Mama Amon bandiko lako limelenga uhuru wa kitaasisi ambao kimsing ni zao la sheria zinazounda taasisi husika. Swali langu ni dogo tu: Je uhuru wa kifikra kwa watendaji wa taasisi husika upo ?
Sijaelewa kwa nini unatofautisha uhuru wa kitaasisi na uhuru wa mtu mmoja mmoja ndani ya taasisi. Kwa maoni yangu taasisi ni watu. Uhuru wao una vikwazo vya ndani, kwa upande mmoja, na vikwazo vilivyo nje ya miili yao, kwa upande mwingine. Sheria mbaya ni vikwazo vya nje ya miili yao. Ujinga wao, hofu zao, mashaka yao, imani zao za kisiasa, etc ni vikwazvo vya ndani ya miili yao. Aina zote mbili za vikwazo zinaikwaza Tume kama taasisi.
Kwa ufafanuzi zaidi, soma maelezo haya.....
Tofauti kati ya uhuru na utumwa
Tamko kwamba, “Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Tanzania inapaswa kuongezewa uhuru ili iweze kutekeleza kazi zake kwa kasi na ufanisi stahiki,” haliwezi kutetewa au kupingwa kwa ufanisi kama hatujakubaliana kuhusu maana ya “uhuru” inaotakiwa kuongezwa.
Napendekeza kwamba, fasili nzuri ya neno “uhuru” ambalo ni kinyume cha neno “utumwa,” ni ile iliyotolewa mwaka 1967 na Profesa Gerald C. MacCallum (1925-1987) wa Marekani.
Kupitia makala yenye kichwa cha maneno, "
Negative and Positive Freedom," iliyochapishwa katika Jarida la “
The Philosophical Review,” toleo namba 76.3, ukurasa wa 312 hadi 334, mwaka 1967, MacCallum aliwakosoa kwa ufanisi wanafilosofia wanaopenda kuugawanya uhuru katika makundi mawili ya “uhuru hasi” na “uhuru chanya.”
Badala yake, MacCallum (1967) alipendekeza kwamba,
“…freedom is thus always of something (an agent), from something (constraint), to do, not do, become, or not become something (goal); it is a triadic relation.” (uk. 314)
Ndio kusema kuwa, “uhuru ni mahusiano kati ya vitu vitatu kwa mpigo, kwani mara zote tunapoongelea uhuru tunamaanisha uhuru wa
MTENDAJI, dhidi ya
VIKWAZO vinavyoweza kumkabili mtendaji huyo, katika azma yake ya ama kufanya/kutofanya kitendo fulani, au kuwa/kutokuwa katika hali fulani, hili la mwisho likiwa ni
LENGO lake.” (Tafsiri yangu).
Katika fasili hii, MacCallum (1967) anasema mambo mawili kwa mpigo, moja likihusu maana ya “uhuru” na jingine likihusu maana ya “utumwa.”
Kuhusu “uhuru,” MacCallum (1967) anasema kuwa, madai yoyote kuhusu kuwepo kwa “uhuru” katika mazingira fulani, ni madai yanayoambatana na uwepo wa kitu kinachotambuliwa kama
MTENDAJI, uwepo wa kitu kinachotambuliwa kama
KIKWAZO dhidi ya uamuzi wa mtendaji, na uwepo wa kitu kinachotambuliwa kama
LENGO la mtendaji, ambapo, kwa sababu ya kutobanwa na vikwazo, mtendaji yuko huru kuyafukuzia malengo yake kwa ufanisi.
Na kuhusu “utumwa” MacCallum (1967) anasema kuwa, madai yoyote kuhusu kuwepo kwa “utumwa” katika mazingira fulani, ni madai yanayoambatana na uwepo wa kitu kinachotambuliwa kama
MTENDAJI, uwepo wa kitu kinachotambuliwa kama
KIKWAZO dhidi ya uamuzi wa mtendaji, na uwepo wa kitu kinachotambuliwa kama
LENGO la mtendaji, ambapo, kwa sababu ya kubanwa na vikwazo, mtendaji anashindwa kuyafukuzia malengo yake kwa ufanisi.
MacCallum (1967) anafananua kuwa, vikwazo vya uhuru vinaweza kuwa nje au ndani ya mwili wa mtendaji.
Kikwazo cha uhuru kilicho nje ya mwili wa mtendaji, ni kitu kama vile mtu mwingine, kikwazo asilia kama vile mafuriko yaliyoziba barabara, minyororo uliofungwa mguuni mwa mtu, pingu zilizofungwa mikononi mwa mtu, ukosefu wa ajira, mdororo wa uchumi unaosababisha mzunguko hafifu wa fedha, na kadhalika.
Hivyo, kwa kuzingatia vikwazo vya nje, mtu atakuwa sio huru endapo mfumo au watu wengine wanamzuia kufanya anachotaka kukifanya, wanamkataza kwenda anakotaka kwa kumfungia chumbani, anataka kwenda mahali lakini anaogopa kufika huko kwa kuwa kuna mbwa mkali, au anataka kwenda mahali lakini hana nauli ya kumwezesha kusafiri hadi huko.
Na vikwazo vya uhuru vilivyo ndani ya mwili wa mtendaji, vinaweza kuwa ni vikwazo vya kisaikolojia kama vile ni ujinga, woga (phobia); hisia kama vile hasira, chuki, wivu, upendo; upumbavu, yaani urazini hafifu; ugonjwa wa kijenetiki, kama vile ugonjwa wa kutoweza kuona rangi za aina fulani; vikwazo vya kiafya kama vile upofu, ukiziwi, na homa ya malaria inayokufanya ushindwe kwenda kazini.
Kusudi tuelewane, hebu tutumie mifano ya wavuta sigara wawili wanaoendesha magari kwenda kununua sigara kutoka madukani, kila mmoja akiwa anaendesha gari lake.
Katika mfano wa kwanza, tuseme kwamba dereva mmoja yuko huru, tukiwa tunamaanisha kuwa, dereva yuko huru dhidi ya vikwazo vilivyo nje ya mwili wake, kama vile trafiki au alama za barabarani zinazoweka ukomo wa kasi ya gari, kufanya anachotaka au kwenda anakotaka kufika.
Katika mfano wa pili, tuseme kwamba dereva mwingine hayuko huru, tukiwa tunamaanisha kuwa, dereva hayuko huru dhidi ya vikwazo vilivyo ndani ya mwili wake, yaani ujinga unaomzuia kujua kwa ufasaha ni duka gani linauza aina ya sigara anayoitaka.
Kwa upande mmoja, mifano hii miwili inafanana katika jambo moja kubwa. Yaani, katika kila mfano kuna kipengele cha uhuru chanya na kipengele cha uhuru hasi. Uhuru chanya ni uhuru wa mtendaji dhidi ya vikwazo na uhuru hasi ni uhuru wa mtendaji kuwa anavyotaka au kufanya anachotaka.
Na kwa upande mwingine, mifano hii miwili inatofautiana katika jambo moja kubwa. Jambo hilo linahusu mahali viliko vikwazo vilivyombana mtendaji.
Katika mfano wa kwanza, kuna vikwazo vya uhuru vilivyo nje ya mwili wa mtendaji, wakati katika mfano wa pili kuna vikwazo vilivyo ndani ya mwili wa mtendaji.
Nje ya mwili wa dereva kuna binadamu ambaye ni trafiki, vitu kama vile alama za usalama zinazotamka ukomo wa kasi ya gari au makorongo. Kwa ujumla, vikwazo vya uhuru vilivyo nje ya mwili wa mtendaji vinaweza kuwa ni maamuzi na matendo ya watu baki kama vile trafiki, vitu vilivyotengenezwa na binadamu kama vile alama za barabarani, na vitu asilia kama vile makorongo na mafuriko.
Na kwa upande mwingine, ndani ya mwili wa dereva, kuna kikwazo cha ujinga wake, ambalo ni tatizo la kisaikolojia.
Kama hii ndio tofauti kati ya “uhuru” na “utumwa” swali linafuata: Je, katika Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini Tanzania kuna uuru kiasi gani na kuna utumwa kiasi gani?