Kiteto kuweka historia leo
na Joseph Zablon
Tanzania Daima~Sauti ya Watu
WAKATI uchaguzi mdogo wa mbunge wa Kiteto unafanyika leo, mji wa Kiteto na vitongoji vyake jana ulikuwa katika heka heka kubwa kutokana na shamrashamra za wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kufunika za wapinzani wao, Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Hali hiyo iliibuka baada ya kumalizika kwa mkutano wa mwisho wa kampeni za uchaguzi za Chadema zilizohitimishwa na Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Freeman Mbowe.
Hali katika mitaa mbalimbali ya mji wa Kiteto ilikuwa ya uchangamfu mkubwa kwa wafuasi wa Chadema ambao baada ya kumalizika kwa mkutano huo walianza kuandamana kumsindikiza Mwenyekiti wao, Mbowe pamoja na Mgombea wa chama hicho Victor Kimesera waliokuwa katika gari moja.
Wakati wafuasi wa Chadema wakiandama kumsindikiza mgombea na mwenyekiti wao, wenzao wa CCM walikuwa wamesimama pembeni mwa barabara wakiwaangalia kwa namna ya kuwashangaa.
Hekaheka za maandamano hayo zilianza baada ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, kumtangaza mgombea ubunge kupitia chama hicho, Victor Kimesera, mbele ya mamia ya wananchi waliojitokeza kwenye mkutano huo.
Mara baada ya kumalizika kwa mkutano huo, umati wa wafuasi wa CHADEMA pamoja na wakazi wengine wa mji huo waliohudhuria mkutano huo, walianza kulisukuma gari lililokuwa limembeba Mbowe na Kimesera hadi hosteli za Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) ambako viongozi hao wamefikia.
Awali akizungumza katika mkutano wa kuhitimisha kampeni za uchaguzi huo, Mbowe alisema wakati umefika kwa wananchi wa Kiteto kupigana na umaskini na kuachana na ushabiki wa vyama kwa vile CCM kimekuwa chama cha matajiri walioko Dar es Salaam na katika miji mingine mikubwa.
Kwa maana hiyo nawaomba wananchi wa Kiteto kutumia nafasi yenu kesho (leo) kufanya mapinduzi katika maisha yenu, kuchagua upinzani kupitia mgombea wetu Kimesera,alisema Mbowe.
Alisema katika kipindi cha miaka 46 tangu Tanzania ilipopata uhuru, kipindi ambacho CCM kimekuwa madarakani, hakuna cha maana kilichofanyika kwa Watanzania wakiwemo wananchi wa Kiteto.
Kwamba vijana wengi waliozaliwa wakati Tanzania inapata uhuru walizaliwa katika maisha duni, wamekulia katika maisha duni na sasa wakiwa katika umri wa utu uzima bado wanaishi maisha duni.
Alisema sehemu nyingi za taifa hili hazina huduma muhimu na za msingi kama vile zahanati, barabara za kuaminika na shule za maana kwa ajili ya watoto.
CCM ina wenyewe, ni wale wanaoishi Oysterbay, Masaki na Mikocheni na si ninyi mlioko huku vijijini, mmekuwa mkitumiwa kwa ajili ya kupiga kura, alisema.
Mbowe ambaye jana alitumia tena helikopta baada ya juzi kushindwa kuitumia kutokana na kupata hitilafu aliweza kumnadi Kimesera katika kata nane za mji wa Kiteto ambazo ni Dodosi, Songambele, Olgune, Ongasero, Matuli, Naniroki, Njolo, Narangitomoni na Kibaya.
Kabla ya Chadema kufanya mkutano huo, CCM ilifanya mkutano wake wa kuhitimisha kampeni kaktika Shule ya Msingi Kibaya.
Katika mkutano huo, Makamu Mwenyekiti wa CCM, Pius Msekwa, alimnadi kwa mara ya mwisho mgombea wa chama hicho, Benedict ole Nyangolo, kwa kuwataka wapiga kura wa jimbo hilo kumpigia kura za ndiyo.
Msekwa aliwataka wana Kiteto kutochagua mgombea mwingine kwa sababu hawezi kuwaletea maendeleo. Katika mkutano huo, kikundi cha Tanzania One Theatre kilitumbuiza.
Msimamizi mkuu wa uchaguzi wa Jimbo la Kiteto, Feston Kamombe, jana aliwaambia waandishi wa habari kuwa maandalizi yote yamekamilika na kwamba zoezi la kupiga kura litaanza saa moja asubuhi leo.
Kabla ya kufanyika uchaguzi huo leo, kumekuwa na matukio mbalimbali yasiyo ya kawaida ya kupigwa kwa baadhi ya viongozi waandamizi wa Chadema na kundi la watu wanaodaiwa kuwa wafuasi wa CCM.
Kufuatia vitendo hivyo, Jeshi la Polisi limeimarisha ulinzi katika sehemu zote za Kiteto.