Uzi maalum wa kupeana Likes: Comment chochote upate "Like"

Katika miezi ya mwanzo, watu wetu wa nyumbani wakiruhusiwa kuja kutuona kila baada ya muda fulani, na pia tulikuwa tukiruhusiwa kuletewa chakula kutoka majumbani kwetu. Lakini hayo hayakuendelea kwa muda mkubwa, ila yote yalipigwa marufuku. Kwanza watu wa "Msalaba Mwekundu" walikuwa wakiruhusiwa kuja kutukaguwa na baadae na wao pia walipigwa marufuku. Karume na kundi lake la Baraza la Mavamizi, walikuwa kila baada ya muda waliokuwa wakikutana wenyewe, wakija gerezani kwa kuwatoa wawatakao.
 
Mwendo ulikuwa kama hivyo mpaka kufika taarikh mosi Januari, 1965 yaani mwaka mmoja tokea kutokea hayo yenye kuitwa 'mapinduzi', wananchi wengi waliyokuwa wamewekwa magerezani na waliyokuwepo viziwizini vyengine walikuwa wamesha achiliwa huru. Wachache, na mimi nikiwa miongoni mwao ndio waliyokuwa wamebakia kiziwizini gerezani kwa "kuhifadhiwa usalama wao", kama walivyokuwa wakisema wakuu wa Serikali ya 'mavamizi'.
 
KUFUNGWA KIFUNGO CHA MIAKA 10 GEREZANI
Taarikh 1 Januari, 1965 kiasi ya saa nne za asubuhi, Karume Raisi wa Serikali ya Mavamizi ya Zanzibar akifuatana na wenzake wa Baraza lake la Mavamizi walikuja gerezani. Walipofika walitukuta sisi wachache tuliyokuwa tumebakia kiziwizini tumesimama kwa kungojea kwa matumanio makubwa sana ya kuachiliwa huru kama walivyo achiliwa wa kabla yetu.
 
Alipofika mbele yetu, Karume alisema, "Leo tumekuja kuwaachilia huru wote waliyokuwa wamewekwa humu ndani kuanzia siku za mwanzo za mapinduzi". Kiasi ya kusema hivyo tu, tuliwaona baadhi ya waongozi wa Baraza la Mavamizi, wakiwemo Ibrahim Mbwana (Ibrahim Makungu), Said Natepe, Seif Bakari na Khamis Darwesh wamevutana upande na wakinon'gonezana.
 
Baadae walimnon'goneza Karume; na hapo hapo mpira uligeuzwa kuelekea upande mwengine. Tuliona tunatolewa mmoja mmoja na kuwekwa upande mpaka tulitimia watu 25. Karume na kikosi chake waliondoka na kutuacha sisi watu 25 upande mmoja na wenzetu wengine wachache waliachwa upande wao. Baada ya muda alitujia Ofisa wa Gereza, Bwana Oliver Fernandes akifuatana na sajini (sergeant) Nyankabwa pamoja na askari wao wawili. Oliver alikuwa akitwambia na huku ameinamisha uso wake chini kwa kutuonea taabu kututizama kwa namna alivyokuwa akiona dhulma na unyonge tuliyopitishiwa ambao tokea kuanza kwake kazi hajapata kuuona wala kuusikia.
 
Alisema kutwambia,
"Baraza la Mapinduzi, limeamua kukufungeni gerezani kifungo cha miaka 10 kwa kila mmoja wenu kuanzia hii leo Januari 1, 1965"! Kila mmoja kati yetu kwa kusikia hayo, alitokwa na kijasho mwilini mwake. Hapana hata mmoja aliyetarajia kuwa yataweza kutokea mambo kama hayo ya kufungwa bila ya kuwa na makosa na bila ya kupelekwa mbele ya mahakama. Sisi watu 25 ndio watu wa mwanzo katika taarikh ya visiwa vya Zanzibar kufungwa gerezani bila ya kutenda kosa lolote na bila ya kuhukumiwa.
 
Ulimwengu unafaa umuulize Mwalimu Nyerere na hao wenye kujiita "progressives", kuwa huko ndio kuondoa dhulma na unyonge na kuleta usawa na demokrasi? Hao Masultani na Mamwinyi, waliwahi kutenda hata nusu ya hayo mliyoyetenda nyie katika huo utawala wenu? Tulinyolewa vipara na tulipewa nguo za kifungwa, nguo zetu, na kila kilichokuwa chetu, kilichukuliwa na kuwekwa katika 38 dhamana ya gereza. Ni shida kueleza hali zetu zilivyokuwa siku hiyo hata ikafahamika.

Tulikuwa tukilia bila ya kutokwa na machozi, na tulikuwa tukitizama na ilhali tulikuwa hatuoni kitu. Tulikuwa tukisema na ilhali ilikuwa hatukijui nini tukisemacho. Mwenzetu mmoja Sheikh Mohammed Rajab (Machungwa) alipindukwa na tumbo la kuhara damu kwa uchungu wa kudhulumiwa maisha bure.
 
[emoji818][emoji818]
 
Yafuatayo ndio majina ya hao wadhulumiwa 25 tuliofungwa miaka 10 gerezani bila ya makosa na bila ya kupelekwa mbele ya mahakama: Suleiman Sultan Malik Hassan Usi Walid Fikirini Ali Issa Ali (Mataa) Mohammed Rajab (Machungwa) Haji Hussain Ahmed Yahya Mohammed Ali Shambe Hussain Bachu Ramadhan Khamis Shariff AbdulRahman Othman Mzee Maalim Mwita Rashid Mohammed Marjeby Ali Raza Nathani (Ali Bomu) Omar Hamad (Mkame Ndume) Sheha Abdulqadir Thiney Sheha Suleiman Khamis Ali Mohammed Suleiman Wazir Ali bin Maalim Mzee Ismail Salim Said Halua Nasser Mohammed Husein Jessa Bhaloo Ali Mdungi Ahmed Abdulqadir (Qullatain) Aman Thani Fairooz
 
Kwa hakika siku hiyo ilikuwa ni siku ngumu sana katika maisha yetu. Tulishindwa kula na tulikesha usiku kucha bila ya kufumba jicho hata muda mdogo. Kulipokucha siku ya pili taarikh 2 Januari 1965, baada ya kupewa uji wa sembe na chembe mbili tatu za maharagwe, tulipelekwa kuonana na Mkuu wa Magereza.

Wakati huo alikuwa Bwana Kilonzi. Lakini, aliyetukabili alikuwa Bwana Oliver Fernandes, msaidizi wake. Oliver alitupa Daftari kubwa lenye kuwekwa majina ya wafungwa pamoja na makosa yao na muda wa vifungo vyao. Tulipo litupia jicho, tuliyaona majina yetu yamesha andikwa pamoja na makosa yetu na mahakama yaliyotuhukumu na hakimu aliyetuhukumu na muda wa vifungo vyetu. Maelezo ya hukumu ya kufungwa kwetu huko kama yalivyoandikwa katika Daftari hilo yalikuwa kama hivi:
 
Baada ya hapo, tuliondolewa katika gereza hilo la mjini na tulipelekwa kwenye gereza la shamba, Langoni. (Langoni ni kiasi cha maili 10 kutoka mjini). Wakati wa kikoloni, mfungwa yoyote ilikuwa hafanyishwi kazi ya namna yoyote mpaka kwanza aangaliwe na Daktari mwenye ujuzi (sio muuguzaji) kukhusu siha yake. Na uamuzi wa Daktari ndio uliyokuwa ukifuatwa juu ya namna za kazi zinazomfalia mfungwa fulani kuzifanya kutokana na siha yake.

Serikali ilipoingia watawala wenyekujiita, "wapigania haki za wanyonge na waleta usawa kwa wote", hapo hapo mambo yote yalibadilika ikawa wagonjwa, wazima, wadogo, wakongwe na hata walemavu, wote walifanyishwa kazi kwa kulazimishwa, tena bila ya kuangaliwa laa na daktari walaa na muuguzaji.
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…