CHIFU ALIYEKUWA NA WAKE ZAIDI YA 100. NI SILIMBWELU MWAKALUKWA MWAMAKULA!
Baba aliponiambia ya kuwa baba yake mkubwa alikuwa na wake zaidi ya 100 sikuweza kuamini kwa sababu haikuweza kuingia akilini mwangu ya kuwa mtu angeweza kuwa na wake wa kuoa zaidi ya 100.
Lakini baadaye, niliweza kuongea na mmoja wa wajukuu zake wengine ambaye ni mkubwa kwa umri kuliko mimi ambaye alikadiria kuwa Chifu huyo alikuwa na wake kati ya 82 au zaidi. Hivyo kwa ajili ya kutunza historia nikaacha simulizi ya baba yangu kuwa alikuwa na wake 100 na zaidi nikawa nasema na kuandika ile idadi ya wake 82.
Lakini wiki hii, nabadilisha historia hiyo nikiwa na mamlaka ya kihistoria kwa babu alikuwa na wake zaidi ya 100 kama nilivyoambiwa na baba yangu, Chifu Timoti Bandekile Mwalubanga Mwamakula wa Itunge, Kyela baada ya kupata ushahidi wa jambo alilonieleza baba mwaka 1984 nilipokuwa naye kijijini Itunge. Ushahidi huo ni picha ya chifu mwenyewe iliyopigwa na wamisionari wa Kanisa la Mmoravian kutoka Ujerumani kati ya mwaka 1829 na 1830. Katika picha hiyo, chifu anaonekana akiwa pamoja na wake zake wawili. Utambulisho wa wake hao ni jambo la kulifanya katika andiko lingine.
Wamisionari hao wa Kijerumani walieleza kuwa Chifu huyo alikuwa na wake 100, lakini siku ile wakati wanampiga picha, aliongozana na wake zake wawili. Hivyo, picha hii ina umri wa miaka 94 wakati huu ninapoandika habari hii. Lakini je chifu huyo ni nani?
Huyu ni Chifu Silimbwelu jina lingine alijulikana kama Kifukwe. Baba yake alikuwa Chifu Mkuu Mwanyesya Mwamakula (Mwamakula I) lakini mama yake, Kugwilila Kalukwa alikuwa ni mke mkubwa kati ya wake 14 wa Chifu Mwamakula I. Wake wengine walikuwa Igwengelile Kalinga, Kyeja, Ngupili, Twandeabangi Kisunga, Seba, Kapala, Bwagilo, Ipungu, Ihojo, Ngupili, Kalile, Kibinga na Inyekule.
Kwa kuwa mama yake alikuwa mke mkuu wa Chifu Mwamakula I, baada ya kifo baba yake mdogo Chifu Mkuu Mwanjabala Mwamakula (Mwamakula II), Silimbwelu akawa Chifu Mkuu akitawala Mwaya na Chifu Kilota Mwakalinga Mwamakula wa Kajunjumele, Kyela ambaye mama yake, Kalinga alikuwa ni mke wa pili na yeye akapewa utawala Kajunjumele, Kyela.
Chifu Mwanjabala Mwamakula (Mwamakula II) aliwasimika utawala Silimbwelu na Kilota muda mfupi kabla hajafariki dunia mwaka 1853. Hata hivyo, bado hatujakubaliana juu ya mwaka wa kifo cha Chifu Mwanjabala Mwamakula na hata mwaka aliowasimika uchifu hao wanae wawili.
Yeye ndiye aliyetawala eneo lote - Mwaya na nKilwa (Kajunjumele). Eneo hilo la utawala ni karibu nusu ya Wilaya yote ya Kyela. Maeneo yaliyobaki ya Itete yalitawaliwa na ndugu zake wa ukoo wa Chifu Mwakipesile, Makwale ilitawaliwa na Chifu Mwambelo na Nndamba ikitawaliwa na Chifu Mwakabulufu.
Lakini Chifu Silimbwelu Kifukwe Mwakalukwa Mwaisaka Mwamakula aliwapataje wake wote hao zaidi ya 100? Wake zake wakubwa wawili alilipiwa mahali (aliozwa) na baba yake Chifu Mwanjabala Mwamakula (Mwamakula II), lakini wake zake waliofuatia kwa ukuu, mahali ililipwa na mafumu (wasaidizi wa chifu). Lakini wake wengine alilipa mahali yeye mwenyewe baada ya wake zake wakubwa kumletea wadogo zao waolewe naye (ukusakuligwa au isakulwa). Wake wengine alioa mwenyewe au aliletewa na mafumu (wasaidizi wake) lakini mahali alilipa yeye mwenyewe.
Wake wengine aliwarithi kutoka kwa nduguze. Kwa mfano, baada ya Chifu Kilota Mwakalinga Mwamakula kufariki dunia mwaka 1897, wake zake wakiwemo Itenda na Inyekule walikwenda Mwaya kurithiwa na Chifu Silimbwelu ambapo alipata au alizaa nao watoto wengi pia. (Lakini huyo Inyekule sio Inyekule aliyekuwa mke wa Chifu Mkuu Mwanyesya Mwamakula). Lakini kuna wake aliowaoa kutoka kwa machifu wa himaya nyingine ikiwa njia yake ya kuimarisha utawala wake. Machifu hao ni wale wa Tukuyu, Busokelo, Makwale, Itete, Bulambya, Bukinga, Ileje nk.
Chifu Mkuu Silimbwelu Kifukwe Mwakalukwa Mwaisaka Mwamakula alifariki mwaka 1932 akiwa ameshiba umri wa miaka mingi sana. Wajukuu zake wengi hawajuani ingawa kila mjukuu anajijua kuwa ni mjukuu wake. Lakini baadhi ya watoto wake maarufu ni pamoja na Chifu Fubile Mwakisisile Mwamakula, Chifu Lazaro Mwakisisile Mwamakula, Mchungaji Chifu Makilini Mwakyusa Mwamakula, Mch. Anyigulile Mwakajoka Mwamakula na binti yake Lamasani Kalukwa.
Chifu Silimbwelu alimpenda sana mtoto wa dada yake. Mtoto huyo namkumbuka kwa jina moja la Mpombo. Kutokana na kupendwa sana na Chifu, Mpombo aliheshimiwa kama chifu na majirani zake. Lakini huyo Mpombo alikuwa pia na utisho wa aina yake.
Marehemu Chifu Francis Kifukwe Mwambinga Mwakalukwa Mwamakula, aliyefariki India siku ya Jumamosi, ni mjukuu wa Chifu Silimbwelu akiwa mtoto wa mwisho wa Chifu Mchungaji Makilini Mwakyusa Mwamakula ambaye pia alikuwa mmoja wa watoto wakuu au watawala wa Chifu Silimbwelu na hivyo alikuwa kitukuu wa Chifu Mkuu Mwamakula I wa Mwaya.
NB: Picha inamuonyesha Chifu Silimbwelu Mwakalukwa Mwaisaka Mwamakula baada ya kushiriki Ibada katika Kanisa la Moravian kati ya mwaka 1929 na 1930. Chifu alifariki dunia miaka miwili baadaye, mwaka 1932, akazikwa pamoja na baba zake Chifu Mwamakula I na Chifu Mwamakula II huko Mwaya, Kyela. Lakini picha hii pia ni kwa hisani kubwa ya Rungwe Moravian Misheni, Tukuyu.
Je, nini kimekushangaza? Je, nini maoni yako?
Mwana Kondoo Ameshinda! Tumfuate!
Askofu Emmaus Bandekile Mwamakula
Kitukuu wa Chifu Mkuu Mwanjabala Mwamakula (King Mwamakula II) wa Mwaya
Itunge, Dar es Salaam; 18 Agosti 2026; Saa 1:10 magharibi.