Anaandika, Robert Heriel
Mtibeli.
Kila mtu kasema lake, wapo waliomsifu na wapo waliomponda. Mimi nitajadili Jambo hili Kwa uchache katika mizania ya Haki, ukweli na upendo. Kama mnavyojua mambo hayo Matatu ndio ninayoyapigia debe. Hiyo ndio dini ya Watibeli.
Kwa taarifa za kesi nilivyoisikia mpaka sasa nadiriki kusema HAKIMI hakutenda HAKI. Kwa sababu zifuatazo;
1. Hakimi hakuwa mwaminifu.
Hakimi hakuwa mwaminifu katika ndoa yake katika maeneo yafuatayo;
a) Mapenzi, HAKIMI anatuhuma za kum-cheat Mkewe achilia mbali hiyo kesi ya ubakaji inayomkabili.
b) Fedha na Mali,
HAKIMI hakuwa mwaminifu katika suala la fedha na Mali katika ndoa. Kukosa uaminifu, kutokuwa mkweli kunamfanya Hakimi asiwe mwenye Haki.
2. Hakimi hakumpenda mkewe.
HAKIMI anampenda Mama yake kuliko Mkewe. Hii katika mahusiano ya ndoa sio Haki kwa Mke au Mume. Kwenye ndoa au familia ni Haki ya Mke au Mume kupendwa na Mwenza wake kuliko MTU yeyote Yule.
Haiwezekani 80% umuingizie Mama yako Wakati umeoa na unampenda Mkeo au Mumeo. Upendo wa Hakimi kwa Mama yake ni mkubwa maradufu kuliko alivyompenda Mkewe. Hiyo sio Haki.
3. Hakimi alikusudia kumtapeli Mkewe. Hakuwa anampenda.
Ndio maana aliweza kum-cheat na kumsaliti kimapenzi na muda huohuo akawa anamficha masuala ya Mapato yake. Huo ni Utapeli, na hii ni Kutokana alikuwa hampendi.
Mambo ya muhimu;
1. Kama HAKIMI angekuwa mwenye Haki angekuambia Binti wa watu tangu mwanzo kuwa Kipato changu kitakuwa kinamilikiwa Kwa sehemu kubwa na Mama. Ili binti mwenyewe aamue. Hii ni pamoja na Mali zitakazonunuliwa Kutokana na kipato chake. Kama wanavyofanya Watu wengine wenye Haki.
2. Yule Mwanamke hakuomba Talaka Kwa lengo la Kutaka Mali za Hakimi, isipokuwa ni Makosa ya Hakimi ya kutokuwa mwaminifu Kwa kumsaliti ndio kumemfanya aombe Talaka. Kwa watu waaminifu na wenye Haki Usaliti ni kosa lisilosameheka.
3. Ni kweli Mshahara wa mtu anaweza kuutumia vile atakavyo ilimradi anatekeleza majukumu ya kifamilia vizuri.
Hivyo Hakimi anaweza kuwa na Haki ya kutumia Mshahara wake atakavyo. Tatizo linakuja Kuwa matumizi ya Pesa au kipato yatatafsiri moyo wa mtu ulipo. Wanasema hazina ya mtu ilipo ndipo moyo wake ulipo.
Hakuna Mwanamke ambaye atajiona anapendwa ilhali zaidi ya 80% ya kipato cha mume wake kinatumika nje ya matumizi ya Nyumbani.
Jambo moja la kuweka Akilini hapa ni kuwa, Wanawake Hawana sababu ya kuogopa Michezo ya namna Hii Kwa sababu nao ni kina Mama wamezaa, hivyo Kile wanachokifanya wanaume ndicho watakachokifanya Watoto wao.
Hii ni kusema, ikiwa kuna mwanaume atamuiga Hakimi kuwekeza Kwa Mamaye, vivyohivyo watoto wako uliowazaa watawekeza kwa mkeo (Mama Yao) uliyemkatili. Hivyo Ngoma inakuwa droo!
Kwenye upendo kuna ukweli na Haki. Kwenye upendo mambo ya Pesa na Mali hayawezi kuwa kitu kikubwa.
Alichofanya HAKIMI ni uhuni, hasa kama ni kweli amem-cheat Mkewe mpaka akaomba Talaka. Ni uhuni ambao Watibeli hatuuungi Mkono. Na inaonekana Amekataa hata kuomba Msamaha.
Ieleweke kuwa ku-cheat Kwa wengine ni kosa lisilosameheka. Na hakuna mwenye uhalali WA ku-cheat iwe mwanaume au Mwanamke.
Wewe kama unajijua huwezi kuwa mwaminifu ni Bora usioe au kuolewa. Kwani unachoenda kufanya ni utapeli, uhuni na dhulma
Nipumzike sasa.
Robert Heriel,
Taikon wa Fasihi,
Kwa sasa Dar es salaam.