Msanii wa Bongo Fleva nayefahamika kwa jina la Abdulaziz Abubakari (30) maarufu kama Dogo Janja, ambaye kwa sasa anagombea Udiwani katika kata ya Ngarenaro Jijini Arusha, anadaiwa amemjeruhi mwanafunzi kwa risasi
kwa tuhuma alitaka kumvamia akiwa anashuka kwenye gari Jijini humo.
Familia ya mwanafunzi huyo aliyetambulika kwa jina la Bakari Halifa (19) anayesoma kidato nne katika shule Sekondari Sombetini Jijini humo, ikizungumza na vyombo vya habari Agasti 24, 2025, imesema majira ya usiku Agasti 23, 2025 wakiwa nyumbani, ilisikika milio ya risasi mara tatu na kelele za watu, na walipotoka nje walikuta mwanafunzi huyo akiwa anatokwa damu nyingi mguuni.
Aidha, Familia hiyo imesema kuwa mwanafunzi huyo akiwa na wenzake wakielekea kula chakula kwa ndugu yao aliyepo jirani na kwa babu yao, walikutana na msanii huyo sehemu ambapo amekuwa akionekana kuja mara kwa mara, ndipo tukio hilo likatokea kwa madai walitaka kumvamia Msanii huyo.
Kwa upande wa Jeshi la Polisi mkoa wa Arusha, limethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema tukio hilo limetokea Agasti 23, 2025 majira ya saa tano na nusu usiku, wakati Msanii huyo akiwa anashuka kwenye gari na kutaka kuvamiwa na vijana hao kwa silaha za jadi, na msanii huyo kufyetua risasi huko katika kata ya Sombetini Jijini humo.
Mmoja wa kijana aliyekuwa ameongozana na mwanafunzi huyo ameiambia GADI TV kuwa hawakua na nia kumkaba msanii huyo bali walikuwa wanaelekea kula chakula kwa ndugu yao kama ilivyo utaratibu wao wa mara kwa mara kwenda kula chakula mahali hapo.
Kadhalika, Jeshi la polisi limesema limewashikilia watu wawili kwa ajili ya uchunguzi wa tukio hilo.
Hata hivyo GADI TV tumemtafuta Msanii huyo kwa njia ya simu, na mara baada ya kupokea simu yetu na kusikia kuwa ni mwandishi wetu amepiga simu hiyo mawasiliano hayo yalikatika upesi, na hata alipopigiwa kwa mara nyingine hakupokea tena.