Watu wasiojulikana walitoa hukumu ya Kifo kwa Tundu Antipas Lissu ili asiishi tena hapa duniani kwa sababu ya makosa aliyoyafanya - alistahili hukumu ya KIFO kwa sababu hakuna adhabu nyingine mbadala iliyo nafuu ambayo ingemfaa.
Watu wasiojulikana si tu waliona kwamba Lissu hastahili tena kuishi duniani kwa makosa aliyofanya bali pia hata Familia yake nayo isononeke daima kwa kukosa uwepo wake - Mke wa Lissu awe mjane na watoto wa Lissu waishi bila baba hapa duniani, wazazi na ndugu zake wa karibu wasimuone tena mpendwa wao, lazima afe tu.
Kisheria unaweza kuhukumiwa KIFO kama wewe ni Jambazi Sugu ama Gaidi sugu la kimataifa. Na hapo utahukumiwa kunyongwa hadi kufa ama kifungo cha maisha jela - sasa Kosa la Lissu ni kubwa zaidi ya haya mawili kwani alitakiwa kufa bila kusikilizwa kokote, bila kujitetea wala kusubiri aandike wosia ama neno moja kwa Mkewe ama watoto wake, hakutakiwa kabisa - afe kwa ghafla. Hati ya kifo chake ikapitishwa ili itekelezwe.
Yote haya watu wasiojulikana waliyatafakari kwa kina kabla ya kutoa HUKUMU YA KIFO kwa LISSU ila wakaona ni lazima binadamu huyu ayaonje mauti - tena auawe si kwa risasi moja ama mbili bali auawe hadi afe kwa idadi yoyote ile ya risasi. Kwa hiyo mtekelezaji yeye anaamua kuzimimina zaidi ya 38 ili ahakikishe huyu Mwanadamu habaki hata na chembe moja ya uhai - SMG siyo mchezo ni Bunduki ya kivita hii.
Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kawaida yeye ndiyo huidhinisha adhabu hizi kutimilika, mara nyingi huwa haingilii sana lakini kwa hili la Lissu akasema HAPANA. Kilichofanyika pale wakati wa zoezi la kuteketeza uhai wa Lissu ni siri kubwa, Je ni kipi kilimzuia Lissu asifungue mlango wake ili atoke na watesi wake wazimimine hizo risasi watakavyo?
Je ni kipi kilimpata huyo mfyatuaji wa Risasi hizo apate kitete na kulenga shabaha hata moja kati ya hizo 38 akiwa mita chache tu toka kwa mlengwa. je kuna kipi kilimzuia yeye kufika na kuchungulia ndani ya gari na kuhakikisha anammaliza kabisa Lissu?
Hapo ndugu zangu, ndipo uwezo wa mwanadamu kufikiri hufikia mwisho, na hata ukiwa mpagani basi unaanza kuamini uwepo wa Mwenyezi MUNGU muumbaji wa ulimwengu huu.
Mwenyezi Mungu aligoma kusign file la Lissu alilokuwa analetewa na Islaeli mtoa roho - akasema "NO". Lissu bado hajamaliza kazi yake niliyompa, lazima arudi aimalizie - file la Islaeli mtoa roho halikupokewa akaamriwa alirudishe duniani haraka, kwa hudhuni kubwa Islaeli akawakabidhi watesi wa Lissu hilo file la hukumu ya kifo.
Sasa tatizo linakuwa kubwa sana kwa wale watesi wa Lissu; maisha yao yanakuwa magumu mno kwa mawazo kwa mantiki kuwa uliyetaka awe kaburini yupo kitandani anauguza maumivu makali; majonzi yake yote yanakurudia, vilio vya wapendwa wake wanavyosikitika vinakurudia wewe, hilo linakupa mawazo makuwa mno na msongo wa mawazo; kila ulifanyalo unasikia sauti ya Lissu ikilalama wakati ule wa shambulio - sauti yaweza kusema (si hakika) " mnaniua kwa nini? kwa nini mnaniua kwa nini jamani, nikekosa nini mimi?" Sauti hii ndiyo inawasumbua wale wasiojulikana kila usiku na kila kukicha masikoni mwao.
Sasa wa ninyi mnaojifanya hamjulikani kwa MUNGU mnajulikana fika; adhabu yenu ya kifo imekataliwa (imetenguliwa) na Muumba wa mbingu na nchi, mna kazi ngumu ya kumwomba msamaha muumba wenu maana mmemkosea kwa kitendo cha kuamua kutoa roho ya mwanakondoo wake bila idhini yake. Sasa kwa ushauri tu mnaweza kupitia vitabu vitakatifu mkaona wale wenzenu waliomkosema Mwenyezi Mungu walifanya nini ili wasamehewe, hii ni adhabu kubwa kwenu na msipoangalia inaweza kuwatafuna kizazi hadi cha tano na sita. (Pitieni Biblia adhabu aliyopewa Kaini baada ya kumuua Abel mdogo wake)
Kwa sisi wengine tujue fika kwamba hakuna mwenye mamlaka ya kutoa uhai wa mwenzake hapa duniani, kama unaona mwenzio amekukosea basi kuna Mahakama ambazo Mwenyezi Mungu anazitambua tangu enzi za kale; waweza mpeleka huko akahukumiwa wa mujibu wa sheria.
MUNGU Aligoma kupolea file la kifo akaamuru lirudishwe duniani kwani kazi aliyopewa bado hajaimaliza. ( Fikiri mara mbili ewe mwanadamu).