UTANGULIZI: UTAWALA WA MAARIFA KATIKA KARNE YA 21
Katika karne hii ya 21, nguvu siyo tu silaha, siyo tu fedha – bali maarifa. Taifa linalomiliki maarifa ya kisasa na kuyaendeleza lina nafasi kubwa ya kutawala mustakabali wa dunia. Hivi karibuni, China imeandika sura mpya ya mafanikio ya kisayansi, kwa kufufua teknolojia ya nyuklia ambayo Marekani waliitelekeza zaidi ya miaka 50 iliyopita.
Hili si jambo dogo, bali ni ishara ya namna ambavyo mataifa makubwa huwekeza katika maarifa ya muda mrefu hata kama hayaleti faida ya haraka.
Lakini ni teknolojia gani hiyo? Ikoje tofauti na ile tunayofahamu? Na sisi Watanzania tuna nafasi gani katika muktadha huu?
SEHEMU YA KWANZA: FAHAMU TOFAUTI YA NYUKLIA TULIYOZOEA NA HII MPYA
Kwa miaka mingi, dunia imekuwa ikitumia teknolojia ya nyuklia inayotegemea madini ya
Uranium-235. Mtambo wa kawaida wa nyuklia huchemsha maji kwa kutumia joto linalotokana na mgawanyiko wa atomu (
nuclear fission), kisha mvuke husukuma turbine ili kuzalisha umeme.
Hata hivyo, changamoto kubwa ya mfumo huu ni hatari ya kulipuka, uhitaji wa maji mengi ya kupoza, na kuzalisha taka za mionzi (
radioactive waste) zenye uhai wa maelfu ya miaka — ambazo hata mataifa yaliyoendelea hayajui zitatupwa wapi.
Hapo ndipo teknolojia ya
Thorium Molten Salt Reactor (TMSR) inapokuja na mapinduzi yake. Tofauti na Uranium,
Thorium-232 haiwezi kutumika kutengeneza silaha za nyuklia moja kwa moja. Ina kiwango cha juu sana cha usalama kwa sababu:
- Mtambo wa molten salt unatumia chumvi iliyoyeyushwa kama kiyeyuzi cha joto, ambayo haichelewi kulipuka hata kama mfumo utavurugika.
- Thorium inapogawanyika hutoa mionzi ya kiwango cha chini mno, na taka zake hubaki na mionzi kwa muda mfupi zaidi — miaka 300 hadi 500 badala ya maelfu.
- Haizalishi Plutonium, kiungo kikuu cha silaha za nyuklia.
SEHEMU YA PILI: MAREKANI WALIPOACHA, CHINA WAMECHUKUA HATAMU
Miaka ya 1960, maabara ya Oak Ridge National Laboratory nchini Marekani ilifanya majaribio ya awali ya
Molten Salt Reactor. Utafiti huo uliashiria uwezekano mkubwa wa teknolojia hii kuwa mbadala bora wa mitambo ya kawaida ya nyuklia.
Hata hivyo, Serikali ya Marekani haikuona umuhimu wa kuendeleza mfumo huu kwa kuwa haukuwa na faida ya kijeshi – haungeweza kutumika kutengeneza silaha.
Hapo ndipo utafiti huo ukawekwa kwenye mafaili ya vumbi.
Miaka kadhaa baadaye, China ilipekua mafaili hayo na kuanza kuwekeza mabilioni ya dola kuendeleza teknolojia hiyo. Matokeo yake? Mnamo mwaka 2024, China ilizindua kwa mafanikio mtambo wa majaribio wa TMSR katika jangwa la Gansu.
Huu ni mtambo wa kwanza duniani kufanya kazi kwa kutumia thorium kama mafuta, katika mfumo wa chumvi iliyoyeyuka — bila kutumia maji wala shinikizo kubwa.
Mtambo huu unaweza kuwekwa hata jangwani au maeneo ya mbali yasiyo na maji – jambo linalovutia zaidi.
SEHEMU YA TATU: THORIUM NA TANZANIA – RASILIMALI TULIYOIKALIA
Ukweli mchungu ni kwamba
Thorium si madini ya ajabu wala adimu. Tanzania, kupitia miamba ya pegmatite na madini ya monazite, inatajwa kuwa miongoni mwa nchi zenye hifadhi ya madini haya – hasa maeneo ya Ulanga, Mbeya na Ruvuma.
Taarifa hizi zipo, lakini zimeachwa kwenye ripoti za utafiti bila mpango madhubuti wa kuyatumia kwa mustakabali wa nishati safi.
Je, tunawezaje kujifunza kutoka kwa Wachina?
- Moja: Tunahitaji sera ya taifa ya utafiti na ubunifu katika nishati mbadala – isiwe kwenye karatasi tu bali yenye bajeti na utekelezaji.
- Mbili: Vyuo vyetu vikuu vianzishe program za nuclear engineering na material science zenye mwelekeo wa kutumia madini yetu kwa faida ya kiuchumi.
- Tatu: Ushirikiano wa kimataifa ulenge uhamisho wa teknolojia na si utegemezi wa vifaa vilivyotengenezwa tayari.
SEHEMU YA NNE: TUNAPASWA KUTAZAMA MBALI – SIYO KUTAZAMA TUMBO
Katika taifa lenye changamoto ya upungufu wa umeme, kupanda kwa bei ya mafuta, na utegemezi mkubwa wa vyanzo vya nishati vya kizamani – kufikiria juu ya teknolojia ya nyuklia inaweza kuonekana kama ndoto.
Lakini kila mafanikio huanzia kwenye ndoto zenye maono. Hatuwezi kuwa nchi ya viwanda kama hatuwezi kufikiria mbele ya wakati.
Mfumo wa TMSR unaweza, kwa muda mrefu:
- Kuondoa utegemezi kwa makaa ya mawe na mafuta,
- Kutoa umeme wa uhakika kwenye viwanda na migodi,
- Kupunguza gharama ya uzalishaji na kuongeza ushindani wa bidhaa zetu.
HITIMISHO: MAARIFA HAYANA TAIFA – LAKINI TAIFA LISILOYAWEKA KWENYE MIPANGO HUENDA LIKAANGAMIA
Wachina hawakugundua upya gurudumu – wamesoma, wakachambua, wakaendeleza.
Leo hii wanaongoza mbio za kuwa taifa la kwanza kutumia kikamilifu thorium kama chanzo salama, safi na nafuu cha nishati.
Sisi Watanzania tuna nafasi, tuna rasilimali, na tuna akili. Tunachokosa ni dhamira ya kisera na uwekezaji wa kisayansi unaolenga vizazi vijavyo.
Je, bado tutazidi kusema ‘hatuna uwezo’ au tutaanza kuuliza ‘tunafanyaje tufike huko’?
Muda wa kufikiri kisayansi ni sasa – si kesho.