Mohamed Said, huu ni mchango wangu wa mwisho katika santuri hii yako ambayo imechuja lakini bado wapo watu wanaomeza tu ngano zako bila takafuri yoyote.
Wakati wote unapodai unaandika historia ya Waislaam ukweli ni kuwa unaandika historia ya wazee wako, Wazulu na Wamanyema.
Unapodai unaandika historia ya Watanganyika ukweli ni kuwa unaandika historia ya wazazi wako na babu zako,Wamanyema na Wazulu.
Kwa kukufahamisha Watanganyika walikuwepo sana tu ingawa huwapi kipaumbele stahiki katika hizi ngano zako.
Huwezi kuongelea AA bila kumtaja muasisi na Kiongozi wake Mkuu wakati inaanzishwa mwaka 1929 na huyo si mwingine bali Mtanganyika Myao na Msomi Hayati Mwalimu Cecil Matola.
Baada ya Matola kufariki, AA ilikosa uongozi madhubuti hali iliyoifanya AA kuwa kama chombo kilichokosa dira hadi Zanzibar ilipojitoa mwaka 1948 na kuzaliwa TAA.
Lakini hata ilipozaliwa TAA, uongozi thabiti ulikuja kupatikana mwaka 1950, Mtanganyika Mhaya Dr. Vedasto Kyaruzi alipochaguliwa kuwa Raisi wake wa kwanza.
Baada ya Wakoloni kumpa uhamisho wa nguvu Raisi wa TAA, shughuli za TAA zilizorota kwa sababu kiongozi mkuu hakuwepo.
Kumbuka kwamba Dr. Kyaruzi alipopewa uhamisho wa kwanza hakupelekwa mbali na hivyo aliweza kuendelea kuwasiliana na wasaidizi wake mojawapo akiwa Abduwahid Sykes.
Wakoloni walipogundua hilo ilibidi wamhamishe tena wampeleke mbali zaidi ili mawasiliano na wasaidizi wake yawe magumu zaidi na hivyo kupelekea TAA kuzorota hadi ujio wa Mwalimu Nyerere mwaka 1952.
Hivyo nafasi ya Abdulwahid Sykes ndani ya TAA wakati Mwalimu Nyerere yuko Makerere ni kwamba wakati huo TAA haikuwapo, ilikuwepo AA iliyoasisiwa na Cecil Matola mwaka 1929.
Huyu Abdulwahid Sykes unamtajataja sana na bila shaka kwa sababu unazozijua wewe mwenyewe lakini ukweli ni kwamba hakuwahi kuwa kiongozi Mkuu wa TAA wala TANU wakati wowote ule.
Dai la kuwa ndiye alipendekeza jina la TANU ni kweli kwa kiasi Fulani kwani alichofanya ni kwamba jina alilopendekeza awali Mwalimu Nyerere lilikuwa gumu kidogo kutamkwa kwa haraka ingawa maneno yalikuwa yale yale.
Mwalimu Nyerere alitaka maneno manne yasikosekane nayo ni
AFRICAN, TANGANYIKA, NATIONAL na
UNION yawepo na iliyobakia ni namna tu ya kuyapanga na ndipo Abdulwahid Sykes kupendekeza
Tanganyika African National Union (TANU)
Mag3,
Cecil Matola alifariki mwaka wa 1933 miaka minne baada ya kuasisiwa kwa African Association na akiishi Mission Quarter.
Nyumbani kwake ndiko mkutano wa kuasisi African Association ulipofanyika.
Waliohudhuria mkutano huu walikuwa yeye Cecil Matola, Kleist Sykes, Mzee bin Sudi, Ibrahim Hamisi, Ali Said Mpima, Zibe Kidasi, Rawson Watts na Raikes Kusi.
Haya majina kayaandika Kleist katika mswada wa kitabu cha maisha yake ambao ndiyo rejea kuu ya historia ya African Association.
Kleist katika mswada wake anaeleza sababu kwa nini waliokuwa wamejitokeza katika siasa walikuwa wengi Waislam na akaeleza kuwa kabla ya African Association, mwakilishi wa Waafrika Alikuwa Father Gibbons kutoka Pugu Mission.
Katika mswada huu yapo mengi yaliyoelezwa pamoja na msuguano uliokuwa unatokea mara kwa mara kati ya wenyeji na hiki kizazi cha kwanza cha watoto wa wahamiaji kutoka Sudan, Belgian Congo na hawa Wazulu kutoka Mozambique waliopewa jina la "Wakuja" yaani Wanubi kama Ibrahim Hamisi, Wamanyema kama Mzee bin Sudi na Wazulu kama Kleist Sykes.
Walikuwa wakilaumiwa kwa kujitia kimbelembele katika mambo ya Dar es Salaam ilhali wao ni ''wageni.''
African Association wao viongozi wapo, Maulid Committee wao viongozi wapo, ilmradi hawapungui.
Umesema kweli kuwa naandika historia ya wazee wangu Wamanyema na Wazulu lakini na wengine pia kama Ali Said Mpima, Mwinjuma Mwinyikambi, Max Mbwana, Said Chamwenyewe kuwataja wachache ambao ni Wamashomvi, Warufiji na Wazaramo pia nimeandika historia zao.
Nimeandika hadi historia za Waafrika ambao hawakuwa Watanganyika lakini walishiriki katika kupigania uhuru wa Tanganika kama Dome Budohi Mkenya na Denis Phombeah Mnyasa,
Hawa wamesahauliwa na historia mimi nimekuelezeni kuwa walikuwapo na picha zao nimekuonyesheni.
Watafute kwenye kitabu changu utawakuta.
Kuwa siwapi kipaumbele hii si kweli kila mmoja nimemweleza kwa stahili yake.
Kuwa Cecil Matola ni muasisi wa African Association mswada wa Kleist haukumueleza kwa sifa hiyo.
Kleist ameeleza jinsi yeye alivyokutana na Dr. Aggrey mwaka wa 1924 na akamshauri kuasisi chama hicho.
Si kweli kuwa alipofariki Cecil Matola chama kilikosa uongozi madhubuti.
Mzee bin Sudi alichaguliwa kuwa Rais na huu ndiyo mwaka Kleist na Mzee bin Sudi waliunda Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika (Umoja wa Waislam wa Tanganyika).
Nafasi walizoshika katika Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika ni hizo hizo walizoshika katika African Association.
Maendeleo haya si dalili ya viongozi waliochoka.
Umemtaja Dr. Vedasto Kyaruzi na TAA kuzaliwa 1950.
Hakika huijui historia ya TAA.
TAA ilibadili jina 1948 wala haikuwa kuwa chama kipya kimeanzishwa na sababu ni kujitofautisha na African Association ya Zanzibar.
Lakini umeshindwa kueleza Dr. Kyaruzi kaingia vipi katika uongozi wa African Association mwaka wa 1950.
Nina mswada wa Dr. Kyaruzi, "Mhaya Doctor," kuna sura kaipa jina, "Action Group," humo kaeleza mchango wa Dr. Tsere na yeye katika African Association na kamtaja Abdul Sykes na "uncle," wake Schneider Abdillah Plantan katika mabadiliko haya.
Unaweza kusema Schneider, Hamza Mwapachu ndiyo waliofanya mabadiliko haya ya uongozi.
Ati Abdul Sykes "msaidizi," wa Dr. Kyaruzi.
Hii wewe umeitoa wapi nimeipenda sana kama una ''citation.'' nipatie.
Hayo yote ya Dr. Kyaruzi hayapo popote katika historia za TANU zilizoandikwa isipokuwa katika kitabu cha Abdul Sykes halafu unanirudishia mimi historia uliyoisoma kutoka kitabu changu.
Umenifurahisha sana
Kumtajataja Abdul Sykes.
Mimi si "nimemtajataja," nimemwandikia kitabu kizima na humo ndimo ulipotoa mengi uliyoandika hapa.
Kivukoni wamejaribu kuandika historia ya TANU bila kumataja Abdul Sykes.
Sina haja ya kukueleza balaa lake.
Tuko hapa mwaka wa 10 tunamjadili Abdul Sykes.
Abdul Sykes hakushika nafasi ya kuongoza TANU lakini mikutano yote ya siri ya kuunda TANU na "retreat" zote baada ya kuunda TANU walizokuwa wanafanya viongozi wa TANU wakiwa na jambo zito, mikutano hii ikifanyika nyumbani kwake Mtaa wa Stanley na Sikukuu.
Ushajiuliza kwa nini?
Ushajiuliza kwa nini Nyerere alipofika Dar es Salaam mwaka wa 1952 alikwenda nyumbani kwa Abdul na alipojiuzulu kazi mwaka wa 1955 alikwenda kukaa kwa Abdul?
Jina la TANU wala si kitu mimi na wewe tuvutane hapa.
Mimi nakuuliza kitu kimoja.
Haikushangazi kuwa historia ya TANU haimtaji Abdul Sykes au mdogo wake Ally au baba yao Kleist kama waasisi na wafadhili wa harakati hizi?