Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam,
Paul Makonda, nakuandikia ujumbe huu mfupi kupitia mtandao huu wa kijamii wa Jamiiforums kutokana na kinachoendelea dhidi yako. Mitandaoni kunaandikwa na kusemwa kuwa unahusika na kutumia cheti ambacho si chako cha kidato cha nne. Wapo wanaofikia hata kukuita jina la Daudi Albert Bashite.
Najua wewe ni kiongozi wa kiserikali: Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam. Najua kuwa Rais alikuwamini kila idara inayokuhusu kabla ya kukuteuwa kuwa katika nafasi hiyo. Najua kuwa Rais anakufuatilia kila uchao kama mteule wake. Najua pia nafasi yako kiuongozi inakupa heshima na hadhi tofauti katika jamii ya watanzania.
Kuambiwa kuwa umetumia cheti cha mtu mwingine kwakuwa wewe ulifeli kwa kupata sifuri (kulingana na Mchungaji Gwajima) ni suala kubwa. Ni suala linalogusa maadili,heshima na hata utendaji wako. Cheti ndicho kinachompa mtu nafasi fulani ya kimaisha katika jamii na ndiyo maana kinapaswa kwanza kuwa cheti chake mwenyewe muhusika.
Kelele nilizozisema hapo juu zikiendelea zitaonekana ni ukweli. Mkuu wa Mkoa,
Paul Makonda, nakushauri ufanye hivi. Kama unaamini kuwa unachafuliwa na kutwezwa kwakuwa kinachosemwa si kweli, waburuze mahakamani wote wanaokuchafua na uwadai mabilioni kulingana na heshima na hadhi yako. Tafadhali usitumie vyombo vya dola kwa mambo yako binafsi.
Muda wa kuweka kumbukumbu zako sawa ni huu kwakuwa unapaswa kuuanika ukweli juu ya kinachosemwa. Zinatumika media katika suala hili kwakuwa nawe ni mtumiaji mzuri wa media hizo. Nawe tumia media kujisafisha na kutangaza kuwashughulikia kimahakama wote wanaosema hayo, kama wanayoyasema si kweli. Kama ni kweli, endelea kukaa kimya.