Kampuni ya nchini Misri inayomilikiwa na serikali, Arab Contractors imeshinda tenda ya kubuni/kusanifu na kujenga bwawa la Stiegler's Gorge katika maporomoko ya mto Rufiji.
Baada ya Kampuni hiyo kushinda tenda, Rais wa Misri, Abdel-Fattah al-Sisi amempigia simu Rais Magufuli na kutoa shukrani huku akimwambia kama atamkaribisha atapenda kuhudhuria katika sherehe ya uwekaji wa jiwe la Msingi la ujenzi wa bwawa hilo kuonyesha mahusiano ya karibu ya kiuchumi kati ya nchi yake na Tanzania.
Rais Abdel-Fattah al-Sisi aliwahi kutembelea Tanzania mwaka 2017. Kabla ya Al Sisi, Rais wa mwisho kutoka Misri kuitembelea Tanzania ilikuwa mwaka 1968.
Kampuni ya Al Moqaweloon Al Arab iliyoshinda tenda inasifiwa kwa kazi mbali mbali za ujenzi ambazo inazifanya hasa katika nchi nyingi za Mashariki ya Kati na barani Afrika.
Hii ni kampuni ambayo imejenga bwawa linaloitwa Aswan high dam mwaka 1970 ambalo liko nchini Misri. Bwawa hili liligharimu zaidi ya US $1 bilioni.
Inakadiriwa bwawa la Stiegler's Gorge likimalizika kujengwa litatoa umeme wa zaidi ya 2,100 MW. Kwa sasa Tanzania ina uwezo wa kuzalisha umeme wa 1,540 MW nchi nzima.