Yericko,
Haitapendeza kwangu mimi nishindane na wewe kuhusu kitabu chako.
Uungwana unanikataza.
Kitabu kipo na kama mimi nitafanya, ''critique,'' yoyote basi iwe ya kisomi
isiwe kuishambulia kazi yako.
Kama kweli ''umechimba,'' historia ya mapinduzi hilo ni jambo jema na
wa kulisemea hilo si mimi na wewe bali ni wasomaji wa kitabu chako na
watakaokufanyia ''book review.''
Nasubiri kusoma ''reviews,'' za kitabu kama ninavyongoja kuona na kusoma
habari mpya za mapinduzi ambazo unasema Dr. Ghassany hakuziona katika
utafiti wake.
Ghassany alikuja na Mohamed Omari Mkwawa na Victor Mkello na kina
Lumumba, Aboud Mmasai na hawa wote picha zao na sauti zao zipo katika
Maktaba kwa ajili ya rejea kwa watafiti wengine siku za usoni.
Ghassany kaja na Kipumbwi, kambi ya askari mamluki waliovushwa kuingia
Zanzibar kusaidia mapinduzi.
Habari hii ya Wamakonde kutoka mashamba ya mkonge ya Sakura ambayo
haikufahamika toka mwaka wa 1964 ikaja kusomwa mwaka wa 2010 katika
kitabu cha Dr. Ghassany baada ya miaka 46 kupita.
Vumbi la habari hizi kila msomaji wa kitabu kile analijua.
Ikiwa wewe kitabu chako kina mambo zaidi ya hayo utakuwa umefanya kazi
kubwa sana ya kupigiwa mfano na itasaidia sana kukitangaza kitabu chako
kama utaeleza haya yakafahamika.
Nakushauri usiache kuonyesha na kueleza mambo kama haya ili wasomaji
wavuitiwe na ukweli uliokujanao katika kitabu chako hiki.
Itakuwa vizuri sana kama hawa wasomi wanaopendekeza utunukiwe shahada
kwanza kabla ya hayo wao kwa usomi wao ungewaomba waandike ''review,''
ya kitabu chako ili wasomaji wajue nini umeeleza katika kazi hii yako.
Nionavyo mie si busara mathalan kwa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam au chuo
chochote kile kuanza kukupa shahada kabla ya kuonyesha kwanza uzito wa kazi
yako au hata kabla kitabu hakijaandikiwa, ''reviews'' na kuchapwa katika majarida
kama Cambridge Journal of African History.
Kweli unastahili sifa kubwa sana kuwa kitabu ni cha Kiswahili lakini kinasomwa
dunia nzima na watu ambao hawajui Kiswahili.
Unastahili sifa sana kwani hiki ulichofanikiwa wewe si kitu kidogo.
Nakueleza haya kutoka moyoni kwangu kwani mimi kama mtu wa vitabu naujua
vizuri ugumu uliopo katika biashara ya vitabu hasa kitabu kilichoandikwa na
mwandishi ambae hajawahi kuandika kitabu.
Umenishauri niandike kitabu nipinge kitabu chako.
Sidhani kama hili ni jambo la busara kwani huwezi kuandika kitabu juu ya kitabu.
Hakuna ''publisher,'' atakaegusa mswada kama huo kwa kuwa somo nimeshaliandika
na kitabu kipo.
Kitabu chako wewe kimekuja nyuma ya kitabu changu kwa takriban miaka 20.
Ninachoweza kufanya ni mimi kufanya ''book review,'' ya kitabu chako.
Hili ndilo muhimu na nitakuwa khasa mtu ninaestahili kufanya "review" kwa kuwa
hili somo la mapinduzi na uhuru wa Tanganyika nalijua vyema.
Hivi ndiyo baadhi ya vitu mwandishi anatakiwa awe anavijua kuepuka makosa ambayo
si ya lazima.
Umenishambulia kwa kuniita mvivu na mtu mwenye wivu.
Sidhani kama hizo sifa zinanienea mimi.
Ama hili la ''porojo,'' waliokuwa katika haya mambo ya utafiti na uandishi na baadhi ya
vyuo vikuu na taasisi nyingine za elimu ambao tumefanyakazi pamoja aidha kwa kuhariri
au kuandika au nilkopita na kufanya mihadhara kwenye vyuo vyao nadhani wananijua
kuwa mimi si mvivu wala si mpiga porojo.
Lakini akutukanae hakuchagulii tusi.
Inawezekana nina kasoro kama ilivyo kawaida ya binadamu yoyote, kakini hii sifa ya uvivu
si sifa yangu.
Napenda kuhitimisha kuwa kusema kuwa umeifanyia nchi yetu hisani kubwa kwa kuandika
historia ya TANU na mchango wa Jesuits katika historia hiyo.
Sasa tuna historia tatu za TANU.
Historia ya Chuo Cha Kivukoni, historia hiyo yako ya Jesuits na historia mnayoijua ya TANU
na uhuru wa Tanganyika niliyoandika
kama nilivyopokea kutoka kwa wazee wangu.