Naamini kifo cha Magufuli kitaleta muelekeo mpya kwenye masuala kadhaa ikiwemo utawala bora na haki za binadamu, ili kulileta pamoja tena taifa letu.
Lakini kwenye kufanya kazi kwa bidii itabidi tumuenzi kwa kuendeleza pale alipoishia, ameonesha kwa vitendo kuwa kiongozi mkuu wa nchi unatakiwa kuwatumikia watanzania kwa dhati, sio kukaa tu ofisini, ili kuwapelekea maendeleo ya kweli wananchi.
Na masuala mengine yakiwemo kulinda mali za umma, na uwajibikaji, watu wasifanye kazi kwa mazoea, ukikosea mahali pako pa kazi uwe tayari kuwajibika/wajibishwa, pia uthubutu wake kwenye utendaji ikiwemo ujenzi wa miradi mikubwa kama SGR na mingineyo.
Hakuna mwanadamu aliye mkamilifu. Kuna mambo ambayo sidhani kuna atakayepinga - Rais Magufuli alitamani sana Tanzania iwe na maendeleo makubwa kwa muda mfupi. Dhamira yake hiyo, kuna wakati ilimfanya afanye makosa hapa na pale, lakini kuna mengi mazuri aneyafanya.
Mwalimu aliwahi kusema, 'wakati wa utawala wangu, kuna maeneo tulifanya makosa, tusifanye makosa, sisi ni malaika? Kila utawala utafanya mazuri, utafanya makosa pia. Utawala unaofuata unayachukua mazuri, unayaacha mabaya. Kinachoshangaza, kuna wakati mnachukua mabaya mnayaacha mazuri".
Mazuri aliyoyafanya, tuyaenzi na kuyaendeleza. Yaliyo mabaya tuyaache. Mambo yafuatayo, tuyaendeleze na kuyaboresha:
1) Kupambana na ujambazi. Kwenye hili tuangalie namna ya kuhakikisha yale mapambano dhidi ya ujambazi wa mtaani yanaendelea. Lakini tuongezee udhibiti wa ujambazi wa vyombo vya dola dhidi ya raia. Mauaji, utekaji na upotezwaji wa watu unaofanywa na wasiojulikana; na mauaji ya watuhumiwa yanayofanywa na Polisi.
2) Ujenzi wa miundombinu. Ukiachilia ujenzi wa reli na bwawa la umeme, barabara za mijini nyingi zilitengenezwa
3) Udhibiti wa matumizi ya fedha za serikali
4) Ukusanyaji wa kodi ulioboreshwa, unaozingatia dhamira ya kukuza biashara, mitaji na uwekezaji
5) Nidhamu ya watumishi wa umma
6) KUFANYA KAZI KWA BIDII - Marehemu alilikazia sana jambo hili, na hakika ni msingi sana. Ujanja ujanza hautalipeleka Taifa popote
Yanayotakiwa kuangaliwa upya na kurekebishwa haraka:
1) Haki za watu, uhuru wa maoni na uhuru wa vyombo vya habari
2) Haki ya kukosoa bila kubughudhiwa
3) Tume huru ya uchaguzi
4) Katiba mpya ya wananchi
5) Haki za vyama vya siasa kufanya siasa
6) Kufanya mabadiliko ya haraka yatakayoruhusu demokrasia kumea na kukua. Kwenye eneo hili tulirudi sana nyuma kiasi hata cha kushindwa kufanya uchaguzi ambao una sifa ya kuitwa uchaguzi 2020. Viongozi waliopo, hasa wabunge wautambue ukweli kuwa wao kwa kiasi kikubwa ni wateuliwa na wala hawakuchaguliwa na wananchi. Kwa kuujua ukweli huo wanastahili kuenenda kwa hekima badala ya kiburi.
7) Wajibu wa kuwafikisha wahalifu wote waliotenda uovu kwa kivuli cha uzalendo.