6 Wale makuhani wakuu na viongozi wa Wayahudi walipomwona wakapiga kelele, “Msulubishe! Msulubishe!” Pilato akawajibu, “Mchukueni mumsulubishe ninyi, kwa sababu mimi sioni kosa alilo tenda.” 7 Wao wakamjibu, “Sisi tunayo sheria ambayo inamhukumu kifo kwa sababu yeye anajiita Mwana wa Mungu.” 8 Pilato aliposi kia haya aliingiwa na hofu. 9 Akaingia ukumbini tena akamwuliza Yesu, “Wewe unatoka wapi?” Lakini Yesu hakumjibu. 10 Pilato akamwambia, “Kwa nini hunijibu? Hujui ya kuwa nina mamlaka ya kukuachilia huru au kukusulubisha?” 11 Ndipo Yesu akamwambia, “Wewe hungekuwa na mamlaka ye yote juu yangu kama Mungu hakukupa mamlaka hayo; kwa hiyo mtu aliyenishtaki kwako ana dhambi kubwa zaidi.” 12 Tangu wakati huo Pilato akaanza kutafuta njia ya kumfungua Yesu, lakini Wayahudi wakazidi kupiga kelele wakasema, “Ukimwachilia huyu mtu, wewe si rafiki wa Kaisari. Mtu ye yote anayejifanya kuwa mfalme anampinga Kaisari.” 13 Pilato aliposi kia maneno haya alimtoa Yesu nje tena akaketi katika kiti chake cha kuhukumia, mahali palipoitwa Sakafu ya Jiwe - kwa Kiebrania paliitwa Gabatha.