungumze na mama kwa utulivu na unatafakari kufanya hivyo na kisha ndio uondoke.
Kama kweli una hasira sana, basi hasira zako kazitolee kwenye kazi, kwenye kilimo, biashara au ujasiriamali na sio kwa mama yako.
Nani kama mama?