Wataalamu wa Afrika wamepongeza nafasi ya China katika kuendeleza haki ya maendeleo katika bara zima la Afrika, wakisisitiza namna inavyoheshimu njia ya kipekee ya maendeleo ya kila nchi.
Hayo yameejiri wakati Semina ya Kwanza ya Haki za Binadamu kati ya China na Afrika ilifanyika Ijumaa huko Addis Ababa, nchini Ethiopia, ikiwa chini ya kaulimbiu "Kujenga jumuiya ya China na Afrika yenye mustakabali wa pamoja na kufanya kazi pamoja ili kufikia haki ya maendeleo."
Semina hiyo iliwaleta pamoja zaidi ya watunga sera 200, wanazuoni, wanadiplomasia, na wawakilishi wa vyombo vya habari kutoka China na Afrika kwa minajili ya kuchunguza njia za kuendeleza haki za binadamu, hasa haki ya maendeleo.
Katika mahojiano na Xinhua, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Urafiki ya Zambia na China, Fredrick Mutesa, amesema China inaendelea kushirikiana na Afrika na Dunia ya Kusini ikiheshimu muundo wa utawala wa kila nchi na njia ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
"China inatoa fursa ya kweli kwa bara la Afrika kujadili upya ushiriki katika utaratibu wa kimataifa unaozingatia kutoingilia masuala ya ndani ya kila mmoja, kuheshimiana na kupata matokeo ya kunufaishana. Katika suala hilo, China ina jukumu muhimu sana katika kuisaidia Afrika kutambua haki ya maendeleo," Mutesa aliiambia Xinhua.
Mtaalamu huyo alitoa wito wa kufanya juhudi za pamoja kati ya wasomi wa Afrika na China na washauri bingwa ili kuandaa mkakati mpana wa kulinda manufaa ya ushirikiano wa Afrika na China.
"Huwezi kuwa na bara ambalo zaidi ya watu milioni 300 wanakumbwa na njaa, na sasa hivi tumesaliwa na miaka michache tu kufikia ukomo wa lengo la 2030 la kumaliza njaa," alisema. "Ni muhimu tuzungumze kuhusu haki ya maendeleo na pia kuangalia nani anashirikiana na Afrika kuweka mazingira mazuri ya kupatikana kwa haki hii."
"China iko mstari wa mbele katika kuwekeza katika masuala ya kufungua uwezo wa bara la Afrika kupitia maendeleo ya miundombinu na sekta nyingine za uchumi," aliongeza.
Balew Demissie, mtafiti katika Taasisi ya Mafunzo ya Sera ya Ethiopia, aliunga mkono maoni ya Mutesa, akisisitiza jukumu la China katika kukuza mitazamo anuai ya haki za binadamu huku ikiheshimu njia ya kipekee ya maendeleo ya kila nchi.
"China inatetea ushirikiano wa haki za binadamu unaozingatia kuheshimiana, usio wa kisiasa au vigezo viwili. China inaona kuwa masuala ya ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini ni misingi muhimu katika kutambua haki za binadamu, hasa katika mataifa yanayoendelea," Demissie alisisitiza.
Akizungumzia mchango chanya wa China katika kukuza haki ya maendeleo ya Afrika katika majukwaa mbalimbali ya nchi mbili na kimataifa, mwanazuoni huyo alisema China inaunga mkono mageuzi katika taasisi za kimataifa ili kupaza sauti za nchi za Dunia ya Kusini na kuunga mkono uhuru wa taifa.