Mkutano mkuu wa Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) umemalizika hivi karibuni mjini Beijing, ambapo dunia nzima inaendelea kufuatilia kwa karibu mambo yaliyojadiliwa kwenye Mkutano huo. Xi Jinping alitoa hotuba muhimu kwenye ufunguzi wa mkutano huo, ambayo kimsingi imetaja msingi wa kazi zilizofanywa na chama katika miaka mitano au zaidi iliyopita, na msingi wa kazi zitakazofanywa katika ujenzi wa nchi.
Inawezekana kuwa Mkutano huu ni Mkutano Mkuu wa CPC unaofuatiliwa zaidi duniani kuliko mikutano kama hiyo iliyotangulia. Sababu kubwa ni kwamba Mkutano huu unafanyika wakati nguvu ya uchumi wa China na mchango wake kwa dunia inajulikana wazi, na wakati ambapo sauti ya China katika jukwaa la siasa za dunia haiwezi kupuuzwa. Kwa hiyo kufuatilia mkutano huu, ni jambo la muhimu na lazima kwa mdau yeyote wa uchumi au mahusiano ya kimataifa.
Pamoja na kuwa kuna vyama vingi vikubwa vya siasa duniani, Chama cha Kikomunisti cha China kina utofauti na vyama hivyo kwa sababu ni chama ambacho kimeshika hatamu za uongozi wa taifa kubwa, na uongozi wake umefungamana moja kwa moja na uongozi wa taifa. Hali hii inafanya mambo ambayo yangeweza kutajwa kuwa ni mambo binafsi ya chama, si binafsi tena kutokana na matokeo yake kugusa sehemu kubwa na nyeti ya dunia.
Kwenye hotuba ya ripoti ya majumuisho ya kazi za chama iliyotolewa na Xi Jinping kwenye ufunguzi wa mkutano huo, wananchi na taifa wameonekana kuwa ni walengwa wakuu wa kazi zote zilizofanywa na Chama. Kuanzia kutekeleza mageuzi kwa kina, kujenga jamii ya kijamaa yenye neema na kupambana na umaskini uliokithiri, yote haya undani wake ulikuwa ni katika kuhakikisha mwananchi wa kawaida wa China anawekewa mazingira ya kuishi maisha bora na yenye neema.
Ripoti pia ilitaja mambo mengine muhimu yaliyofanywa na chama ambayo matokeo yake yamesaidia kuifanya China iwe nchi yenye nguvu zaidi na yenye ushawishi zaidi duniani. Kwa sasa China ni nchi ya pili kwa nguvu ya uchumi duniani, na matokeo haya yanatokana na uongozi imara wa Chama cha Kikomunisti cha China. Matokeo hayo yamewezekana licha ya changamoto mbalimbali zilizotokea katika kipindi cha miaka 10 iliyopita. Cha muhimu zaidi iliyotajwa katika ripoti hiyo ni kushikilia uongozi wa chama na ujamaa wenye umaalum wa China, na kutafuta maendeleo ya kiwango cha juu.
Dunia nzima ni shahidi wa matokeo ya kazi za Chama cha Kikomunisti cha China katika kuwaletea maendeleo wachina, na kuimarisha nguvu ya uchumi wa China. Ni kweli pia kuwa katika miaka iliyopita China imekuwa ikigusa maisha ya watu wengi wa nje ya China kwa njia moja au njia nyingine. Kwa sasa moja ya changamoto kubwa ambayo inagusa binadamu wote duniani ni suala la mabadiliko ya tabia nchi. Kwenye hotuba yake Xi amerudia ahadi ya China kuwa itaweka uwiano kati ya maendeleo ya binadamu na mazingira, wakati ikiweka mipango ya maendeleo. Amekumbusha kuwa China itaunga mkono viwanda au sekta zenye utoaji mdogo wa hewa ya carbon, kuhakikisha hali ya kuwepo kwa mifumo anuai ya ikolojia, kutafuta mapinduzi ya nishati, na kuhimiza matumizi ya makaa ya mawe yenye ufanisi na yasiyosababisha uchafuzi wa mazingira.
Xi Jinping kurudia ahadi ya China kuhusu kukabiliana na tatizo la uchafuzi wa hewa, ni kuthibitisha kuwa kazi zitakazofanywa katika miaka mingine mitano, sio tu itaendelea kuzingatia maslahi ya walio wengi nchini China, bali pia itazingatia maslahi ya walio wengi duniani.